Thursday 19 September 2013

Balozi Msuya : Vijana acheni kukimbilia Sauzi si peponi

Balozi Radhia Msuya 

Na Phinias Bashaya, Mwananchi

Posted  Jumatano,Septemba18  2013  saa 10:5 AM
Kwa ufupi
Baadhi ya vijana hao kupata matatizo ndipo kukumbuka  hukimbilia katika ofisi  yetu kwa ajili ya kupatiwa msaada

Pretoria. Kwa siku za karibuni limetokea wimbi kubwa la vijana  wa Kitanzania kukimbilia nchi mbalimbali duniani ikiwamo Afrika Kusini kwa madai ya kusaka maisha bora.
Baadhi ya vijana hao wamekuwa wakikamatwa na hata kurudishwa nchini baada ya kukosa uhalali kisheria wa kuendelea kuishi katika nchi hizo.
Wengine kati yao wamejikuta matatani kwa kuhusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na maovu mengine baada ya  kuingia katika nchi hizo kwa njia halali na zisizo halali.
Kwa upande wa Afrika Kusini, baadhi ya vijana hao wemeamua kuhamishia shughuli zao za kibiashara nchini humo.
Balozi wa Tanzania nchini humo, Radhia Msuya  anasema vijana wengi wanadanganyika kwa kufikiri kuwa maisha katika nchi hiyo ni rahisi na kuwa baada ya kufika huko mambo yatakuwa rahisi na kinyume chake mambo huwawia magumu na baadhi yao kuhitaji msaada wa kurudishwa nyumbani.
Vijana 200 kwa mwezi
Balozi Msuya anasema kila mwezi wastani wa vijana  200 hurudishwa nyumbani Tanzania kutoka nchini humo kutokana na sababu mbalimbali wakiwamo wale walioingia katika nchi hiyo bila vibali.
 ‘’Huku siyo peponi, maisha bora yanafanyiwa kazi kama ilivyo huko nyumbani. Kila mwezi tunarudisha nyumbani vijana  200 wanaokamatwa mitaani hapa wakiuza  bidhaa ndogo ndogo huku wengi wao wakiwa hawana vibali,’’ anasema Balozi Msuya.
 Anasema shughuli ndogo ndogo za biashara wanazofanya vijana hao kutoka Tanzania haziwawezeshi kumudu gharama kubwa za maisha nchini humo na baadhi yao hudaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, balozi  huyo  anawataka vijana wasiamini kuwa majibu yote ya changamoto zote zinazowakabili yanapatikana serikalini.
Anasema  baadhi ya majibu ya changamoto hizo yako mikononi mwao na utatuzi wake siyo lazima kukimbilia nchini humo.
 Anasema ni kweli  Afrika Kusini imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo maendeleo  ya kiuchumi, ingawa  pia yapo matatizo mengi  ambayo vijana hukumbana nayo baada ya kufikiri kwamba kukimbilia nchini humo litakuwa ni suluhisho la matatizo yote waliyoacha nyumbani.

