Sunday, 22 September 2013

Utumishi wa Mungu unahitaji uelewa wa ya dunia

 
Posted  Jumapili,Septemba22  2013  saa 13:2 PM
Kwa ufupi
Mtumishi huyu hajui kwamba katika maisha mtu anakuwa na malengo yake, ambayo angependa yatimie na anaweka mikakati ya kuhakikisha yanatimia. Kufanya kazi ya kuajiriwa siyo lengo ila ni mkakati wa kutimiza lengo.

Ni miaka mingi imepita, lakini bado nakumbuka jinsi wenzangu wengine niliokuwa nao sekondari walivyopotoshwa na watu wanaojiita watumishi wa Mungu. Mtumishi alikuja akawapa rafiki zangu wengine mawazo kwamba kumtumikia Mungu ni kusali na kuomba tu.
Inasikitisha kwani walikuwapo wenye akili zao, ambao hakika kila mtu aliwaweka kwenye orodha ya watu watakaosonga mbele kwenye masomo yao, lakini walikataa kabisa bidii ya kusoma na kuamua kumwomba Mungu tu.
Sijui pengine ulikuwa ni utoto au vipi. Hatukuwauliza mbona akina Nabii Danieli Mungu aliwapitisha kwenye elimu walizozipata au wainjilisti kama Luka walikuwa wasomi wakubwa.
Ninachokumbuka ni kwamba wengi wao walipata matokeo mabaya kwenye mitihani. Waliopata matokeo mazuri ni wale walioweza kugawa muda wao katika kuomba na kusoma.
Pamoja na kwamba unaweza kusema walijitakia wenyewe kwa wale waliofanya vibaya katika mitihani yao, bado mimi namlaumu mtumishi kwa kuwaongoza vibaya, hasa ikizingatiwa kwamba walikuwa bado kwenye umri mdogo uliohitaji mwongozo thabiti.
Kwa kuwa lengo kuu la Mtumishi wa Mungu ni kuzifikisha roho zetu salama kwa Muumba wetu, naamini hata mtumishi yule alikuwa na nia hiyo hiyo, ila ufahamu wake wa mambo mengine ya kidunia ndiyo ulikuwa mdogo. Ni bahati mbaya sana kwamba mpaka leo wapo watumishi wenye ufahamu mdogo katika maisha ya kawaida kiasi kwamba wanakuwa wapotoshaji na wanaleta majanga kwenye jamii.
Tunapambana na watumishi wanaoshangaa kitu ambacho hakika ni cha kawaida na kina maelezo, lakini kwa kuwa ufahamu wao ni mdogo kuhusu mambo yahusuyo miili yetu, chakula tukilacho, viumbe vilivyoumbwa na Mungu, matatizo ya kisaikolojia ya wanadamu, basi wanashindwa kutoa huduma ipasavyo.
Tuna mifano mingi ya majanga yanayoletwa na umbumbumbu wa watumishi kama hao. Nilimsikia mtumishi akihubiri kwenye msiba mmoja kwamba mtu kuandika barua ya kuacha kazi ni sawa na kutamka kwamba utakufa.
Kwake yeye anasema yeye hawezi kusema atakufa kwani hilo ni kumwandikia Mungu barua ya kuchukua uhai wako wakati wapo wale ambao watakutwa hai siku ya mwisho na huenda na yeye akawa mmoja wao. Hilo la imani ya kufa au kutokufa namwachia mwenyewe, lakini hili la kuandika barua ya kuacha kazi sitamwachia mtumishi huyo.
Mtumishi huyu hajui kwamba katika maisha mtu anakuwa na malengo yake, ambayo angependa yatimie na anaweka mikakati ya kuhakikisha yanatimia. Kufanya kazi ya kuajiriwa siyo lengo ila ni mkakati wa kutimiza lengo.
Kama mtu anaona ana mkakati mwingine ambao ni halali mbele ya Mungu na wanadamu ambao ana uhakika utatimiza lengo lake kwa ufanisi zaidi kwa nini asiache kazi na kuuchukua huo mkakati mwingine kama wa kwenda kwenye kazi nyingine ya ajira au kujiajiri?
Hakika mtumishi huyu nilimwona kuwa ni kipofu kwa masuala ya kimaisha ambayo naye ni sehemu. Nahofia sana ustawi wa vijana waumini wa kanisa kama hilo. Hapa karibuni nimeona kwenye vyombo vya habari kijana wa Kitanzania akipewa tuzo na taasisi moja nchini kwa ubunifu wake na namna ambavyo ameutumia ubunifu huo kumfanya milionea.

