Kwa ufupi
Ataka watu waseme kama Tanzania haina mtu mwenye sifa ya kuwa Rais au la ili nafasi hiyo ifutwe
“Kama mnaona hakuna mtu anayefaa kuwa Rais mseme
mapema ili hiyo nafasi ikiwezekana ifutwe na la, mkiona yupo anayefaa
kuwa Rais, mjue kuna mambo atayafanya kama Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
na hili halina ubishi jamani.”
Hii ni kauli ya Mwenyekiti wa Timu ya Wajumbe wa
Tume ya Taifa ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akitoa
ufafanuzi wa Rasimu ya Katiba kwa wajumbe wa Baraza la Katiba la
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini.
Profesa Kabudi alitoa kauli hiyo baada ya kuzuka
malumbano miongoni mwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuhusu mamlaka ya
Rais yaliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwenye rasimu hiyo
ya awali.
Aliendelea “Mbona mna wasiwasi sana na hii nafasi
ya Rais? Jamani naomba muiamini Tume na msiwe na hofu na madaraka ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano yaliyopendekezwa katika hii Rasimu ya Katiba
ambayo mtaenda kuijadili hapa na kutoa maoni yenu.”
Mwenyekiti huyo anasema kuwa tume imeangalia mbali
na kupendekeza Serikali tatu ambapo katika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano, imependekeza afanye mambo machache ambayo ni ya Muungano tu
na siyo mambo madogo kama ilivyokuwa awali.
Alisema katiba ya sasa imekuwa ikimpa Rais
madaraka makubwa mno ambayo mengine amekuwa akiyafanya na kujikuta
yanamtia doa yeye Rais moja kwa moja, huku makosa yakiwa yamefanyika
chini kwa watendaji waliopo.
“Mnajua hivi sasa kuna baadhi ya mambo ambayo Rais
amekuwa akipata doa kwa sababu tu katiba imemvisha moja kwa moja kama
mtendaji. Kwa mfano masuala ya kudorora elimu nchini na mengineyo
yamemchafua, lakini sasa katika hii rasimu, Tume imependekeza yeye
kushughulika na mambo ya Muungano tu hayo mengine ya elimu, barabara,
zahanati yatamhusu mtu mwingine,” alisema Profesa Kabudi.
Ametaja baadhi ya madaraka na majukumu ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano kuwa ni pamoja na kuwa Amiri Jeshi Mkuu, kusimamia
na kulinda katiba, kulinda utaifa wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
kuteua mabalozi na kuteua Mwanasheria Mkuu.
Akiendelea kutoa ufafanuzi wa hoja za wajumbe hao,
mwenyekiti huyo ameongeza kwa kuwataka wananchi wasiangalie madaraka
bali waangalie uwakilishi wa maendeleo.
Aidha amewataka wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
wilayani humo kutoa maoni yao waliyotumwa na wananchi na siyo vyama vyao
kwani wao hawajafika kwenye vikao hivyo kwa sura ya vyama bali
uwakilishi wa wananchi wa maeneo wanakoishi.
chanzo: Mwananchi news paper
chanzo: Mwananchi news paper