Wednesday 25 September 2013

BARUA YA ANANILEA NKYA KWA RAIS KIKWETE: Rais Kikwete, jiandae kisaikolojia kupokea tuzo ya dunia

 
Na Ananilea Nkya

Posted  Jumatano,Septemba25  2013  saa 14:22 PM
Kwa ufupi
Nauona ujumbe huu kama ujumbe wa mtu aliaye nyikani. Hivyo kwa heshima na taadhima nakuomba  rais wangu uusome na kuutafakari kwa jinsi Mungu anavyokujalia.

Natumaini hujambo na Mungu wetu mwema anaendelea kukujalia afya njema, furaha na amani. Hongera sana kwa ujenzi wa taifa letu.
Ninakuandikia leo hii 23/09/2013 ujumbe huu wa wazi wenye maneno machache ambayo yalinijia akilini mwangu usiku wa manane na nikalazimika kuamka mapema na kuyaweka kwenye kumbukumbu. Napitisha ujumbe huu kwenye jukwaa la Mabadiliko lakini naridhia kwamba chombo chochote cha habari kinaweza kuuchapisha, nimeridhia.
Nauona ujumbe huu kama ujumbe wa mtu aliaye nyikani. Hivyo kwa heshima na taadhima nakuomba  rais wangu uusome na kuutafakari kwa jinsi Mungu anavyokujalia.
Rais wangu Kikwete, awali ya yote niweke bayana kwako kwamba mimi Ananilea Nkya, sina chama chochote cha siasa ninachofungamana nacho na wala sina mpango wowote wa kuwa mwanasiasa ama kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa.  Naridhika sana na taaluma yangu na hakika nijuavyo mimi, wanahabari anayetambua na kutekeleza majukumu yake kwa taifa lake, mchango wake unakuwa ni mkubwa pengine kuliko mchango wa mtu mwingine yeyote katika nchi yake.
Rais wangu, ujumbe wangu ni mfupi tu, kwamba tulipofika sasa kama nchi, hakuna Rais awe kupitia Chadema, CCM, NCCR-Mageuzi au chama kingine chochote atakayeweza kuivusha nchi hii 2015 kwa hali tuliyofikia sasa.
Mwanasiasa pekee mwenye UWEZO na MAMLAKA ya  kuivusha nchi hii tuweze kubaki  salama kama taifa moja la watu wanaopendana kwa dhati ni wewe peke yako.
Rais wangu Kikwete, kwa maono niliyoyapata usiku wa kuamkia leo,  nakuona ukiivusha nchi yetu hii kwa kujitoa mhanga ili ipatikane KATIBA MPYA YA UKWELI itakayondoa mamlaka  mikononi mwa mtu mmoja mmoja au chama kimoja kimoja na badala yake  kurejesha mamlaka mikononi mwa umma wa  Watanzania, ili tuepuke balaa la umwagaji damu linaloinyemelea nchi yetu  tuendako.
Rais wangu Kikwete, mimi ni ndugu yako wa ukweli. Ni Mtanzania ninayeipenda na kuithamini sana nchi yangu na wananchi wenzangu. Nakuomba ufungue macho yako ya rohoni uione TUZO YA DUNIA YA UTUMISHI ULIOTUKUKA inayokuja taratibu kwako kutokana na utumishi wako ukiwa Rais wetu.
Hata hivyo, Rais wangu Kikwete, ukiwasikiliza wasioithamini Tanzania na roho za Watanzania wenzao, watu wenye fikra kwamba chama cha siasa ni zaidi ya nchi na kufanya mambo yanayotoa dhana kwamba CCM ni zaidi ya Tanzania na kwamba bila CCM kutawala hakuna Tanzania,  nishani hiyo itakuponyoka na hakika mimi nitasikitika sana.  Rais wangu  Kikwete, nakutia shime, songa mbele kwa UJASIRI  upate kuifikia na kuipokea nishani yako, Tanzania  tujulikane duniani kote na heshima yetu ipande juu  kama nchi ya mfano inayoweza kufanya mabadiliko yake ya ukweli kwa amani, furaha na mshikamano.
Siku hiyo ya wewe  utakapokuwa unapokea nishani hiyo, mimi Ananilea Nkya, ni mmoja wa Watanzania watakaobubujikwa na machozi ya furaha kwa kuifikisha TANZANIA kwenye USHINDI.
Binafsi, Rais wangu Kikwete, ninakuamini na kukuthamini sana maana ninakujua tangu zama ukishiriki nasi harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi pale kwenye matamasha ya jinsia ambayo yalikuwa yanaandaliwa kwa pamoja kati ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika washirika wa FEMACT.  Nakujua uhalisia wako unapoamua kusimamia jambo, linatoka. Mungu akubariki sana na aendelee kukutunza na sote tuendelee kuombeana.
Mimi kwa sasa niko masomoni, ninaamini Mungu akitujalia tutaonana siku hiyo ya TUZO au kwenye harakati ukistaafu.

Wasalaam, Ananilea Nkya

SOURCE: MWANANCHI