Kwa ufupi
Kutokana na hali hiyo, ni wakati mzuri kwa Rais
ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kuwakamata mafisadi wizarani, mikoani,
wilayani hadi vijijini.
Kutokana na hali ya ufisadi nchini ilipofikia
sasa, kwa maoni yangu ipo haja kwa Rais Jakaya Kikwete kuwatuliza
Watanzania kwa kutenda jambo ambalo halijawahi kutokea kwa kipindi
kirefu.
Watanzania wengi wanaamini kwamba Rais Kikwete ni
muumini mzuri wa dini, anajali hali za watu, ni kiongozi makini, lakini
wanakata tamaa kutokana na kasi ya ufisadi inavyozidi kushika kasi
katika Serikali yake.
Ufisadi kwenye halmashauri nchini sasa unatajwa
kuwa ni kama chama kikuu kilichojipanga kuiangusha Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Pamoja na wakurugenzi wengi wa halmashauri kushughulikiwa, lakini ukweli ni kwamba ufisadi umekithiri serikalini.
Kutokana na hali hiyo, ni wakati mzuri kwa Rais
ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kuwakamata mafisadi wizarani, mikoani,
wilayani hadi vijijini.
Rais achukue hatua ikiwamo ya kuwataka warudishe
fedha zote ndani ya muda maalumu. Wakabidhi kwa serikali ‘mahekalu’ yote
yaliyojengwa kwa ufisadi. Pamoja na kwamba wamejenga kwa majina ya
watoto, wajukuu na hata ndugu wengine, lakini wajisalimishe na kujieleza
ni jinsi gani walivyopata fedha.
Kwa wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi mpya, Rais
aseme neno likiwamo la kuwataka wajibu hadharani mbele ya Watanzania
kupitia vyombo mbalimbali vikiwamo vya habari na hatimaye kuwapeleka
kortini.
Ikumbukwe, Watanzania wengi wanaipenda Serikali iliyoko madarakani.
Watanzania wamesikia mambo ya watumishi wa
Serikali kukamatwa na nyara, mambo ya Bandari, Mambo ya Wizara ya Mambo
ya Nje, ufisadi ujenzi wa barabara ambako ufisadi umesababisha gharama
za ujenzi kuwa kubwa. Kilometa moja ya lami sasa inakaribia Sh1 bilioni
bila sababu za msingi.
Wizi mwingine wa mafisadi sasa ni wa maandishi kwa
kuongeza cha juu kuanzia Sh100 milioni na kuendelea hadi mabilioni.
Viongozi waliopewa dhamana wanapokubali kila kitu wanachoambiwa na
wataalamu wao hususan masuala ya fedha, ni wazi wanaruhusu ufisadi.
Kikwete atoe neno sasa.
Taarifa za ufisadi zinaripotiwa kuanzia wizarani,
mikoani, halmashauri hadi vijijini. Hata mwanasheria mkongwe wa
kimataifa, Nimrod Mkono anaamini kwamba asilimia 60 ya fedha za Serikali
kwa ajili ya kununua madawati zinaishia kwenye mikono ya watu binafsi.
Rais kamata wanaotajwa kuhusika.
Mkono alinukuliwa na gazeti hili akisema ufisadi
kwenye fedha za Serikali ni balaa. Kwa hali hiyo Rais anaweza kuwatuliza
Watanzania kama atatenda lolote zito dhidi ya watu wanaotuhumiwa.
Mwananchi news paper
Mwananchi news paper