Sasa kwa matamshi ya mtumishi huyo akitokea kijana wa namna hiyo kwenye kanisa lake, lakini yupo kwenye ajira hatathubutu kuchukua hatua ya kuacha kazi na kutumia vipaji vyake hivyo? Mtumishi anapaswa kujua zaidi kuhusu fursa zilizopo sasa kwa vijana. Cha ajabu naye pia ni kijana, lakini hana habari na fursa za vijana leo.
Wakati mwingine kutofahamu huko kwa watumishi kunazalisha mawazo potofu ya kurogwa au kutupiwa mapepo kwenye vichwa vya watu wakati tatizo linaelezeka na lina sababu ya kutokea.
Kuna mkasa ambao mtoto wa kike aliyekuwa akijisikia kizunguzungu, mwili wake ukapauka, akawa anapata homa za mara kwa mara. Watumishi wakaingia kazini wakidai Roho wa Bwana amewaonyesha kwamba kuna mapepo yananyonya damu ya binti huyo. Hivyo ikawa ‘Kwa jina la Yesu toka, toka’ lakini mapepo yasitoke” mpaka hapo wenye ufahamu walipoamua kumpeleka binti huyo kwa daktari akampime ili isije ikawa ni tatizo linaloelezeka.
Binti alipopimwa ikajulikana kuwa siyo pepo bali ni mjamzito. Watumishi wakayeyuka! Hii ni aibu kwa mtumishi. Kwa nini kwa hali kama hiyo mtumishi akimbilie kwenye mapepo?
Kwa nini Watumishi wengi wa sasa wanaamini kila kitu ni kurogwa? Kwa nini hawataki hata kuamini kwamba wakati mwingine Mungu huruhusu mambo kama ilivyokuwa kwa Ayubu? Hivi ni mtumishi gani angemwombea Ayubu wa kwenye Biblia akapona wakati ule? Inawezekana kuna utapeli pia, lakini katika hilo namwachia yeye Yule, wanaodhihaki aseme nao mwenyewe, mimi nipo na hao mbumbumbu tu.
Tunapata watumishi vipofu kwa sababu wengine wanafikiria utumishi wa Mungu unahitaji watu watupu. Hivi kweli mtu hata kusoma na kuandika ni shida kwake atayapataje yale yaliyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu? Mtu atakuambia Roho Mtakatifu atamfundisha. Kama huo ndiyo mpango wa Mungu mbona Roho Mtakatifu huyo huyo alipita kwenye vinywa vya manabii na kusema; “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako”.
Jamani watumishi wa Mungu kuweni na kiu ya kujua yale ya Mungu na ya dunia yake ili muweze kutoa huduma stahiki. Mtoto mwenye tumbo kubwa la utapiamlo kwa kukosa lishe bora hana haja ya kuondolewa mapepo, badala yake ni kumwambia mama yake aache kuja kanisani kwako akiwa amevaa vitenge vya gharama ili aweze kupata fedha ya kumnunulia mtoto wake chakula chenye virutubisho vinavyotakiwa.
Haya yanawezekana kama tu naye mtumishi atakuwa ameelimika. Naamini kila mtumishi wa Mungu akiwa ameelimika tutapunguza majanga mengi ya kijamii kwani watu wanawaamini wao zaidi kuliko hata viongozi wa kisiasa.
Asante na Jumapili Njema.

SOURCE: MWANANCHI