Kwa ufupi
- Wakati watu wakijipongeza kama vile sote tulikuwa kwenye mkabiliano ule yakaandikwa kwenye ubao mkubwa uwanjani pale maandishi makubwa yaliyokuwa yakimeremeta meremeta “A WORLD RECORD – 3.32.16”.
Kwenye makala zake hizi, Tido Mhando, ambaye
amefanya kazi ya utangazaji kwa muda mrefu anasimulia baadhi tu ya mambo
ya kusisimua aliyowahi kukutana nayo wakati wa hizo enzi zake. Wiki
jana alielezea mwanzo wa mbio maarufu za mashindano ya riadha za mita
1,500, kwenye Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974, huko
Christchurch, New Zealand, ambapo Filbert Bayi wa Tanzania alikuwa
mshiriki nyota na yeye Tido akiwa mwandishi wa habari wa Radio Tanzania
Dar es Salaam (RTD), kwenye michezo hiyo. SASA ENDELEA...
Naam, Filbert alikuwa amefyatuka kweli kweli tangu
mwanzo tu wa mbio hizo, akiwa na dhamira ya wazi wazi kuwa hakuna
ambaye angeweza kumkamata, hata miongoni mwa wale wapinzani wake wakuu
wawili, John Walker wa New Zealand na Ben Jipcho wa Kenya.
Kinyang’anyiro hiki kilinitia kiwewe na
kuniogopesha kupita kiasi, hadi kunifanya nikimbilie chooni. Nilidhani
huko nitasalimika, nijifiche hadi mwisho, ili nikitoka iwe kazi
imekamilika, nifahamishwe tu nani kashinda na nani kashindwa, kwani kwa
hakika, hali yangu ya mwili ilikuwa mbaya mno!
Lakini kumbe hatua hiyo haikuweza kusaidia kitu,
maana mlipuko wa kelele na mayowe yaliyokuwa yakivuma yalikuwa yakiingia
hadi huko nilikokuwa. Na jinsi muda ulivyokuwa ukisonga mbele, ndivyo
kelele hizo zilivyozidi kuvuma.
Wakati nikiwa natafakari hili na lile, akili zangu
zikanirudia, na kukumbuka ya kuwa kazi kubwa na muhimu kuliko zote
iliyonifanya nije New Zealand ilikuwa ni ya kutangaza mchezo huo, mbio
za mita 1,500 uliokuwa ukifanyika wakati huo. Nikajiambia kwamba
nilikuwa na wajibu mkubwa wa kuwafahamisha Watanzania hali halisi ya
pambano hilo.
Nikatoka chooni humo mithili ya kifaru
aliyejeruhiwa, nikikimbia kulingana na ongezeko la mayowe ya uwanjani
yalivyokuwa yakiendelea kurindima. Nilijua sasa mambo yalikuwa yameiva
zaidi na kwa kweli, yalikuwa yanakaribia nchani, kwenye mduara wa
mwisho.
Lahaula! Macho yangu yalipoona tu mwanga
yakakutana na kitimbi cha kutisha zaidi. Filbert Bayi bado alikuwa mbele
lakini mahasimu wake Walker na Jipcho walikuwa kama wanaoruka wakiwa
kwenye kasi ya mfano wa radi inayojirudiarudia. Zilikuwa zimebakia kama
mita 300 tu!
Kila binadamu aliyekuwepo uwanjani pale alikuwa
wima, halikuwa tukio la mtu kuweza kutulia kimya ama kuketi. Halikuwa
jambo la hali ya mtu kulaza damu, hata kama hukuwa mshiriki pale
kiwanjani. Sote tulitimbilika na jasho kututoka vilivyo.
Sasa mvuto wangu zaidi uliegemea kwa wale jamaa
wawili Jipcho na John Walker, waliokuwa wamepania kutunyang’anya tonge
mdomoni mwetu. Niliamua kuwafuatilia wao tu kwani nilijua endapo
watamfikia Bayi, basi macho yangu yataweza kuiona hali hiyo vyema zaidi,
hali ambayo sikuwa nataka kuiona hata kidogo.
La kutisha zaidi ni kwamba miamba hao walikuwa na
uzoefu na ujuzi wa muda mrefu kwenye mbio hizi ukilinganisha na ule wa
nyota wetu. Sasa zikiwa zimebakia mita 100 tu; Bayi bado alikuwa mbele
na wala hakuonyesha dalili yoyote za kuchoka. Ilionekana alikuwa kwenye
dhamira ya kufa na kupona, lakini wenzake nao walikuwa wanamkaribia
zaidi na zaidi.
