Tuesday, 17 September 2013

Itikafu ya Ponda yatangazwa

17th September 2013
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu,Sheikh Ponda Issa Ponda
Wakati hatma ya dhamana kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, inatarajiwa kujulikana leo katika kesi ya uchochezi inayomkabili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms) umesambazwa ukiwahimiza Waislamu kukutana msikitini kwa itikafu.

Katika ujumbe huo ambao NIPASHE imeouona, Waislamu wametakiwa kukutana katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mjini hapa kwa ajili ya kusoma dua na kukesha kisha kuelekea mahakamani leo. Msikiti huo upo katika kata ya Kiwanja cha Ndege, mjini hapa.

Kwa mujibu wa ujumbe huo, itikafu hiyo ilipangwa kuanza jana saa 3:00 usiku hadi alfajiri ya leo huku mkusanyiko huo ukishirikisha masheikh kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Tanga, Arusha na Dar es Salaam.

Mmoja wa viongozi wa Kiislamu amesema kuwa itikafu hiyo ni ya kumtakia mema Sheikh Ponda ili ashinde kesi inayomkabili.

“Kesi ndiyo muhimu na ndiyo makusudio ya itikafu. Lengo ni kumueleza Mungu kutokana na dhuluma anayofanyiwa Sheikh Ponda, ana majeraha, lakini anafikishwa mahakamani kwa kuporwa Muhimbili, jambo hili siyo haki,” alisema kiongozi huyo.

Ujumbe huo unasema: “Tangazo Waislamu wote wa Morogoro, mnatangaziwa Itikafu kubwa ya kitaifa itafanyika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja uliopo Kiwanja cha Ndege Septemba 16, itikafu hiyo itaanza saa tatu usiku hadi alfajiri na baadaye kuelekea mahakamani kusikiliza kesi ya Sheikh Ponda Septemba 17, Itikafu hiyo itahudhuriwa na masheikh kutoka Mwanza, Kagera, Tanga, Arusha na Dar es Salaam. Asibaki mtu nyumbani wabillahi Tawfiq sambaza kwa waumini.”

Kwa mujibu wa mwanazuoni wa Kiislamu, Itikafu ni kikao cha kukaa msikitini kwa madhumuni ya kufanya ibada mbalimbali, kama kuomba dua, kusoma Kurani hata kulala ndani ya msikiti kwa nia ya kuelekeza maombi kwa Mungu ili atoe baraka zake kwa jambo linalokusudiwa.

Mwanazuoni huyo alifafanua kuwa mwenye kukaa itikafu ni suna kwake kusoma Kurani tukufu, kuomba dua, kuleta istighfaar (kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu) na kumswalia Mtume (S.AW).

Kesi hiyo ambayo imekuwa ikivuta umati mkubwa watu ambao wanadhaniwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda, inatajwa kwa mara ya tatu na leo itatolewa maamuzi kuhusu Sheikh Ponda kupatiwa dhamana ama kuendelea kukaa rumande wakati kesi hiyo ikiendelea.

Kesi hiyo ilipotajwa wiki iliyopita, Sheikh Ponda hakupelekwa mahakamani hapo kutoka mahabusu ya Segerea jijini Dar es Salaam kwa kilichoelezwa na mahakama hiyo kuwa hapakuwapo na ulazima wa kiongozi huyo wa dini kuwapo mahakamani kwa kuwa ilikuwa kwa ajili ya kutajwa tu.

Shekh Ponda aliposomewa mashtaka kwa mara ya kwanza Agosti 18, mwaka huu alisafirishwa kwa helikopta ya Jeshi la Polisi na ulinzi mkali wa jeshi hilo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Agosti 28, mwaka huu Serikali pia iliingia katika gharama kubwa kwa mara ya pili kwa kumsafirisha Sheikh Ponda kutoka Dar es Salaam kuja mjini Morogoro na kurudi kwa kutumia basi la Jeshi la Magereza.

Shekh Ponda ambaye anatetewa na mawakili watatu wakiongozwa Juma Nasoro, anadaiwa kutenda makosa hayo Agosti 10, mwaka huu saa 11:45 jioni katika maeneo ya Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro.

Inadaiwa alitoa maneno ya uchochezi kuwa  “Ndugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati wa ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata (Baraza la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana.”

 Wakili wa serikali, Bernard Kongola, alidai kuwa kwa kufanya hivyo alivunja masharti ya mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Hakimu Vicky Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ya Mei 9, mwaka huu iliyokuwa ikimtaka kuhubiri amani.

Katika shitaka la pili, Shekh Ponda anadaiwa kuwashawishi Waislamu kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia kuwa: “Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”

Kesi hiyo ya jinai namba 128 ya mwaka 2013 ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Morogoro, Richard Kabate.
CHANZO: NIPASHE