Kwa ufupi
- Hata hivyo anasema: “Moyo wangu ulichoka, nilipenda mazao ya mizizi, nilipenda kukutana na wakulima, sikupenda kazi ya maabara; …sikufanikiwa. Nilitaka kwenda katika siasa, nikaacha baada ya kuona aina ya ubaguzi hasa kwa watu wapya kwenye siasa, nikakata tamaa.”
Ukipita katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Unguja, Kibibi Mihogo ni miongoni mwa majina maarufu.
Umaarufu wa jina hilo umetokana na mchango wake
katika kufanikisha mambo mbalimbali kwenye jamii hasa kwa wanawake wa
Zanzibar, akielemea zaidi katika masuala ya kilimo, utafiti na harakati
za kupunguza umaskini.
Kibibi Mihogo ambaye jina lake halisi ni Kibibi
Mwinyi Hassan ni mzaliwa wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini, Unguja
katika Visiwa vya Zanzibar.
Ni mtoto wa kwanza kati ya wanne kwa baba mmoja na mama mmoja, akiwa na ndugu wengine wa baba mmoja mzee Mwinyi Hassan.
Mwanamke huyu ambaye pia ana watoto wanne akiwa
pia ni mjane baada ya mumewe kufariki dunia, Juni mwaka jana, alianza
safari yake ya elimu katika shule ya msingi iliyopo kati ya Kijiji cha
Bwejuu na Paje.
Baadaye alijiunga na Sekondari ya Machipi iliyopo
Ifakara, wilayani Kilombero, Morogoro, ambapo alisoma mchepuo wa kilimo
na kuhitimu mwaka 1979.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya,
wilayani Kilindi mkoani Tanga, alipokuwa kikazi na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba anayoifanyia kazi sasa, Kibibi aliye na Shahada ya Uzamili ya
Rasilimali Watu, anaeleza kuwa baada ya kumaliza kidato cha nne
alijiunga na Chuo cha Kilimo Ilonga, wilayani Kilosa, pia mkoani
Morogoro kabla ya kuajiriwa na Wizara ya Kilimo Zanzibar katika Idara ya
Elimu kwa Wakulima.
“Kati ya mwaka 1982 hadi 1985 nilifanya kazi ya
vipindi vya kilimo katika Televisheni ya Zanzibar (TVZ) na vipindi vya
redio, Sauti ya Tanzania Zanzibar. Pia nilikuwa nikitoa ushauri kwa
wakulima. Mwaka 1986 nikaenda kusomea Diploma ya Kilimo na Uzalishaji
Mazao, nikahitimu mwaka 1988,” anaeleza Kibibi.
Anasema kuwa baada ya hapo alipangiwa kazi katika
Kituo cha Utafitijeni wa Mazao ya Mizizi maarufu Kizimbani mjini
Zanzibar na kuwa Ofisa Utafiti wa zao la muhogo na nazi.
“Utafiti ulinifundisha mengi, nilisafiri nchi
nyingi, ulinifanya nijulikane Unguja yote. Nilikutana na wakulima, pia
kuwafundsha uandaaji na uzalishaji mazao bora ya mizizi hasa mihogo,
niliojifunza Nigeria. Niliweza kutambua aina ya mihogo na magonjwa ya
mimea kwa kutazama majani yake tu na hapo ndipo nikapewa jina la Kibibi
Mihogo. Najivunia utaalamu na kujulikana ,” anasimulia.
Kibibi anamtaja Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Salmin
Amour Juma kuwa alimwezesha kupata shahada baada ya kuwatangazia
Wazanzibari nafasi za udhamini wa masomo nchini Mauritius mwaka 1998,
ambapo miaka mitatu baadaye alihitimu na aliporejea Zanzibar alikuwa
mkuu wa Maabara ya Kuzalisha Mbegu katika Kituo cha Utafiti Kizimbani.
Hata hivyo anasema: “Moyo wangu ulichoka,
nilipenda mazao ya mizizi, nilipenda kukutana na wakulima, sikupenda
kazi ya maabara; …sikufanikiwa. Nilitaka kwenda katika siasa, nikaacha
baada ya kuona aina ya ubaguzi hasa kwa watu wapya kwenye siasa,
nikakata tamaa.”