Posted Jumapili,Agosti11 2013 saa 12:29 PM
Kwa ufupi
Hoja yetu kuu hapa ni kwamba, wananchi wamejaa woga na hofu kwa kutokuwa na uhakika wa usalama wao. Jambo linalochochea hali hiyo ni Jeshi la Polisi kutoonekana kufadhaishwa wala kukerwa na hali hiyo.
Wiki inayomalizika leo, wananchi waliendelea
kushuhudia matukio makubwa ya mauaji na vitendo vingine vya kihalifu
vinavyoashiria kwamba Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za usalama
pengine hazina tena uwezo au utashi wa kulinda raia na mali zao. Hali ya
usalama imeendelea kuzorota kwa kasi ya ajabu, hivyo hakuna mwananchi
anayeweza kujidanganya hivi sasa kwamba maisha yake yako salama na
kwamba atapata mahali pa kukimbilia iwapo maisha yake yatakuwa hatarini.
Tunaelewa fika kwamba kauli hiyo hapo juu ni
nzito, lakini tumeitoa bila woga wala kutafuna maneno kwa kutilia
maanani ukubwa wa tatizo. Tatizo la mauaji ya watu wasiokuwa na hatia
katika nchi yetu hivi sasa ni kubwa. Silaha zimezagaa ovyo mitaani na
zinauzwa kama njugu, huku zikitumika kuwaua watu kwa lengo la kupora
mali zao, kuwatia vilema vya maisha au kulipiza visasi. Hali hiyo ni
mbali na mashambulizi wanayofanyiwa baadhi ya watu kwa lengo la
kuwadhuru, ikiwa ni pamoja na kuwamwagia tindikali, kuwateka nyara,
kuwanyofoa macho na kuwang’oa meno na kucha.
Hoja yetu kuu hapa ni kwamba, wananchi wamejaa
woga na hofu kwa kutokuwa na uhakika wa usalama wao. Jambo linalochochea
hali hiyo ni Jeshi la Polisi kutoonekana kufadhaishwa wala kukerwa na
hali hiyo.Baya zaidi ni pale Serikali inapobaki tu kuwa mtazamaji wa
hali hiyo ya kutisha pasipo kubuni mbinu za kuhakikisha Jeshi la Polisi
linawajibika vilivyo. Inakuwaje kila kukicha mauaji yanaendelea katika
sehemu mbalimbali nchini, huku Polisi nao wakithibitika kuhusika na vifo
vya raia wasio na hatia katika baadhi ya matukio?
Katikati ya wiki, wafanyabiashara wawili maarufu
katika Mikoa ya Arusha na Manyara waliuawa katika matukio tofauti kwa
kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Kama hiyo haitoshi, siku mbili
zilizopita mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliuawa jijini
kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akitoka benki, huku
wasichana wawili raia wa Uingereza wakimwagiwa tindikali mjini Zanzibar
na watu wasiojulikana. Kuhusu tukio la Zanzibar vyombo vya habari
duniani kote vimeandika na kutangaza sana tukio hilo, ambalo
linasemekana litaathiri sana utalii wa Zanzibar kwa muda mrefu.
Kama tulivyoeleza hapo juu, matukio hayo ni kama
tone moja tu la maji katika Bahari ya Hindi, kwani matukio ya aina hiyo
katika kipindi cha miezi sita iliyopita ni mengi mno kuyaorodhesha
katika safu hii. Wananchi hawajasahau matukio ya kutekwa na kuteswa kwa
Absalom Kibanda na Dk Ulimboka jijini Dar es Salaam, wala hawajasahau
kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padre Ambrose Mkenda, kuuawa kwa
kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mushi na kumwagiwa tindikali kwa Sheikh
Saroga wote wa visiwani Zanzibar.
Ajabu ni kwamba Serikali imetia pamba masikioni na
tunahisi inafanya hivyo makusudi. Ukimya wa Serikali unatokana na
kulikumbatia Jeshi la Polisi na kushindwa kuliwajibisha, kwani jeshi
hilo limethibitika kuibeba Serikali na chama tawala dhidi ya vyama vya
upinzani. Ni maoni ya wengi kwamba mpaka pale jeshi hilo litakapojivua
minyororo ya utumwa wa kisiasa, likavunja ndoa na wanasiasa na kuwa
jeshi lenye weledi, ndipo tutakapoona mwisho wa mauaji na uhalifu
mwingine ambao umepandikiza hofu na kuchafua taswira ya nchi yetu.
chanzo: Mwanachi.co.tz
chanzo: Mwanachi.co.tz