Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiwaonyesha waandishi wa
habari jana picha ya dawa za kulevya zilizokamatwa katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere , juzi usiku. Picha na Aika
Kimaro.
Kwa ufupi
- Amesema umefika wakati wa kuacha kuogopaogopa kwa masilahi ya taifa na kwamba hiyo ni vita ya kusafisha nchi.
- Akizungumzia
hali ya Uwanja wa JNIA baada ya kufanya ziara juzi, Dk Mwakyembe
alisema tatizo halipo kwenye vitendea kazi, bali wafanyakazi wasiokuwa
waaminifu.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kufanya ziara
ya ghafla Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema leo ataweka hadharani majina
ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini.
Dk Mwakyembe juzi alifanya ziara hiyo JNIA kukagua
utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku chache baada ya kutokea
kashfa ya kupitishwa kwa dawa za kulevya na baadhi ya Watanzania
wakiwamo wasanii kukamatwa sehemu mbalimbali duniani.
Aidha, hatua ya waziri huyo imekuja siku tatu
baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki
mbili kuanzia juzi, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika
mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja
vyote vya ndege nchini.
Akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa
ya Vijana iliyoandaliwa na Taasisi ya Jitambue Foundation,
yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana, Dk Mwakyembe alisema yuko
tayari kufa katika vita hivyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake
jana, Dk Mwakyembe alisema: “Kesho (leo) nitawataja wanaojihusisha na
dawa za kulevya. Kwa sasa nakamilisha ushahidi wa kutosha ikiwa ni
pamoja na picha za wahusika.”
Aliwaonyesha waandishi wa habari picha ya
mtuhumiwa mmoja ambaye alisema alikamatwa saa nane baada ya waziri huyo
kufanya ziara uwanjani hapo. “Ninataka watu wafahamu wanaoliingiza taifa
hili katika aibu hii, ambayo inasababisha Watanzania wasiaminike katika
viwanja vya ndege vya mataifa mengine.”
“Hatuwezi kuwa taifa la kuogopaogopa, hii ni vita
ya kusafisha nchi yetu, kwani ni nani mwenye mkataba na Mungu kuwa
ataishi milele?” alihoji Waziri huyo alipokuwa akijibu swali kuwa suala
la kuwataja watu wanaowafichua wasafirisha unga linaweza likaweka rehani
maisha yake.
“Kama hupendi joto usiingie jikoni”, alisema.
Akizungumzia watendaji wa JNIA kuhusiana na dawa
za kulevya, alisema: “Mfanyakazi yeyote atakayebainika kuhusika
kuwasaidia wasafirisha unga atafukuzwa kazi na ambaye atafanya juhudi ya
kuwakamata wasafirishaji hao atapewa zawadi.”
“Kuna watu wanadhani tunafanya mzaha katika jambo
hili. Jana baada ya mimi kuondoka usiku wa saa 2:30 huyu (kijana
aliyekamatwa) akaingia na mzigo,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa
alikamatwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi
aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.
Aliiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuwatunuku wafanyakazi waliofanikisha kukamatwa kwa kijana huyo.
Akizungumzia hali ya Uwanja wa JNIA baada ya
kufanya ziara juzi, Dk Mwakyembe alisema tatizo halipo kwenye vitendea
kazi, bali wafanyakazi wasiokuwa waaminifu.
“Tulikagua ili kujiridhisha kwa vifaa vilivyopo
na tumeridhika kuwa kiwanja ni kizuri, hata Shirika la Kimataifa
linalokagua viwanja vya ndege limeukubali kuwa uko vizuri katika vifaa
kwa hiyo tatizo lipo kwa sisi wenyewe wenye dhamana.
“Ukaguzi huu utaendelea katika viwanja vyote hapa
nchini mpaka bandarini na kila tutakayemkamata tutachapisha picha yake,”
alisema Dk Mwakyembe.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika
Kusini huku wengine wawili wakikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za
kulevya zenye thamani ya mabilioni ya fedha.
Akizungumzia kijana aliyekamatwa, mmoja wa askari
ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema: “Tulipewa taarifa za
kiitelijensia saa tisa alasiri na raia mwema kuwa kuna mtu anasafiri na
atafika uwanjani hapo kuanzia saa moja usiku na anasafiri kwenda Italia.
“Baada ya kupewa taarifa hizo tulijipanga na
ilipofika saa 1:49 usiku alifika kijana mmoja, kwa kuwa tulishaelezwa
wajihi wake, hatukupata shida, tulimchukua, tukamhoji na tulipompekua
tulimkuta na kete 84.”
Kamanda wa Vikosi vya Uwanja wa Ndege, Deusdedit
Kato akizungumzia tukio hilo alisema: “Alikuwa kwenye ukaguzi wa kawaida
akiwa kwenye mstari na ilipofika zamu yake aliamriwa akae pembeni
akafanyiwa upekuzi.
Alisema Mtanzania anatumia muda mwingi kukaa
Italia na kwamba polisi wanaendelea kumfanyia mahojiano ili kujua
alikozitoa na mhusika anayempelekea huko.
Alisema dawa hizo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa
Serikali kupimwa ili zifahamike ni za aina gani na anatarajiwa
kufikishwa Mahakama ya Kisutu kati ya leo na Jumatatu kutegemea
kukamilika kwa upepelezi.
Imeandikwa na Zacharia Osanga, Pamela Chilongola na Bakari Kiango.
Source: Mwananchi