Kwa ufupi
Mgogoro huo wa kisiasa ni wa muda mrefu. Kwa
upande mmoja unamhusisha Menya, Dk Anatory Amani na badhi ya madiwani na
upande wa pili yupo Mbunge, Balozi Khamis Kagasheni na kundi jingine la
madiwani. Wote wanatuhumiana kwa mambo mbalimbali, lakini nyuma ya
pazia inadaiwa ni mbio za uchaguzi mwaka 2015
Keshokutwa hatima ya madiwani wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotimuliwa itajulikana mjini Dodoma.
Mgogoro huu ulianza kama mchicha sasa umekua na
kugeuka mbuyu. Ulianza kama tishio la chama hicho mkoani Kagera pekee na
Baraza la Madiwani la manispaa ya Bukoba, leo umekomaa hadi unajadiliwa
na Kamati Kuu ya CCM inayokutana Ijumaa.
Hatua ya CCM mkoa kuwatimua madiwani hao ni
jaribio la kwanza kwa chama ngazi ya mkoa kufikia uamuzi mgumu tangu
ilipotangazwa sera yake ya kujivua gamba.
Mgogoro huo dhidi ya Meya Dk Anatory Amani si
habari mpya, umevuma kwa zaidi ya mwaka mmoja. Nyuma yake kuna kivuli
cha mbunge wa Bukoba, mjini Balozi Khamis Kagasheki anayeunga mkono
tuhuma za ufisadi dhidi ya meya.
Upepo wa kisiasa usingebadilika ghafla hivi, kama
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete asingefanya ziara mkoani hapa
hivi karibuni na kushauri tofauti zilizopo baina ya makundi hayo
zimalizwe.
Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara yake
alisema lazima soko jipya lijengwe, mpango unaopingwa kwa nguvu zote na
madiwani waliotimuliwa.
Kauli hiyo ilionekana kutoa ushindi kwa upande wa pili na hivyo madiwani hao wakajipanga kulipa kisasi.
Kwa vyovyote vile kundi hili haliwezi kukubali
mradi wa kujenga soko jipya kwani wengi wao wanamiliki idadi kubwa ya
vibanda sokoni ambavyo huvikodisha kwa wafanyabiashara wengine.
Kabla Rais Kikwete hajatua Dar es Salaam, madiwani
waliandika barua ya kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa kuitisha kikao cha
kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya. Kauli ya Kikwete ilionekana
kuwa tofauti na matarajio yao.
Madiwani walitaka kumwonyesha Mwenyekiti wao kuwa
upo wakati sikio linaweza kuzidi kichwa. Maelekezo yaliyotolewa na
Mwenyekiti wao jinsi ya kumaliza mgogoro huo yalipuuzwa. Katika hatua
hii pia walifanikiwa kumnasa Diwani wa Kata ya Bakoba, Felician Bigambo
(Cuf).
Kabla ya kuhamia kundi hili, Bigambo alikuwa
mstari wa mbele kutetea miradi waliyoibua. Alitoa ushahidi mbele ya Tume
ya Abbas Kandoro jinsi madiwani walivyoshiriki hatua zote za vikao vya
uamuzi. Ghafla alijiunga na kundi la madiwani wa CCM ili awasaidie
kulipa kisasi dhidi ya matamshi ya Rais Kikwete.
Mwanzoni mwa mgogoro huu,Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kagera ilithibitisha kuwahoji
baadhi ya madiwani waliotimuliwa kwa tuhuma ya kupokea rushwa. Tangu
wakati huo ukweli wa tuhuma hizo umebaki kuwa siri ya Takukuru
Vioja vya Madiwani
Madai ya madiwani hao yameambatana na vituko
kadhaa zikiwamo tuhuma za kunyang’anywa simu na kufungiwa eneo moja ili
wasipatikane wakati wa vikao vya Baraza. Ni mpango wa kumkomoa Meya wao,
ili kukwamisha vikao baada ya akidi kupungua.
Hii ni dhambi inayowatafuna, kwani madiwani wale
wale waliwekwa ‘mateka’ wilayani Chato ili kufanikisha mpango wa
kumng’oa meya wa zamani, Samwel Ruhangisa kwa hofu kuwa wangerubuniwa.
Diwani huyo wa zamani amejiunga na kundi la kumpinga meya wa sasa.
Kwa mwaka mzima madiwani wamegomea vikao hata
walipofika ilikuwa kwa ajili ya kushinikiza ajenda yao ya kumng’oa Meya.
