Kwa ufupi
Morogoro. Hali ya wasiwasi imetanda mjini Morogoro baada ya
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa
Ponda, kudaiwa kupigwa risasi begani wakati polisi wakiwa katika
harakati ya kumkamata.
Habari kutoka katika eneo hilo zinadai kuwa Ponda
alipigwa risasi saa 12:25 jioni, wakati akisindikizwa na wafuasi wake
kuelekea katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja, baada ya kumaliza
kutoa mhadhara katika kongamano lilifanyika mjini Morogoro jana.
Tukio hilo lilitokea katika Barabara ya Tumbaku,
baada ya kumalizika kwa mkutano wa kongamano lililoandaliwa na Jumuiya
ya Wahadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro.
Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa
Msema aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa Ponda alipigwa risasi
sehemu ya bega, na askari polisi na kwamba aliwahishwa kutibiwa katika
Hospitali ya Kiislamu iliyopo eneo Msamvu mjini Morogoro.
Hata hivyo, wakati Sheikh huyo akisema hivyo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alikanusha madai
ya kuwa polisi wamempiga risasi.
Alisema polisi walifika katika eneo hilo kwa ajili
ya kumkamata Ponda, baada ya kumaliza mhadhara wake na kwamba wakati
wakitaka kumkamata ndipo wafuasi wake wakawazuia polisi na kulazimika
kupiga mabomu ya machozi na risasi hewani kuwatawanya.
Katika tukio hilo inadaiwa kuwa Sheikh Ponda
aliyekuwa katika gari ndogo huku wafuasi wake wakimsindikiza kwa miguu,
walipofika eneo la gereji mabomu ya machozi yalipigwa na polisi
waliokuwa katika magari aina ya defender wakati wakijaribu kuwatawanya
wafuasi hao.
Baada ya tukio hilo baadhi ya wafuasi wake
walimchukua Sheikh Ponda kutoka katika gari lake na kumkimbizia katika
gereji moja, kisha wakatoka wakiwa wamempakia katika pikipiki na
kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Mlinzi mmoja wa lango namba moja alisema kuwa
ulifika msululu wa pikipiki zaidi ya 50, lakini pikipiki zote
zilizuiliwa isipokuwa iliyokuwa imembeba Sheikh Ponda na kwenda naye
mpaka mapokezi.
Aidha, alisema wakiwa katika eneo hilo magari
kadhaa ya polisi yaliingia katika lango la hospitali hiyo. Hivyo wafuasi
wa Sheikh Ponda wakalazimika kumbeba begani na kutoroka naye kupitia
lango namba mbili.
Taarifa zilizopatikana baadaye zinadaiwa kuwa Sheikh Ponda alikimbizwa katika Hospitali ya Kiislamu ya Msamvu.
Baadhi ya watu walidai kumwona Sheikh Ponda akiingizwa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro, lakini walishangaa alivyotoweka.
Ni Morogoro mjini wakati akiongoza maandamano kuelekea katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja.
Katika Hospitali ya Msamvu taa za hospitali
zilizimwa baada ya kudaiwa Ponda kuingizwa katika hospitali hiyo, huku
milango ya kuingilia nayo ikifungwa na watu wachache waliruhusiwa
kuingia ndani.
Baadaye walinzi wa hospitali hiyo pamoja na baadhi
ya watu wengine walioonekana kama wafuasi wa Ponda, waliwafukuza.
Waandishi wa habari waliokuwa wakitaka kupata taarifa za kiongozi huyo
wa kidini pia walifukuzwa.
Katika kongamano lililofanyika katika Viwanja vya
Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Sheikh Ponda alisema kuwa matatizo ya
kunyanyaswa na kuteswa kwa Waislam yamekuwa yakichangiwa na Serikali
iliyoko madarakani na kuwataka Waislamu kuhakikisha kuwa katika Uchaguzi
Mkuu ujao wa 2015 wanachagua Serikali mpya yenye kujali haki sawa.
Sheikh Ponda alitolea baadhi ya mifano ya Waislamu
kunyanyaswa kuwa ni pamoja na Serikali kuingia mkataba na Wakristo
ujulikanao kama ‘Memorandum of Understanding’ ambao unawawezesha
Wakristo kupatiwa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa huduma za kijamii.
Alisema kuwa wakazi wa Mtwara wameonyesha mfano
kwa Waislamu kwa kudai haki yao ya msingi ya gesi iliyogunduliwa huko,
kwa kukataa gesi kutoka mpaka wakazi wa eneo hilo wanufaike kwanza hali
ambayo alidai kuwa ilizua taflani baada ya jeshi kupelekwa huko.
source: Mwananchi
source: Mwananchi