Thursday 15 August 2013

Makunga, Kibanda wana kesi ya kujibu


Na James Magai  (email the author)

Posted  Jumatano,Agosti14  2013  saa 21:11 PM
Kwa ufupi
Mashahidi hao ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Magazeti, Raphael, Hokororo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza (ACP) kutoka Kitengo cha Sheria cha jeshi hilo, George Mwambashi na Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP), David Hizza.

Dar es Salaam. Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Theophil Makunga na wenzake wawili, wamepatikana na kesi ya kujibu katika kesi ya makala ya uchochezi inayowakabili.
Makunga na wenzake Absalom Kibanda na Samson Mwigamba wanakabiliwa na kesi ya uchochezi dhidi ya askari wa majeshi ya ulinzi kwa kuchapisha makala kwenye Gazeti la Tanzania Daima yenye maneno yaliyolenga kuwashawishi wasiwatii viongozi wao.
Makala hayo ya Novemba 30, 2012 yaliyokuwa na kichwa cha habari `Waraka maalumu kwa askari wote’ yaliandikwa na mshtakiwa wa kwanza, Mwigamba ambaye ni mwandishi wa makala katika safu yake ya `Kalamu ya Mwigamba’ katika gazeti hilo.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema jana aliwaamuru washtakiwa hao kujiandaa kupanda kizimbani kujitetea baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.
Wakili wa Serikali Beatha Kitau, alisema upande wa mashtaka haukuwa na shahidi mwingine zaidi hivyo kuiomba mahakama kufunga ushahidi wao. Kabla ya kufunga ushahidi wake, upande wa Jamhuri uliwaita mashahidi watatu kutoa ushahidi.
Mashahidi hao ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Magazeti, Raphael, Hokororo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza (ACP) kutoka Kitengo cha Sheria cha jeshi hilo, George Mwambashi na Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP), David Hizza.
Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake, mawakili wa utetezi wakiongozwa na Isaya Matambo waliiomba mahakama iwapatie mwenendo wa kesi hiyo kwa ajili ya kuandaa hoja kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.
Mbali na Matambo, mawakili wengine wa utetezi ni Nyaronyo Kicheere na John Mhozya ambao wote watatu wanawatetea Mwigamba na Kibanda na Imam Daffa kwa niaba ya Makunga.
Hata hivyo, Hakimu Lema aliwakatalia akisema kuwa hawezi kutoa nafasi ya kufanya majumuisho ya hoja kama washtakiwa wana kesi au la.
Hata hivyo, Hakimu Lema hakufafanua sababu ya kukataa ombi hilo, badala yake alitoa uamuzi papo hapo kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.
“Baada ya prosecution (upande wa mashtaka) kufunga ushahidi wake na kwa kuzingatia ushahidi ulioko mahakamani, Mahakama hii imeona kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu na wanatakiwa wajiandae kwa utetezi,” alisema.
Kutokana na uamuzi huo, Hakimu Lema aliamuru washtakiwa waanze kujitetea Septemba 3, mwaka huu.

Wakati uamuzi huo ukitolewa, mshtakiwa wa kwanza, Mwigamba hakuwepo mahakamani, badala yake aliwakilishwa na mdhamini wake Rose Moshi ambaye alisema mshtakiwa huyo hakuweza kufika mahakamani kwa kuwa ni mgonjwa na amelazwa Hospitali ya St. Thomas Arusha.
Makunga ambaye ni mshtakiwa wa tatu aliunganishwa katika kesi hiyo kutokana na gazeti hilo kuchapisha makala hayo katika mitambo ya uchapaji ya Kampuni ya MCL, wakati alipokuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda alidai kuwa Novemba 30, 2011, Makunga akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications ilichapisha waraka wenye kichwa cha habari “Waraka Maalum kwa askari wote”.
Kibanda ambaye ni mshtakiwa wa pili, anakabiliwa na mashtaka ya kuruhusu makala hayo kuchapishwa katika gazeti hilo, wakati huo akiwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima.
Upande wa mashtaka unadai kuwa makala hayo yaliyotoka katika gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 ni kinyume na kifungu cha 32 (1) (c) na 31 (1) (a) cha Sheria ya Magazeti, Sura ya 229, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Unadai kuwa makala hayo yalilenga kuwashawishi askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi, Magereza na Mgambo kutokutii amri za viongozi wa majeshi hayo na Serikali kwa jumla.

Source: Mwananchi news paper