Waligoma hata kujadili bajeti ya Manispaa ambayo ndiyo msingi wa
kufanikisha shughuli za maendeleo ya wananchi wanaowawakilisha.
Miezi michache iliyopita madiwani hao walikwenda
Dodoma kupeleka mashtaka yao kwa Waziri Mkuu dhidi ya Meya wao.
Waliondoka kwa mbwembwe, ingawa walirejea kwa mafungu baada ya lengo lao
kukwama.
Ni madiwani walewale walioibua madai kuwa hawakuwa
na imani na Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza tuhuma dhidi ya
meya, wakidai kiongozi wa Tume hiyo Abbas Kandoro alionekana
akizungumza na mtuhumiwa.
Wakurugenzi wawili wang’oka
Katika mgogoro huu hata watumishi wa Manispaa ya
Bukoba hawako salama. Wako makini kwa kauli na vitendo ili wasituhumiwe
kuunga mkono moja ya makundi yanayopingana.
Tayari wakurugenzi wawili wameng’olewa kwa sababu
za kisiasa zaidi kuliko utendaji wao wa kazi. Mkurugenzi aliyekuwepo
wakati mgogoro unaanza, Hamis Kaputa alihamishwa ghafla baada ya moja ya
pande zenye mgogoro kupoteza imani naye.
Mkurugenzi aliyechukua nafasi yake, Trazias
Kagenzi akitokea wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha naye alikaa majuma
mawili na baadaye kuondolewa ili kuridhisha moja ya upande wenye
mgogoro.
Kilichomponza Mkurugenzi huyo ni kuwa baada ya
uchunguzi wa madiwani ilionekana Mkurugenzi mpya alikuwa amesoma darasa
moja na Meya, Dk Amani na kujenga hisia kuwa utendaji wake ungependelea
upande mmoja.
Sasa kuna Mkurugenzi mpya Limbakisi Shimwela
ambaye hofu ya kuogopa makundi yenye mgogoro inasomeka vyema usoni
mwake. Hataki kuzungumza lolote kuhusu miradi ya Manispaa hadi hapo hali
ya hewa itakapotulia.
souce: Mwananchi
Dar es Salaam. Polisi Makao Makuu Kitengo cha Makosa ya Jinai
Rasimali Watu, juzi ilimhoji Amir Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za
Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha kwa kile walichodai kuwa mtu huyo ni
rafiki mkubwa wa Sheikh Kondo Bungo anayetafutwa polisi.
Taarifa kutoka kwenye vyanzo vya polisi Makao
Makuu zilieleza kuwa Bungo anatafutwa na polisi kwa kile walichodai
alitoa maneno ya uchochezi katika Mkutano wa Waislamu uliofanyika
Viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Advocate
Nyombi, kutoka Kitengo cha Upelelezi Makao Makuu alipotafutwa jana
kuzungumzia suala hilo, simu yake ilikuwa haipatikani.
Chanzo chetu kilidokezwa kuwa baada ya mkutano huo
ambao pia ulihudhuriwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert
Kiondo, Polisi walipanga kumkamata Bungo kwa wakati maalumu na siyo eneo
lile ili kuepusha vurugu ambazo zingeweza kutokea endapo angetiwa
nguvuni.
“Kundecha aliitwa jana (juzi) na kuhojiwa kwa saa
kadhaa na kumtaka amlete Bungo ambaye ni mtu wake wa karibu, “ alisema
mtoa habari huyo kuongeza kuwa: “Asipofanya hivyo kwa muda aliopangiwa
basi atakamatwa yeye hadi hapo atakapo patikana Bungo.”
Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu
inamshikilia Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa m Kitengo cha
Utafiti wa Mimea kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi fundi ujenzi,
Fadhili Mkachino.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa
10 alasiri maeneo ya SalaSala Benako wilayani Kinondoni.
Alisema Mkachino akiwa na mafundi wenzake
wakijenga nyumba moja ya Khadija, ndipo profesa huyo alitokea na
kuwataka kusisitisha mpango huo mara moja kwa kile alichodai ni eneo
lake.
“Kabla ya mafundi hao hawajafanya chochote ghafla
Profesa huyo alitoa bastola na kumpiga risasi mbili tumboni Mkachino
ambaye alikuwa kiongozi wa mafundi hao na kumsababishia maumivu makali,”
alisema Kamishna Kova.
Kova alisema kitendo cha kumpiga risasi mtu ni
kosa la jinai na kwamba ni jambo lisilokubalika katika jamii. Alitoa
wito kwa wenye silaha kuwa wavumilivu wakati wote.
souce: Mwananchi