Posted Jumapili,Agosti11 2013 saa 16:23 PM
Kwa ufupi
Kuongezeka kwa ukubwa wa jeraha la kumwagiwa
tindikali kati ya mmoja wa waathirika wawili raia wa Uingereza,
kumeelezwa kumetokana na kumwagiwa maji machafu wakati wa kuwasaidia
wasichana hao.
Uingereza, London
Gazeti la Uingereza la Daily Mail toleo la jana,
liliripoti kuwa watu walioonekana kukata tamaa wakati wa kutoa msaada
kwa wasichana hao, kwa nia njema walitumia maji machafu kumsafisha mmoja
wa majeruhi.
Taarifa zaidi kuhusiana na tukio la kihalifu pia
zilieleza kuwa wasichana, Katie Gee na Kirstie Trup, wote wakiwa na umri
wa miaka 18, waliwaona waliowamwagia tindikali ambapo kabla ya kutenda
uhalifu huo, walitazamana, wakatabasamu na kupeana ishara kwa kichwa.
Wasichana hao waliokuwa wakifanya kazi ya
kujitolea katika Shule ya St Monica mjini Unguja, Zanzibar,
wamehamishiwa kwenye Hospitali ya Chelsea and Westminster, London
wanakotibiwa majeraha ya tindikali.
Mtalii aliyeshuhudia
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Sam Jones,
ambaye ni mtalii kutoka Uingereza aliyekuwa Zanzibar kwa mapumziko akiwa
na mpenzi wake Nadine, aliliambia gazeti la The Sun la Uingereza namna
alivyomsaidia Katie Gee baada ya kumwagiwa tindikali.
Jones alisema akiwa na mpenzi wake kwenye mitaa ya
Mji Mkongwe, Unguja, walisikia sauti ya msichana anayeugulia maumivu
makali, ikitoka katika choo cha mkahawa uliokuwa jirani.
Alisema walipoingia ndani ya choo walimkuta
msichana raia wa Uingereza akiwa ameungua vibaya mwilini, huku wasamalia
wema wakijitahidi kumfuta kwa maji yaliyokuwemo ndani ya choo hicho.
Jones alisema dakika mbili baadaye aliingia
msichana mwingine ambaye naye alikuwa ameungua, ambapo waliwapa msaada
wa kuwasaifisha kwa maji.
“Tulihisi kuna kitu kinawasumbua na kinahitaji
kutolewa,” alisema Jones na kuongeza kuwa waliwapeleka wasichana hao
kwenye zahanati ya jirani, ambapo Nadine na wanafunzi wa uuguzi walianza
kuwamwagia maji yaliyowekwa chumvi.
Alisema kutokana na kuwepo daktari mmoja tu,
waliamua kuwapeleka hotelini wasichana hao na kuwatumbukiza ndani ya
bwawa la kuogolea, katika jitihada za kuwasaidia kuondokana na maumivu
waliyokuwa nayo.
“Maji ya bahari yalionekana kusaidia kwa sababu
msichana mmoja aliungua vibaya kwa sababu mwanzo tulitumia maji ya bomba
na mengine yalichukuliwa kutoka kwenye ndoo,” alisema.
Jones ambaye alisafiri na majeruhi hao kuja Dar es Salaam na
baadaye Uingereza aliongeza kusema: “Tulishtushwa sana na namna
walivyokuwa na maumivu makali.
“Kitu ambacho nataka kuweka sawa ni kwamba
hawakuwa wamevaa nguo mbaya. Mmoja alikuwa amevaa sweta, suruali ndefu
na raba na mwingine alivaa kama hivyo. Walikuwa Zanzibar kusaidia
wananchi wa kawaida na walimaliza kazi yao salama.”
Alisema tindikali hiyo ilikuwa kali sana kiasi ambacho hata yeye (Jones), alibabuka mkono wakati akitoa msaada kwa Gee.
Jones alisema akiwa na mpenziwe Nadine na wananchi
wengine wa Unguja wakati wakiwasaidia nguo zao zilianza kupukutika kama
zilizooza, zikitoa harufu kali yenye uvundo.
Mwalimu mkuu
Akizungumza na gazeti hili Mwalimu Mkuu wa shule
ya St Monica ambayo wasichana hao walikuwa wakifundisha, Denis Mayemba
alisema waalimu wote wamesikitishwa na tukio na kuitaka kukomesha
vitendo hivyo ambavyo vinaoneka kushamiri visiwani.
“Tulikaa nao kama Watanzania wezetu, lakini
tunashangaa kusikia wamemwagiwa tindikali, kwa kweli wametuumiza sana
mioyo yetu,” alisema Mayemba.
Mwalimu mwingine wa shule hiyo, Margareth Kaleza
alisema wasichana hao walimwagiwa tindikali wakati tayari walishamaliza
muda wao wa kufanya kazi katika shule hiyo, na kwamba walishafanyiwa
sherehe ya kuwaaga.
Alisema walitarajia kuondoka jana kurejea kwao nchini Uingereza.
“Tuliishi nao vizuri bila kukwaruzana lakini nasikitika nani kawaumbua wale watoto,” alisema Margareth.
Alisema wako watu wachache ambao hawapendi kusikia amani iliyopo hapa kwetu ndiyo ambao wanafanya vitendo hivi.
Chanzo: Mwananchi.co.tz
Chanzo: Mwananchi.co.tz