Kwa ufupi
Mitindo ni pamoja na kujiamini, unapovaa nguo ya
kutokea hasa wakati wa usiku, unatakiwa kuonyesha jinsi gani vazi lako
lina thamani. Vilevile onyesha kiasi gani uko huru na vazi hilo. Kwa
mujibu wa wataalamu wa mambo ya mitindo, sifa ya vazi la usiku ni
kuzungumza.
Vazi lako linatakiwa kutoa taswira halisi
uliyonayo mvaaji. Lijieleze lenyewe kwamba; “Niko kwenye ‘good time’,
siogopi lolote, mimi ni mkali” Lionyeshe unavyojiamini mbele ya watu.
Nguo ya kutokea usiku ni vazi la kipekee na
maalumu. Watu wengi hujaribu kuonekana tofauti wanapokuwa katika mavazi
haya, kwa kufanya kila kitu wanachotumia kuwa maalumu, kuanzia vipodozi
hadi mapambo mengine.
Licha ya juhudi kadha za kutengeneza mwonekano
mzuri, lakini mara nyingi kufikia lengo limekuwa tatizo kubwa kwa
wavaaji walio wengi. Kutokana na ukweli huo, mbunifu Ally Remtulah
amekuja na dondoo kwa mavazi ya usiku;
Uzuri wa vazi
Jambo hili huanzia kwa mvaaji. Hakikisha
unakubaliana na vazi lako, kwani kwa kufanya hivyo, itasaidia
kukuonngezea kujiamini, hivyo kuonekana mrembo zaidi.
Kuwa huru katika kupiga hatua.
Hakisha viatu ulivyovaa vinakupa uhuru wa kutembea
kwa madaha kadri uwezavyo, bila kukuvurugia utaratibu. Mwondoko mzuri
mara nyingi una nafasi katika kukupendezesha na kulipa thamani vazi
lako.
Wanawake wengi wamekuwa wakiamini kuwa nguo ya
kubana ndiyo inayompendeza mtu, lakini ukweli ni kwamba nguo
inayokupendeza ni ile inayokuweka huru. Haijalishi imebana sana ama fupi
sana.
Usivae kitu cha ‘ajabu’ kama wewe si mtu wa ‘ajabu’.
Hakikisha unakuwa wewe halisi katika mavazi yako.
Mavazi ya Lady Gaga ni utambulisho wake, hivyo hayawezi kuendana na mtu
yeyote isipokuwa yeye mwenyewe. Hilo pia unapaswa kulifahamu.
Usichague vazi la bei rahisi.
Mwanamke, simamia kwenye ubora. Wakati mwingine kwa kuchagua
kitu cha bei rahisi unaweza kujikuta unaishia kupoteza thamani yako
halisi. Kwani hata wanaokutazama watakuona.
Usivae ‘Dar Combine’
Dar combine inamaanisha vazi linlovaliwa na wengi.
Hivyo wewe mwanamke jitahidi kutafuta vazi la kipekee, siyo vibaya
ukavaa hata la mtumba, lakini la mbunifu anayejulikana. Hii itasaidia
kukufanya uoenekane unaelewa maana halisi ya mitindo.
Kuwa makini na mtindo wa nguo yako.
Kwa kuwa kila mmoja ana umbo la aina yake ni vyema
unapochagua nguo kuangalia mtindo upi hasa unaendana na aina ya umbo
lako. Ikiwa umbo lako linaendana na suruali, vaa suruali, lakini kama
haliendani, usilazimishe.
Zingatia hali ya hewa
Katika uchaguzi wako ni muhimu kuzingatia hali ya
hewa kwa wakati husika. Kuvaa vazi lisiloendana na hali ya hewa ya
wakati husika, kunaweza kukuondolea hali yako ya kujiamini, hata pia
kukufanya usiwe huru. Kitendo hicho huchangia kuharibu siyo tu mwonekano
wako, bali hata wa vazi ulilovaa.
Imeandaliwa na Maimuna Kubegeya
Mitindo: Fashion Avenu
SOURCE: MWANANCHI