Monday 12 August 2013

Katiba ibainishe nguvu za viongozi katika dini nchini


Na Aidan Mhando, Mwananchi  (email the author)

Posted  Alhamisi,Agosti1  2013  saa 13:39 PM
Kwa ufupi
Pia, wamesema viongozi hao watambulike kama wageni waalikwa na kwamba ili kuliweka jambo hilo wazi ni vyema likaanishwa kwenye Katiba ili kuondoa utata kwa viongozi wa Serikali kuhusishwa na kuwa na itikadi za kidini.


Kigoma. Baraza la Katiba la Wilaya ya Kigoma limetaka Rasimu ya kwanza ya Mapendekezo ya Katiba itamke wazi kuwa viongozi wa Serikali watakapo kuwa kwenye sherehe za dini hawatatambulika kama ni waumini wa dini fulani.
Pia, wamesema viongozi hao watambulike kama wageni waalikwa na kwamba ili kuliweka jambo hilo wazi ni vyema likaanishwa kwenye Katiba ili kuondoa utata kwa viongozi wa Serikali kuhusishwa na kuwa na itikadi za kidini.
Wakijadili kwenye kikao cha baraza hilo jana walisema ili kuepusha masuala mbalimbali na migogoro ya kidini ni vyema Rasimu ikaeleza kila jambo linalohusu dini kwa wazi na kufafanua ikiwa pamoja na kutaja kuwa Serikali haina dini.
Reonald Edson ambae ni mjumbe wa baraza la hilo alisema, “Naomba ifahamike wazi kuwa kiongozi wa Serikali atakapo hudhuria sherehe yoyote ya dini awe kama mgeni mwalikwa na sio mwakilishi wa dini yake.”
Alisema ilikuliweka jambo hilo wazi na likafahamika kwa kila Mtanzania ni vyema Katiba Mpya ijayo ikaeleza kwa kina nakulitolewa ufafanuzi ili kuepusha masuala ya kidini na udini kuibuka.
“Nchi yetu masuala ya kidini yameanza kuingia, sasa ili kuepusha jambo hili lisisambae kwa urefu ni vyema kila kitu kinacho endana na imani za dini kikatolewa ufafanuzi kwenye Katiba ili kusaidia kuondoa sumu za udini kusambaa nchini,” alisema Edson.
Ubunge
Mjumbe mwingine wa baraza hilo Mbasa Alfonce alisema anapendekeza kuwa mtu yoyote akipata ubunge au udiwani achane na kazi anayoifanya ili aweze kuwahudumia wananchi wake vizuri.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 21 (1) inasema kuwa mtumishi wa umma aliye katika ajira ya kudumu hataruhusiwa kuingia katika ajira nyingine yenye malipo ya mshahara.
“Kifungu hiki napendekeza kiwepo kwenye Katiba Mpya na kwamba kitiliwe mkazo zaidi ili kuhakikisha watumishi wa umma ikwa pamoja na waliyo chaguliwa na wananchi wanafanya kazi za kuwahudumia watu waliyowachagua,” alisema Alfonce.

source: Mwananchi.co.tz