“Ni kwamba  changamoto kubwa iliyopo ni vijana wetu kuacha kukimbilia nchini humu kwa dhana kwamba ‘wataukata’ tena bila ofisi za ubalozi wetu kuwa na taarifa za ujio wao. Baadhi ya vijana hao kupata matatizo ndipo hukumbuka  hukimbilia katika ofisi  yetu kwa ajili ya kupatiwa msaada,” anaeleza Balozi Msuya.
 Kifo cha Mangwea
Mathalan, Balozi Radhia Msuya  anasema ofisi za ubalozi wake hazikuwa na taarifa za ziara au safari ya msanii maarufu wa Tanzania, Albert  Mangwea kwenda nchini humo miezi michache iliyopita na hata alipofariki ghafla wao walipata wakati mgumu sana katika kufuatilia na kupata taarifa zake.
 Anasema baada ya taarifa za kifo cha msanii huyo kusambaa kwenye mitandao watu wengi  kutoka Tanzania  walipiga simu katika ofisi za ubalozi mjini Pretoria ili wapewe ukweli wa tukio hilo,ilihali ofisi za ubalozi hazikuwa na taarifa za msanii huyo kuwamo nchini humo.
Balozi huyo anabainisha kuwa huo ni mfano mmoja wa Watanzania wanaoingia nchini humo bila taarifa.
Anaeleza kuwa hivi sasa ni vigumu kufahamu Watanzania wanaoingia na kutoka nchini humo baada ya kufutwa kwa viza kati ya nchi hizo na hivyo kukata mkondo wa mawasiliano ambao ungewalazimisha kufika katika ofisi za ubalozi.
‘’Kifo cha Ngwea (Albert) kwa upande wetu kimetupa uzoefu, tunakosa  taarifa kamili za Watanzania wote wanaofika na kuondoka hapa nchini baada ya kufutwa kwa viza. Hata hivyo, hilo haliondoi wajibu wetu kama ofisi za ubalozi,’’ anabainisha Balozi Msuya.
 Anatahadharisha kuwa ni muhimu raia yeyete anayefika nchini humo kutoa taarifa kwenye ofisi za ubalozi huo ili kujenga uwezekano wa kupata msaada haraka endapo atapata matatizo tofauti na sasa ambapo wengi wao hawaoni ulazima wa kufanya hivyo.
Mtazamo wa Bushoke
Naye Maxmilian Bushoke, msanii Mtanzania anayefanya shughuli za muziki jijini Johannesburg anasema vijana wengi wanakimbilia katika nchi hiyo kubwa kiuchumi barani Afrika wakidhani kuwa nyumbani  hakuna mazingira rafiki ya kazi wanazofanya.
Anasema wapo vijana wengi kutoka nyumbani katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Johannesburg wanaofanya shughuli ndogo ndogo za biashara na kukiri wengi wao kuhusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Utalii Afrika Kusini

 Akizungumzia nafasi ya vivutio vya utalii nchini Afrika Kusini, Balozi Radhia Msuya anasema kuwa miongoni mwa kazi za ubalozi huo ni kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania na fursa za uwekezaji zilizopo ili kuongeza idadi ya watalii.
 Anasema kupitia ofisi za  ubalozi huo wamefanikiwa kushawishi watalii wengi nchini humo kutembelea Tanzania  hasa maeneo mbalimbali ya vivutio kama  Hifadhi za Taifa na kuwa matarajio ni kufanya vizuri zaidi kuwashawishi watalii wengi zaidi kutoka Afrika Kusini kutembelea nchi yetu.
 Hata hivyo, Balozi  Msuya anasema kuwa Tanzania haijapiga hatua kubwa katika masuala ya kuhifadhi mambo ya kale ikilinganishwa na nchi hiyo ya kusini mwa Afrika ambayo inapata fedha nyingi za utalii ikiwa ni matokeo ya kuhifadhi vyema maeneo muhimu ya  kihistoria. Anasema kwamba yapo mambo ambayo Watanzania wanafikiri ni madogo ingawa yana umuhimu mkubwa katika historia ya nchi.
Anasema kuwa yanayofikiriwa kuwa madogo ni vivutio vikubwa ambavyo huingiza fedha nyingi katika nchi zinazotunza vizuri historia. ‘’Wapo ambao hawana hata kumbukumbu ya cheti cha darasa la saba,hapo ndipo uhifadhi unapoanzia,kuna  vijana wengi ambao hawajui mambo muhimu  yanayohusu historia ya nchi yao,’’ anabainisha Balozi Msuya.
 Anatoa mfano wa eneo la Mnara wa Saa jijini Dar es Salaam analosema kuwa ni eneo muhimu katika historia ya nchi kwani hapo ndipo lilitolewa tamko rasmi  la kutangaza jiji hilo kuwa makao makuu ya nchi, lakini anahoji ni wangapi wanaojua jambo hilo. Hata hivyo, balozi huyo anasema eneo hilo limesahauliwa na hazionekani  dalili za kulihifadhi na kutangaza ‘mnara wa saa’ kama eneo muhimu la historia ya nchi.
Anasema eneo hilo limeendelea kuachwa kama lilivyo huku likisahauliwa na historia ya nchi, jambo ambalo ni hatari.
“Mambo mengi  yamesahaulika. Kwa mfano, njia alipopita Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa mguu wakati wa matembezi ya kuunga mkono Azimio la Arusha akitokea kijijini Butiama hadi Mwanza hazijulikani. Hakuna utambulisho wa  tukio hilo la kihistoria katika maeneo  aliyopita,” anaeleza na kutoa changamoto kwa mamlaka za umma nchini kushughulikia jambo hilo kama kivutio cha utalii.

SOURCE: MWANANCHI