Kwa ufupi
Siku za karibuni umeibuka mvutano bungeni na
kuacha badhi ya wabunge wakiulalamikia uongozi kwa upendeleo, huko
uongozi nao ukidai baadhi ya wabunge watovu wa nidhamu.
Mbunge kijana anasema huwezi kumkalisha
chini kijana anayetetea wananchi wa jimbo lake, hapo panakuwa pagumu
kidogo. Bunge lazima liwe la moto, ndiyo maana unaona hakuna mbunge
anayesinzia
Kabla ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini
mwaka 1992, ilikuwa nadra kuwakuta wabunge vijana kwenye Bunge la
Jamhuri ya Muungano.
Hata baada ya mfumo huo kurejea, katika Bunge la
kwanza la vyama vingi la mwaka 1995 hata 2000, vijana hao hawakuwa
wengi, lakini Bunge la sasa ndilo linaloonekama kuwa na wabunge wengi
vijana na pengine hii yaweza kuwa sababu ya chombo hicho kuonekana
machachari kuliko mabunge yalitangulia.
Ni katika Bunge hili ambapo wabunge wengi wamekuwa
wakipewa adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao, kutolewa nje wakati
vikao na hata kuzua malumbano ya wazi baina ya wabunge wenyewe kwa
wenyewe au baina ya wabunge na kiti cha Spika.
Matokeo ya hali hii, ni wabunge wakongwe au
wazoefu kama wao wanavyotaka kufahamaka, kuwatupia lawama vijana, eti
wao ndiyo sababu ya Bunge kutotawalika, huku wakiweka kando tuhuma za
kiti cha Spika kutotenda haki katika uamuzi.
Kwa baadhi ya wabunge, kuwapo kwa vijana wengi
ndani ya chombo hicho, kumekuwa ni changamoto kubwa kwao na hata wengi
wao kuonekana kupwaya mbele ya umma unaofuatilia mijadala ya Bunge,
hivyo kukerwa na matukio yanayofanywa na wabunge hao vijana na kuyaona
kama utovu wa nidhamu.
Kwa upande wa pili, wabunge vijana mambo ni
tofauti, wao wanasema kuwapo kwao ndani ya Bunge kumeleta hamasa kwa
wananchi kujua na kuzidai haki zao na zaidi wamepata fursa ya kujua aina
ya wawakilishi waliowachagua.
Augustine Mrema, Mbunge wa Vunjo (TLP), anasema
lipo tatizo kubwa kwa Bunge la sasa likilinganishwa na Bunge la Tisa,
akidai kuwa wabunge wengi hivi sasa hawaheshimu wala kuzingatia kanuni
za Bunge.
“Ninachoona hakuna utii, umakini wala kufuata
kanuni. Kwa mtazamo wangu hili ni Bunge la ajabu sana kulinganisha na
mabunge yaliyopita…limekithiri utovu wa nidhamu, naweza kusema
limepoteza umakini,” anasema.
Mrema anasema kama ulivyo mhimili wa Mahakama na
Serikali, Bunge nalo linapaswa kuheshimiwa kabisa, lakini tatizo
lililopo kwa wabunge kudharau mhimili huo.
Anasema kama ambavyo mhimili wa Mahakama una
udhaifu na malalamiko mengi, hakuna mwanasheria yeyote awe wa serikali
au wa kujitegemea anayeweza kuvunja sheria kwa kumdharau jaji kwa namna
yoyote.
Bila kugusia hoja ya majaji kutokuwa wanachama
wala viongozi wa vyama vya siasa, Mrema anahoji, “Iweje Spika
adharauliwe na wabunge licha ya kuongoza mhimili huo wa dola? Kila mtu
anajua mahakamani kuna udhaifu mkubwa, lakini sijasikia wanasheria
wakimbwatukia jaji au hakimu kwa kuchelewesha kesi, mambo yanaenda kwa
nidhamu ya hali ya juu. Ukifungua simu tu jela miezi sita na hakuna
anayeweza kubishia uamuzi wa jaji…kwanini nidhamu inayoonyeshwa
mahakamani isionyeshwe katika bunge?
Anasema la wabunge wengi wa sasa ni mambumbumbu,
wasiozisoma wala kuzijua kanuni na tatizo lao ni kuwa hata zile hoja
nzuri wanazoziibua hazionekani kutokana na kuziwasilisha katika mtindo
wa vurugu.