Kwa muda sasa nilikuwa pia nimewasha kinasa sauti
changu, nikitangaza hatua hizo za mwisho za mbio hizi za kihistoria
lakini hasa nikiendelea kukazia kuhusu mnyemeleo ule wa Jipcho na Walker
kwa Bayi: “Hii ni patashika ya aina yake yenye asili ya ubingwa tena
ubingwa wa dunia!”
“Zimesalia mita 50, Walker, Jipcho lakini bado
Bayi anapepea mbele. Sasa mita ishirini hivi na bado jamani Bayi huyo
yuko mbele tu mama yangu weeeeeee! Mambo bado hawa jamaa hawakati tamaa,
lakini bado Bayi huyoooooooooo anavuka mstari, ameshindaaaaaaaaaa na
tena ni rekodi mpya ya dunia,” nikapiga mayowe ya furaha.
Umati wote ulikuwa kwenye hali ya msisimko mkubwa sana. Tulikuwa
tumeshuhudia jambo ambalo halijawahi kutokea mahali pengine popote
duniani kwenye mashindano ya mbio hizi za mita 1,500. Sote tunaingia
kwenye vitabu vya kumbukumbu kama mashuhuda wakati Mtanzania wa kwanza
anavunja rekodi ya dunia ya michezo ya riadha na si mwingine bali
Filbert Bayi, akiwa kijana wa umri wa miaka 20 na ushei tu.
Wakati watu wakijipongeza kama vile sote tulikuwa
kwenye mkabiliano ule yakaandikwa kwenye ubao mkubwa uwanjani pale
maandishi makubwa yaliyokuwa yakimeremeta meremeta “A WORLD RECORD –
3.32.16”.
Naam, Filbert Bayi akawa ameivunja rekodi ya hapo
nyuma ya dakika 3.33.1 iliyokuwa ikishikiliwa na Mmarekani Jim Ryun
aliyoiweka miaka saba iliyopita kwenye mbio za masafa haya zilizofanyika
Los Angeles, Marekani.
Nilijisikia fahari kubwa kuwepo uwanjani pale siku
sike ile. Nilijisikia fahari kubwa kuwa Mtanzania na zaidi, nilijiona
kuwa mtu mwenye bahati kweli kweli kuwa, ni mimi niliyekuwa nimepewa
dhamana na umma wote wa taifa langu la Tanzania kuwafahamisha kuhusu
tukio hili la kishujaa na kihistoria.
Wakati nikiwa bado natafakari hili na lile, nikiwa
nafikiri jinsi Watanzania watakavyopokea habari hii njema, mara ghafla
nikamwona Filbert Bayi mwenyewe huyu hapa, amekuja hadi pale juu
nilipokuwepo mimi akiwa bado anatweta, anahema huku akiwa anavuja jasho
na kunipa mimi Tido Mhando nafasi ya mwanzo kabisa ya kuelezea furaha
yake isiyo kifani ya kulipatia taifa lake medali ya dhahabu kwenye
michezo mikubwa ya kimataifa ya riadha. Alikuwa mzalendo wa kweli.
Waandishi wengine wote wa kimataifa walipigwa na
butwaa na kupata mshangao. Nilimkumbatia Bayi na kumpongeza na kwa muda
wa dakika kama tatu hivi huku viongozi wa michezo ile wakiwa wanamsubiri
tulifanya mahojiano na bingwa huyu mpya wa dunia.
Haya yakibakia kuwa miongoni mwa mahojiano yangu
muhimu sana kuwahi kuyafanya katika kipindi changu chote cha utangazaji,
ikiwa ni pamoja na yale niliyofanya na Rais mstaafu Benjamin Mkapa
dakika chache tu kabla ya kwenda kuapishwa kwake kuwa Rais wa tatu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mahojiano mengine niliyoyafanya na
Laurent Kabila, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
siku chache kabla ya kupigwa risasi na kuuawa.
Kwenye mahojiano yale, Bayi alielezea jinsi
alivyokuwa amepania kuipatia nchi yake medali ya dhahabu na kwamba
ushindi ule haukuwa wa kwake, bali wa nchi yake. Ni kweli, kwani ushindi
ule uliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya 16 miongoni mwa nchi 32
zilizoshiriki, tukimaliza na medali hiyo moja ya dhahabu na nyingine ya
shaba kwa ushindi wa tatu aliokuwa ameupata Clever Kamanya kwenye mbio
za mita 400. Baada ya Bayi kuondoka, waandishi wengine wengi walinivamia
mimi na kutaka kujua mengi kuhusu yale tuliyokuwa tukiongea tena kwa
lugha yetu ya Kiswahili, na pia kumhusu yeye mwenyewe Bayi na wengine
wakataka kujua mengi kuhusu nchi yangu Tanzania.
