Kwa ufupi
Kauli ya Nape ndiyo iliyomfanya Buhiye jana
kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema haamini kama kauli ya
kupinga uamuzi huo imetolewa na kiongozi huyo wa kitaifa ambaye
anaifahamu vyema Katiba ya CCM inayowapa mamlaka hayo.
Bukoba. Sasa ni dhahiri kwamba kuna mvutano
baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera na taifa kuhusu
kufukuzwa uanachama kwa madiwani wake wanane katika Manispaa ya Bukoba.
Mvutano huo unadhihirishwa na kauli iliyotolewa
jana na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Costansia Buhiye ambaye ametetea
uamuzi wa kuwatimua madiwani hao, huku Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman
Kinana akisema wameitisha mafaili yenye nyaraka zinazoeleza jinsi uamuzi
huo ulivyofikiwa.
Kinana akizungumza na gazeti hili jana kwa simu
kutoka Arusha alisema: “Tayari katibu wetu wa mkoa ametuletea mafaili
yenye nyaraka zinazohusu suala hilo na suala hilo litapelekwa kwenye
kamati ya maadili na baadaye kuamuliwa na Kamati Kuu.”
Kinana alisema msingi wa suala hilo kuamuliwa na
vikao vya juu vya CCM unazingatia azimio lililowahi kupitishwa na vikao
vya chama hicho likielekeza kwamba uamuzi wa kuwafukuza wanachama ambao
waliochaguliwa na wananchi unapaswa kupata baraka za vikao vya juu.
Kauli ya Kinana inaunga mkono ile iliyotolewa juzi
na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye alisema madiwani
waliotimuliwa waendelee na kazi hadi vikao vya juu vitakapofanya uamuzi
wa mwisho na kwamba halmashauri ya chama hicho mkoani Kagera ilifanya
makosa kufikia uamuzi wa kuwafukuza.
Kauli ya Nape ndiyo iliyomfanya Buhiye jana
kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kusema haamini kama kauli ya
kupinga uamuzi huo imetolewa na kiongozi huyo wa kitaifa ambaye
anaifahamu vyema Katiba ya CCM inayowapa mamlaka hayo.
Buhiye alisema uamuzi wa kuwatimua madiwani hao
ulichukuliwa kwa wakati na muda mwafaka na kwamba lazima vikao vya chini
pia viheshimiwe kwani hakuna kikao chenye uhalali wa kufuta uamuzi wa
kikao kingine kilichofanyika kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
“Uamuzi wa kuwawajibisha madiwani ni sahihi na uamuzi wa vikao vya chini
lazima uheshimiwe. Hata Halmashauri Kuu (Nec) ikikutana itarejea katiba
ya chama chetu na kanuni zilezile tulizopitia,’’ alisema Buhiye.
Buhiye alisema amelazimika kuitisha mkutano huo
ili kupunguza shinikizo la wanachama aliodai wanataka kuandamana kutetea
uamuzi uliofanywa na uongozi wa CCM Mkoa.
“Nimewaita ili kutoa ufafanuzi sahihi nipunguze
shinikizo la wanachama wanaotaka kuandamana hadi hapa ofisini, wana
imani na Halmashauri Kuu ya Mkoa tuendelee kutulia,’’ alisema Buhiye.
Chadema yawaponda waliotimuliwa
Chadema Wilaya ya Bukoba Mjini kimewaponda
madiwani wa CCM waliotimuliwa kikisema wanastahili kutokana na kugomea
vikao kwa mwaka mzima, ikiwamo bajeti ya maendeleo ya wananchi
Mwenyekiti wa chama hicho, Victor Shelejei alisema zipo njia
nyingi za kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi lakini si kugoma
kujadili mambo yanayohusu maendeleo ya wananchi.
Mwenyekiti huyo alisema malumbano ya madiwani na
meya yanazidi kudidimiza maendeleo ya wananchi. Madiwani waliotimuliwa
ni Yusuph Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba na
Diwani wa Kashai, Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Alexander Ngalinda
(Buhembe), Samuel Ruhangisa (Kitendagulo), Robert Katunzi (Hamugembe),
Deus Mutakyahwa (Nyanga), Richard Gasper (Miembeni), Mulungi Kichwabuta
(Viti Maalumu) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Ofisi ya Waziri Mkuu yatajwa
Katika hatua nyingine, ukimya wa Ofisi ya Waziri
Mkuu kukalia taarifa ya tume ya kuchunguza tuhuma za ufisadi dhidi ya
Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Aman unadaiwa kuchochea mgogoro
huo.
Tume hiyo ilichunguza tuhuma zilizoibuliwa na
Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki dhidi ya Meya Aman
kwamba ameiingiza manispaa hiyo kwenye miradi ya ufisadi, madai ambayo
yalikuwa yakiungwa mkono na madiwani waliotimuliwa.
Serikali iliunda tume iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa
wa Mbeya, Abbas Kandoro kuchunguza tuhuma hizo na ilimaliza kazi yake
miezi mitatu iliyopita lakini hadi sasa majibu yake hayajawekwa wazi.
Alipoulizwa sababu za majibu ya tume hiyo kutowekwa hadharani hadi sasa,
Kandoro alijibu waulizwe viongozi waliomtuma.
Kwa upande wake, Buhiye alisema CCM mkoani Kagera
haifahamu lolote kuhusu taarifa ya Tume ya Kandoro na kwamba wameomba
makao makuu ya chama hicho iwasaidie kuipata kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu.
source : mwananchi
Sou
source : mwananchi
Sou