Posted Jumapili,Septemba15 2013 saa 12:46 PM
Kwa ufupi
- Haya, baada ya kufanya mazoezi kidogo kwa kutwanga mtoto hadi mama watoto alitahayari niliamua kusoma barua nyingine.
Kama kawaida yake, Bunge letu tukutu limeleta
muvi tamu sana. Tena wameongeza utamu kwa kuleta muvi za vitendo badala
ya manenomaneno tu. Kwa kweli watu wengi siku hizi hatukosi vipindi vya
Mjengo kwa kuogopa kukosa uhondo. Nani anasikiliza maneno yao? Raha
vitendo bwana.
Ndiyo maana nilipata barua nyingi wiki hii.
Makengeza ng’wanamasumbwi
Hujambo bwana? Umefanya mazoezi leo?
Usicheke. Hata wazee msibaki nyuma. Mimi
nashangilia lakini sishangai kwamba hatimaye tunacheka na Cheka,
tumepata bondia aliyeshinda taji la kimataifa maana kwa masumbwi sisi
hatujambo. Tena napendekeza tuanzishe mitalaa rasmi kwenye shule zetu.
Hebu fikiria:
• Kwa masumbwi nyumbani hatujambo. Watu
wanatwangana kila siku. Mara mume kwa mke, mara wazazi kwa watoto, mara
nyumba kubwa kwa nyumba ndogo. Inavyoonekana wengi bila kutwanga,
wanaona wana kasoro. Kwa nini wasifundishwe kupigana kisayansi?
• Sheria ya viboko shuleni imefunikwa kabisa na
walimu viboko ambao licha ya kutofuata sheria kuhusu nani anaruhusiwa
kupiga viboko, kwa wakati gani na idadi gani, wanaona njia bora ni
makonde na ngumi.
• Hali yetu ya daladala inaeleweka. Bila ngumi
ngumu wanafunzi wengi wataingiaje kwenye daladala huku sisi wazee
tunaangalia tu. Na wakichelewa nyumbani sisi wazee tunafanya mazoezi ya
ngumi kwao eti wamekuwa wahuni siku hizi.
• Bila kusahau wanaopenda kufanya mazoezi ya
masumbwi kwa wezi wadogo kwa sababu wamekakamaa zaidi na kuacha wezi
wakubwa eti ni laini mno hawawezi kupigwa, waabudiwe tu.
Na sasa nifurahi sana kwamba hata waheshimiwa wetu
wa sponji wameachana na ulainilaini wao na kuamua kuonyesha mfano bora
kwamba bila kupigana hakuna maisha. Ila tu, nawalaumu wale wote ambao
walipenda kujificha nyuma ya vyombo vingine vipige kwa niaba yao badala
ya kuingia ulingoni wenyewe. Pigo ni uhai na bila kupiga, miili yetu
inadhoofika. Tena nashangaa hawa wengine wanaopenda kupiga nyumbani au
shuleni lakini wanalaani wanaotuwakilisha kwa kufanya vilevile
tunavyofanya nyumbani kwetu. Nchi ya masumbwi yahitaji mifano bora ili
tupevuke katika ngeu.
Kwa hiyo anza mazoezi sasa. Usibaki nyuma!
Haya, baada ya kufanya mazoezi kidogo kwa kutwanga mtoto hadi mama watoto alitahayari niliamua kusoma barua nyingine.
Mwishiwa Makengeza,
Najua wewe huna busara nyingi ndiyo maana
umeshindwa kuponyesha makengeza yako miaka yote hii lakini kwa kuwa
nimekata tamaa na wakalia sponji na kuwaona wenye hasara badala ya
busara, nimeamua angalau nichokoze nyinyi wenye upungufu kibao labda
mtanionyesha njia. Iwapo wenye macho mazuri wanatuongoza hadi shimoni,
si bora kuwafuata wenye makengeza.
Tuchukue mfano wa katiba. Kwanza sikubaliani
kabisa na watu ambao wanasema kwamba katiba inatakiwa kuwa ya wananchi,
si kitu cha wanasiasa. Maisha ni siasa, uamuzi wa kuwa na vyama vingi au
chama kimoja ni siasa, kuweka haki za binadamu ndani ya katiba ni
siasa, kuamua kutoa kipaumbele kwa hiki au kile ni siasa. Na kama kila
kitu ni siasa na wananchi wote hawana msimamo mmoja hiki au kile, ni
dhahiri kwamba wamba ngoma watawamba kweli. Shida yangu ni wawambe tu
siyo kuwanga.
Ndiyo. Mabosi watakuwa na msimamo mmoja na
wafanyakazi wao? Mkulima anayetaka kuuza mazao ili apate kupeleka mtoto
wake shuleni atakuwa na msimama mmoja na mfanyakazi anayetaka kununua
chakula kwa bei nafuu ili alishe watoto wake? Vijana watakuwa na msimamo
mmoja na wazee? Wabinafsi na walafi wanaotaka kuneemeka juu na noma za
watu wengine watakubaliana kweli na wanaotaka maendeleo ya wote?
Thubutu! Ndiyo maana katiba ni mawasiliano, ni kuvutana na kuelekezana
na kushawishiana hadi kufikia mwafaka ambao unazingatia maslahi ya watu
wote si wa kundi moja tu.
Na katika hayo inabidi kuwa wataalamu wa hesabu
pia. Hebu fikiria kuna uamuzi ngapi unayohitaji hesabu. Tunataka
kuhesabu tuwe na nchi ngapi, serikali ngapi, marais wangapi, waheshimiwa
wa sponji wangapi, walaji wa jasho letu wangapi, haki ngapi katika zile
zinazotambulika kimataifa, wateule wa mtu mmoja wangapi, hesabu kali
kwelikweli. Na bila kusahau wangapi wa kutuamulia tuwe na katiba ya aina
gani.
Lakini si hivyo tu. Ndani ya hisabati kuna hesabu
za uwiano pia. Haitoshi kujumlisha tu, ni lazima kutafuta uwiano
unaokubalika. Pia hesabu za kanuni ambazo nazo zinaendana na uwiano moja
kwa moja.
Ndipo hapo napata wasiwasi kama kweli waheshimiwa
wetu wa sponji wamesoma hesabu kweli. Sikatai kwamba hawakubaliani
kwenye kujumlisha maana wengine wanajumlisha kikompyuta na wengine
wanatumia hesabu za mwaka uleee. Lakini wenye uwiano na kanuni
nashangaa. Ni kama hawajawahi kusikia hesabu zingine kabisa. Wote
wanadai kwamba wanataka katiba ambayo inaleta mwafaka na maelewano, na
wote wanapaswa kujua kwamba mwafaka na maelewano hutokana na uwiano na
kanuni. Kwa mfano iwapo a = 8 na b = 3, huwezi kuandika kwamba a = b.
Unaweza kuwalazimisha watu waimbe a = b lakini iwapo, kwa mfano,
unajaribu kujenga kitu, au kufanya biashara kwa hii a = b, matokeo yake
ni janga moja kwa moja.
Ndiyo maana nakimbilia kwako Makengeza, wewe na
wenzio ambao hamtaki kulazimishwa a = b. Utajengaje mwafaka wakati robo
tatu wako kwenye kundi moja na wanajaribu kulazimisha asilimia tisini
wawe wa kundi moja hilohilo. Kwanza hawajui hesabu, na pili, katika
kulazimisha uwiano na kanuni, hawalitakii mema taifa letu hata kidogo.
Na tatu, wanaonyesha kiburi kile cha dhambi ya asili, eti wao wanajua
kila kitu, uamuzi wao wote ni sahihi, matakwa na mawazo ya makundi
mengine yote ni batili. Hawawezi hata kutambua kwamba ili kujenga
mwafaka wapaswa kufikiria mawazo ya watu wengine. Na mwisho wameonyesha
dhahiri kwamba wanajali maslahi yao tu ndiyo maana hesabu za uwiano na
kanuni wamezipiga marufuku katika mitaala ya hisabati kwa sababu inaleta
mawazo mabaya kwenye fikra za watu.
Kweli huwezi kuwa na nchi ya makundi mengi na
katiba ya kundi moja au nchi ya vyama vingi lakini katiba ya chama
kimoja au nchi ya madhehebu mengi lakini katiba ya dhehebu moja. Bora
watangaze kabisa kwamba hawajui kuhesabu zaidi ya moja. Nchi moja, chama
kimoja, amri moja, mteule mmoja, mwenye uamuzi moja na kadhalika.
Lakini wasitudanganye kwamba wanapenda hesabu kubwakubwa na hesabu za
kisasa huku hawajui kabisa.
Mwalimu wa Hisabati
Uzuri wa walimu wa hisabati ni kwamba ni watu wa
mantiki pia. Ndiyo maana huyu mwalimu amechambua kimantiki. Lakini ubaya
wa walimu wa hisabati na hata sisi wengine wengi ni kwamba tunaamini
watu wote wanafuata mantiki.
Hasa katika kutafuta katiba yenye tiba bila
kutibua Hivyo wanangoja mantiki itawale huku maslahi na mihemko
imeshafukuza mantiki zamani au kuifungia jela.
Lakini tusiposimama na kutetea mantiki, kila kikundi kisipokuwa tayari kuvuta kwake pia hati tunavutana kwa uwiano, ngoma itapasuka nakuambia.
SOURCE: MWANANCHI
Lakini tusiposimama na kutetea mantiki, kila kikundi kisipokuwa tayari kuvuta kwake pia hati tunavutana kwa uwiano, ngoma itapasuka nakuambia.
SOURCE: MWANANCHI