Muda mfupi baadaye tangazo muhimu lilitolewa
kwenye vipaza sauti vya hapo uwanjani ya kwamba sherehe ya utoaji wa
medali kwa washindi wa mbio zile za mita 1,500 zilizohitimisha patashika
za michezo ile kwa kuwekwa rekodi mpya ya dunia zinakaribia kufanyika.
Ndipo Filbert Bayi akiwa katikati ya washindani
wake wakuu, John Walker wa New Zealand aliyeshika nafasi ya pili kwa
muda wa dakika 3.32.52 na Ben Jipcho wa Kenya aliyekuwa wa tatu kwa muda
wa dakika 3.35.16 walipoingia uwanjani hapo kwa vifijo na hoi hoi
kubwa.
Halafu ndipo ukafika muda wa fahari kubwa zaidi
kwetu: mara baada tu ya kupokea medali yake ya dhahabu pale jukwaani,
ukapigwa wimbo wa taifa la Tanzania na bendera ya taifa letu
ikapandishwa. Nilisimama kimya na kujiimbia mwenyewe, “Mungu Ibariki
Tanzania…”
Adhuhuri ile baadaye, zikafanyika sherehe za
kusisimua za kufunga michezo hiyo ya Nchi za Jumuiya ya Madola, mgeni
rasmi akiwa Malkia Elizabeth wa Uingereza mwenyewe. Wanamichezo na
viongozi wao waliofikia kiasi cha 1,500 safari hii waliingia uwanjani
pale wakiwa kwenye mavazi yao ya kawaida na kuchangamana kwa pamoja
kuashiria urafiki walioujenga kwenye kipindi cha ushindani mkubwa
viwanjani. Wengine hata walimdhihaki Malkia mwenyewe kwa kudandia nyuma
ya gari lake la wazi. Kuliko wanamichezo wote, wale wa Tanzania walikuwa
wakitamba sana.
Ilipofika saa mbili usiku, ikiwa ni sawa na saa tano mchana Tanzania, siku hiyo ya Jumamosi tarehe 2 Februari, 1974, kama ilivyokuwa kawaida, nilikwenda kutuma ripoti yangu ya michezo hii, lakini safari hii ilikuwa tofauti na siku zilizotangulia. Safari hii, nilikuwa nawapelekea Watanzania habari njema, habari za ushindi.
Ilipofika saa mbili usiku, ikiwa ni sawa na saa tano mchana Tanzania, siku hiyo ya Jumamosi tarehe 2 Februari, 1974, kama ilivyokuwa kawaida, nilikwenda kutuma ripoti yangu ya michezo hii, lakini safari hii ilikuwa tofauti na siku zilizotangulia. Safari hii, nilikuwa nawapelekea Watanzania habari njema, habari za ushindi.
Nilianza ripoti yangu hiyo kwa kucheza kiashiria changu, ule
wimbo wa kitamaduni wa ala tupu za mpigo wa kuonyesha ushindi vitani.
Wimbo ulichezwa na kikosi cha JWTZ. Naam tulikuwa tumeshinda kwenye vita
hivi vya kimichezo na tulikuwa tayari kurejea nyumbani tukiwa washindi.
Niliwafahamisha wasikilizaji wangu nyumbani
Tanzania yale yote yaliyotokea kwenye uwanja huo wa QE11 Park siku hiyo
na wengi wakamsikia Filbert Bayi mwenyewe akielezea furaha yake kuhusu
ushindi ule. Ripoti hiyo ndiyo ilikuwa ripoti yangu ya mwisho kutoka
Christchurch. Nilihakikisha ilikuwa ripoti iliyokuwa na bashasha chungu
nzima, maana nilitaka kumaliza kwa kishindo na kwa kweli kwa kishindo
nilimaliza.
Baadaye usiku ule nilikwenda kwenye ukumbi mkubwa
jijini hapo kuungana na wanamichezo wengine katika tafrija maalumu
iliyokuwa imeandaliwa na Meya wa Christchurch ya kuwaaga wote
waliohudhuria michezo hiyo. Hapa napo Watanzania tulikuwa tunakwenda
kifua mbele.
Wakati tukiwa hapo, ghafla nilikumbuka kwamba bado
nilikuwa sijarejeshewa sanduku langu ambalo lilikuwa limepotea njiani
wakati nilipokuja. Nikakumbuka pia kuwa maofisa wa Shirika la Ndege la
Qantas walionisafirisha walikuwa wameahidi kunirejeshea sanduku hilo
kabla sijaondoka kurejea nyumbani. Muda wa kuondoka ulikuwa umekaribia
na bado kulikuwa hakuna dalili zozote za kupatikana kwake. Nikadhamiria
kuonana nao siku ya pili yake.
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI