Friday, 16 August 2013

Waafrika waongeza kasi kuwekeza barani Afrika

            

Mfanyabiashara maarufu barani Afrika 
Na Zacharia Osanga, Mwananchi  (email the author)

Posted  Alhamisi,Agosti15  2013  saa 12:9 PM
Kwa ufupi
  • Dangote ambaye ni bilionea amewekeza karibu Dola 500 milioni za Marekani sawa na Sh8 tilioni katika kiwanda hicho kitakachojengwa mkoani Mtwara.


Wakati vuguvugu la gesi iliyogunduliwa mkoani Mtwara lilipokuwa likiendelea, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha saruji kinachomilikiwa na Rais na Ofisa Mkuu Mtendaji wa Dangote Group, Alhaji Aliko Dangote.
Dangote ambaye ni bilionea amewekeza karibu Dola 500 milioni za Marekani sawa na Sh8 tilioni katika kiwanda hicho kitakachojengwa mkoani Mtwara.
Kiwanda cha Dangote kinatarajiwa kuzalisha tani milioni 3 za saruji kwa mwaka sawa na mifuko 150,000 kwa siku yenye uzito wa kilogramu 50 na kutengeneza ajira za kudumu 1,000 na zisizo rasmi 9,000.
Mbali na Tanzania, Dangote amewekeza pia katika nchi nyingine 14 barani Afrika katika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu katika ujenzi wa miundombinu, baadhi ya nchi hizo ni Zambia, Ethiopia, Senegal, Ghana n.k.
Kampuni yake ya Dangote Cement imewekeza Dola 5 bilioni za Marekani katika kujenga viwanda vya saruji barani Afrika.
Waafrika tunaweza
Mnigeria huyu ni miongoni mwa Waafrika wanaoondoa fikra ya neno ‘mwekezaji’ lazima atoke Amerika, China, Ulaya na nchi nyingine, lakini siyo Afrika.
Wakati Dangote akifanya hayo, hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Biashara (Unctad) lilitoa ripoti inayoonyesha kwamba uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) katika Bara la Afrika, umongezeka kwa asilimia 5.
Taasisi nyingine ya Kimataifa ya Ernest & Young inayojihusisha na ukaguzi wa mahesabu, kodi na ushauri kwa kampuni, yenye makao yake makuu jijini London Uingereza inasema wawekezaji wa Kiafrika wanaowekeza Afrika imeongezeka kutoka watu 27 mwaka 2003 hadi 145 mwaka 2011 sawa na asilimia 17 ya wawekezaji wote wa kigeni uliofanyika mwaka uliopita.
Utafiti huo unaonyesha kuwa miradi ya uwekezaji ya Waafrika wenyewe katika Bara la Afrika, imeongezeka kutoka miradi 339 mwaka 2003 hadi 857 mwaka 2013 sawa na asilimia 153.
Ernest & Young pia wanasema Benki za Nigeria na Kenya ni mifano halisi ya uwekezaji unaofanywa wawekezaji wa Afrika na imetoa mfano pia kwa Benki ya United Bank of Africa (UBA) ya Nigeria ambayo imewekeza katika nchi 18 barani Afrika ikiwamo Tanzania.
Utafiti wa Ernest & Young unasema ongezeko la Waafrika wanaowekeza barani humu ni dalili ya kujiamini kwamba Waafrika wanaweza shughuli za uwekezaji.

Ukigeukia Tanzania, Benki ya CRDB imewekeza jijini Bujumbura, Burundi ikiwa ni ishara kwamba taasisi za kifedha na kampuni nyingine zimeamka.
Katika mkutano wa uchumi wa Afrika uliofanyika Mei nchini Afrika Kusini, Waziri wa Uchumi na Fedha wa Nigeria, Ngozi Okonjo alihoji ni kwa nini mara zote Waafrika wanafikiria kuwekeza katika FDI badala ya Uwekezaji wa Waafrika kwa Afrika (AIA).
Rais Mstaafu wa Chama cha Wenye Viwanda Biashara na Kilimo, (TCCIA) Mhandisi Aloys Mwamanga alipokuwa akiizungumzia ripoti ya Uwekezaji iliyotolewa na Unctad alisema wawekezaji wanapaswa kuwa ni Watanzania wenyewe na siyo kutegemea wanaotoka nje.
Mwamanga alitolea mfano wa nchi ya China ambayo uchumi wake umekua kwa kasi na kutikisa mataifa makubwa kwa kuwa ilipitia njia hizo.
Katika mazungumzo yake, Mwamanga alilenga zaidi kuongeza thamani kwa bidhaa tunazozalisha.
Katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mamlaka zinazohusika na uwekezaji kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Uwekezaji ya Uganda (UIA) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Kenya (KenInvest) zinajinadi kuwa hali ya utulivu wa kisiasa ni moja ya vivutio vikubwa vya kuwekeza katika nchi zao.
Hata hivyo wakati nchi hizo za EAC zikijinadi hivyo na wawekezaji wa Kiafrika wakianza kuchanua vipo vikwazo wanavyokabiliana navyo ikiwamo hali ya kisiasa.
Nchini Swaziland wawekezaji kutoka Afrika Kusini wamekuwa wakisita kuwekeza nchini humo kwa sababu hali ya kisiasa si nzuri.
Katika utafiti uliofanywa na Taasisi ya DNA Economics ya Afrika Kusini na kuhusisha watu 400, asilimia 60 walisema hawataki kufanya biashara Swaziland kwa sababau hali ya kisiasa siyo nzuri ingawa asilimia 27 kati yao tayari wanafanya biashara nchini humo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 10 tu ya wafanyabiashara wa Afrika Kusini ndiyo wanapenda kufanya biashara katika nchi hiyo ndogo ambayo kijiografia inapakana na Afrika Kusini na Msumbiji.
Siasa ni kikwazo
Utafiti huo pia ulihusisha wafanyabishara 25 wa Swaziland ambao walikiri hali ya kisiasa katika nchi hiyo inawapa wakati mgumu wawekezaji wa kigeni kuvutiwa kuwekeza.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wawekezaji wengi wanawekeza Msumbiji ambako kuna mazingira mazuri kuliko Swaziland.
Hapa nchini licha ya kuwa na maeneo mengi ambayo TIC imeyaainisha kuwa ni vipaumbele katika uwekezaji kama nishati, kilimo, madini na viwanda, teknolojia nyingi bado wawekezaji wanatoka nje ya Bara la Afrika.
Licha wawekezaji wa Afrika wanaanza kuibuka linapokuja suala la ushindani na mataifa yaliyoendelea, matumizi ya teknolojia inabakia kuwa moja ya changamoto kubwa kwa wawekezaji wa Afrika. Dangote ameanza na wengine wafuate.

source: Mwananchi.