
Mbunge wa Mkoani, Zanzibar (CUF) akiomba mwongozo wa Spika kutaka Bunge
liondoe Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
uliosababisha vurugu bungeni Juzi. Picha na Fidelis Felix
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Posted Septemba7 2013 saa 11:43 AM
Posted Septemba7 2013 saa 11:43 AM
Kwa ufupi
Hata hivyo, muswada huo ulipitishwa na wabunge wa
CCM na mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP) huku wabunge wa vyama
vingine vya upinzani wakiususia.
Dodoma. Dakika 90 zilitosha kwa Bunge jana
kupitisha muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya
Katiba na sasa Rais Jakaya Kikwete ndiye anayesubiriwa kutia saini ili
uwe sheria.
Hata hivyo, muswada huo ulipitishwa na wabunge wa
CCM na mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP) huku wabunge wa vyama
vingine vya upinzani wakiususia.
Vyama vilivyosusia majadiliano na upitishaji wa
muswada huo ni Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kutokana na kile walichosema
kuwa ni kukiukwa kwa kanuni na utaratibu mzima wa mchakato wake.
Wabunge walikaa kama Kamati ya Bunge zima kuanzia saa 6:30 mchana na
ilipofika saa 8:00 mchana, muswada huo ulikamilika kwa hatua zote.
Wakati wabunge wa upinzani wakiwa wametoka nje,
Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda na Clara Mwaituka
(CUF) walikuwepo bungeni hadi Bunge lilipofikia kuwa kamati ndipo
walitoka ndani ya ukumbi.
Hata hivyo, Serikali ilikubali mapendekezo ya
wabunge kikiwemo kifungu kilichohusu taasisi kupeleka majina kwa Rais
ili ateue mjumbe mmoja kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba.
Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mathias
Chikawe alisema kutokana na Serikali kuridhia mapendekezo hayo ya
wabunge, sasa taasisi hizo zitapeleka majina tisa ili Rais ateue jina
moja.
Hata hivyo pamoja na kupeleka majina hayo tisa,
sheria haitambana Rais kwamba ni lazima ateue mmojawapo kutoka katika
orodha hiyo na idadi ya wajumbe kutoka taasisi hizo haitazidi 166.
Pia Serikali iliridhia pendekezo la wabunge la
kuondoa takwa la lazima la mwombaji wa nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la
Katiba kwamba awe na ama shahada ya sheria, uchumi ama sayansi ya siasa.
Chini ya mabadiliko hayo sasa, mwombaji wa nafasi hiyo sasa atatakiwa
kuwa na shahada kutoka katika chuo kikuu chochote kinachotambuliwa na
Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).
Pia Serikali imeridhia kukifanyia marekebisho
kifungu kinachohusu ukomo wa Bunge la Katiba kutoka siku 90 zilizokuwa
zimependekezwa awali na sasa suala hilo litakuwa mikononi mwa Rais.
Wakati wa mchakato huo, suala la wabunge wa
upinzani kutoka nje na kususia vikao vya Bunge liliendelea kuchomoza,
huku Serikali ikisisitiza kwamba Zanzibar ilishiriki kikamilifu katika
kutoa maoni ya mabadiliko hayo
source: Mwnanachi