“Hata kama una hoja nzuri kiasi gani na huna
adabu, ule umakini utakujaje? Ukishafanya vurugu mambo mazuri hayawezi
kuonekana…Kanuni zinasema Spika au Mwenyekiti akisimma, mbunge akae,
lakini bungeni ni tofauti. Mbunge akisimama nao wanasimama, huo ni
utaratibu gani? Kuwasha kipaza sauti bila kusubiri kibali cha Spika, huu
ni utovu wa nidhamu ambao unafuta mazuri yote wanayoyaibua,” anasema
Mrema.
Kwa upande wake Ismail Jussa, Mwakilishi wa Jimbo
la Mji Mkongwe (CUF), anasema wabunge wa zamani walikuwa na ujasiri, wa
kuhoji na kuibua mambo na watii Kanuni za Bunge kwa sababu walikuwa
wakizijua baada ya kuzisoma na hata kufundishwa, lakini hawa wa sasa
hawazisomi wala hawazielewi kanuni hizo.
Kwa mujibu wa Jussa, wabunge wengi wa sasa
wanatawaliwa na itikadi za vyama vyao, wakiwamo wale wa upinzani
wanaopinga lolote linaloibuliwa na upande wa serikali na upande wa pili
vivyo hivyo.
Anasema ndani ya Baraza la Wawakilishi hali ni
tofauti, kwani kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
(SUK), wawakilishi wote wasio mawaziri husimama kutetea wananchi kwa
kuipinga au kuiunga mkono Serikali.
“Zamani kabla ya kuwepo kwa SUK hata mpinzani
angekuwa na hoja nzuri vipi, angepingwa tu na wawakilishi wa CCM na hoja
hata ingekuwa dhaifu kiasi gani, mradi imetolewa na Serikali ingeungwa
mkono na wawakilishi wa CCM. Hata hivyo, sasa siyo hivyo, tatizo hili
lipo zaidi katika Bunge la Muungano,” anasema.
Anaongeza kuwa utamaduni wa kisiasa miaka ya
zamani ulijikita katika suala la kutii mamlaka. Zamani mtu anapoelezwa
kuwa amekosea ilibidi kukubali na kukaa chini. Ule utamaduni unaondoka,
hiki ni kizazi kipya sasa watu wanabishana na hata kukaidi maagizo ya
kiti.
Hata hivyo, Jussa anasema hali hiyo inatokana na
wanaokaa kwenye kiti ambao wanaonekana kuelemea upande mmoja tofauti na
zama za Spika kama Adam Sapi Mkwawa na Pius Msekwa, ambao waliheshimiwa
kutokana na kuongoza vyema, licha ya Msekwa kuongoza wakati wa vyama
vingi.
Mmoja wa wabunge vijana, Livingstone Lusinde
(Mtera-CCM) anasema kwa mtazamo wake Bunge la sasa ni zuri kuliko
mabunge yote, linafanya kazi kwa umakini mkubwa na ndiyo maana linaibua
mambo yaliyojificha.
Anasema suala la kutii kanuni linategemea na
wakati, kwani kuna kipindi inamuwia vigumu mbunge kutii amri ya kukaa
chini pale anapotetea wananchi wake, kukemea uovu au kutoa ufafanuzi wa
jambo.
“Huwezi kumkalisha chini mtu anayelalamikia kero
za wananchi wa jimbo lake, hapo panakuwa pagumu kidogo. Bunge lazima
liwe la moto, ndiyo maana unaona hakuna mbunge anayesinzia. Bunge lina
hoja za moto. La kwetu ni zuri kuliko mabunge yaliyopita.
Naye Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany
anasema Bunge la sasa lina umuhimu wake na uimara kutokana na kuwa na
mchanganyiko wa vyama vingi.
“Linao wasomi wa kiasi kikubwa kulinganisha na mabunge
yaliyopita…Wabunge wengi wa kambi ya upinzani wameongezeka hasa kutoka
upande wa bara na wameingiza chachu kutokana na kuibua hoja nyingi
zinazungumzia kero za bara,” anasema.
Anasema tofauti na kipindi cha nyumba ambapo idadi
kubwa ya hoja zilihusu mijadala kuhusu kero za Muungano, sasa nyingi
zinaelezea masilahi ya bara zaidi hali inayoongeza mvuto na umakini wa
Bunge la sasa.
“Bunge la sasa limekuwa la wananchi zaidi kutokana
na kuwa sauti za wananchi…sasa hivi mbunge anaweza akasimama akapigia
kelele hoja kuhusu wananchi na akapata majibu. Hili ndilo Bunge
lililoibua mambo mengi na kuwezesha kusogeza huduma kwa wananchi,”
anasema Barwany
chanzo: mwananchi