Kwa ufupi
Alisema Serikali imeshindwa kutekeleza ilani yake ikiwamo kuwapatia maisha bora wananchi.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ametupa kombora kwa Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), akisema imeshindwa kutekeleza ahadi zake na badala
yake inatumia vyombo vya dola kuwakandamiza na kuwaumiza wananchi.
Lipumba pia aliishutumu Serikali kwa kuwakumbatia
viongozi ambao wanatuhuma za ubadhilifu kwa kuwahamisha katika vituo
vyao vya kazi, hivyo kuendelea kuzorotesha uchumi wa nchi na kusababisha
hali ya ugumu wa maisha kwa wananchi.
Aliyasema hayo jana wakati akifugua mkutano wa
Baraza Kuu la chama hicho, Dar es Salaam, ambapo alisisitiza kuwa
ubadhilifu ambao unakumbatiwa na Serikali hiyo umedhihirishwa pia na
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mtaa (LAAC)ambayo imebaini
kuwapo mtandao unaohusisha viongozi wa Serikali wanaotafuna fedha za
umma.
“Hii ni Serikali ya kisanii sana maana kila inachokisema haitekelezi kwa mfano kule Mtwara wananchi wanaendelea kuteswa .
Alisema Serikali imeshindwa kutekeleza ilani yake ikiwamo kuwapatia maisha bora wananchi.
Profesa Lipumba pia alieleza kusikitishwa kwake na
nguvu kubwa iliyotumika katika kumkamata Kiongozi wa Jumuiya ya Taasisi
ya Kiislam Sheikh Issa Ponda, akidai kuwa licha ya kwamba naye kuna
wakati huwa haungi mkono kauli zake, lakini haoni kama ni sahihi
kumhukumu kwa kumshambulia kwa risasi.
Alisema hatua yake ya kuzungumzia mara kwa mara
suala la Sheikh Ponda haimaanishi kuwa anafanya hivyo kwa kuwa ni
Mwislamu mwenzake, bali anafanya hivyo kwa kutambua ni wajibu wake
kutetea haki kwa wananchi wote.
Alisema ni wajibu wake kukemea na kulaani vitendo
kama hivyo akisema vilianza kwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten,
Mwangosi, vikafuata kwa Ponda na kwamba kesho vinaweza kumkuta yeye.
Kuhusu mchakato wa maoni kwenye Katiba Mpya,
Profesa Lipumba, alikosoa akisema kuwa baadhi ya vipengele havijafafanua
bayana kuhusu muundo wa Serikali na namna inavyoweza kujiendesha.