Thursday 12 September 2013

Hatusomi, hatujifunzi? Huyu katapeliwa 100,000,000/- na “mpenzi” wa mtandaoni


11/09/2013

 
Si jambo geni katika karne hii ya sayansi na teknolojia kusikia utapeli unaofanywa kwa njia ya internet.

Ila ni jambo la kuhuzunisha kuwa hata mwaka huu wa 2013 bado watu wanaotapeliwa kirahisi sana kwa mbinu za muda mrefu ambazo endapo tutajenga tabia ya kusoma, kujifunza na kuzingatia, hatutatapeliwa kirahisi.

Mbinu zinazohusisha kudanganywa kuhusu urafiki na hata ahadi za ndoa kwa mtu mliyefahamiana kupitia mitandao ya kutafuta marafiki ambao watakuwa wapenzi 'dating sites' kwa lengo la kugeuka wachumba kadiri watakavyoivana na hatimaye kufunga ndoa ni za muda mrefu sasa.

Leo nikitizama kipindi cha Dk Phil nimeshangazwa na ushuhuda wa wanawake watatu waliotapeliwa kiasi kikubwa cha fedha na bado walikuwa na imani kuwa iko siku wataonana na watu hao na siyo utapeli.

Mwanamke mmoja ameeleza jinsi alivyowasiliana na mwanaume aliyejitambulisha kuwa ni mwanajeshi wa 
Jeshi la Marekani aliyeko vitani nchini Afghanistan. Akasema mwanaume huyo alijitambulisha kwa ubin wa jina la Advisor, mzaliwa wa Houston, Texas.

Timu ya Dk Phil ikachukua vitabu vyote vya posta ili kutafuta jina la "Advisor" na ajabu ni kuwa halikupatikana hata jina moja, si tu katika kitabu cha orodha ya majina cha Texas, bali pia katika vitabu vya majimbo 50. Dk Phil alikuwa akijaribu kumwelewesha mama huyo kuwa hiyo pekee ni dalili ya kuwa mtu huyo hayupo (does not exist).

Timu ya Dk Phil ilikwenda mbali kwa kujaribu kutafuta kwenye mitandao mbalimbali majina ya mtu anayejiita 'Advisor' na ilifanikiwa kupata majina zaidi ya 26 kwenye tovuti tofauti, yote yakiwa na picha na maelezo ya mtu yule yule mmoja. Hapa nako Dk Phil alijaribu kumwelewesha mama huyo kuhusu matapeli kutumia majina tofauti tofauti ili kukamilisha lengo lao.

Mwishowe Dk Phil alichambua ujumbe kwenye 'chat session' kati ya mama huyo na 'Advisor' ambapo alimweleza makosa makubwa ya kiuandishi ambayo mzaliwa wa Marekani na Texas hawezi kuyafanya, na jinsi ambavyo aina hiyo ya uandishi inatumiwa na matapeli kutoka nchi za Asia au Magharibi mwa Afrika.
Alimwelewesha pia kuwa lengo la tapeli huyo kukataa kuzungumza kwenye simu siyo kama alivyosingizia kuwa katika eneo la mapigano alipo hairuhusiwi kuwasiliana na raia hivyo anajiiba kwa kutumia chat, bali ilikuwa ni mbinu ya kuzuia asigundulike kirahisi lafudhi yake ambayo ingetilia mashaka uraia wake wa Texas.

Tapeli huyo baadaye alimhadaa kuwa anaweza kuzungumza ila amezuiliwa mahali kutokana na matatizo na hivyo anasubiri kuokolewa. Dk Phil aliamua kupiga namba ya simu ambayo tepeli huyo alikuwa anaitumia kumpigia huyu mama, na hapo Dk Phil akamwuliza yeye ni raia wa Texas katika eneo lipi la Houston? (tapeli akakata simu), Dk Phil akampigia tena, akamwambia mawasiliano huenda mabovu, ila anapenda kufahamu anwani yake ili amsaidie kutoka alikotekwa nyara, mara hii pia tapeli alikata simu. Muda wote huu akizungumza, lafudhi yake ilikuwa si ya Kimarekani wala Kimexiko (nchi inayopakana na Texas) bali ya watu ambao baadhi yetu tumezoea kuzisikia lafudhi hizo kwenye sinema za Afrika Magharibi.

Mwanzoni mwa uhusiano wao huo, tapeli 'Advisor' alimwambia mama huyu jina la hospitali alikozaliwa, shule ya awali alikosoma n.k., lakini mara zote Dk Phili alipofuatailia taarifa hizi, si jina la hospitali, wala shule ya awali wachilia mbali chuo vilionekana kwa jina lolote. Hapa nako Dk Phil akatumia njia hii kumwelewesha mama huyu kuwa huu ni utapeli. Haiwezekani mtu azaliwe katika hospitali ambayo hakuna aliyewahi kuisikia, ama asome katika shule ambazo hazijawahi kuwa kwenye rekodi wala kusikika katika eneo hilo.

Dk Phil alipomwuliza mama huyo kuhusu kumbukumbu za fedha alizomtumia tapeli 'Advisor', aliorodhesha mara na kiasi cha fedha anchokumbuka kutuma kwa tapeli huyo kila alipotohadaa. Jumla yake ilikuwa dola za Kimarekani elfu sitini na tatu na ushee (takriban shilingi 100,000,000/= za Tanzania).

Mara zote hizo alizotuma fedha alikuwa anaamini kuwa anamsaidia 'Advisor' ambaye alimwahidi kuwa kuna kontena lenye dhahabu za thamani ya dola za Kimarekeni milioni moja, ambazo zitatumwa kwake na hivyo angeweze kurejesha fedha zake zote alizomtumia.
Kwa bahati mbaya, mama huyu na wengine ambao wametapeliwa (na pengine watakaotapeliwa siku zijazo), ni miongoni mwa wale wasiofahamu wala kujifunza kung'amua mbinu za kitapeli zinazotumiwa sana katika kudanganya watu na kuwaibia. Tapeli wa mama huyu alitumia njia rahisi ya kuzisoma hisia zake na kujua angekuwa mwepesi wa kuanguka mtegoni wa maana alikuwa anatafuta penzi (desperate for love) hivyo alimtumia maneno ya mapenzi aliyoyanukuu kutoka kwenye mitandao. Kwa mfano, Dk Phil alichukua baadhi ya maneno aliyoyabandika 'Advisor' kwenye chat session na mama huyo ya tarehe 4 Machi 2013, kuyakuta neno kwa neno, kituo kwa kituo, kwenye tovuti ya Pigbusters.net (sasa imehamia youreittoday.com)

Tapeli huyu alitumia picha za mtu halisi ambaye ni mwanajeshi halisi aliyefariki tangu mwaka 1994. Kwa bahati mbaya, hawa matapeli wanaweza kutumia hata tukio baya la kweli na wakaunganisha link ya habari kwenye tovuti marufu kama BBC, CNN n.k., ili uongo wao ufanane na ukweli.

Kuna usemi kuwa ukiwa unataka sana kukipata kitu, ni rahisi sana kupoteza fikira, ukaongozwa na hisia na moyo badala ya akili (following your heart and not your mind and reasoning) ni rahisi sana kukubali lolote unaloambiwa ikiwa linakidhi kiu yako.

Kisa cha mama huyu na wenziye kinazidi kutukumbusha kuwa:-

  1. Kuwa mjanja, usiwe mwepesi kumwamini kila mtu.
  2. Si kila kiandikwacho mtandaoni kinachosema ni cha kweli basi ni kweli na uhakika. 
  3. Mtu yeyote anayewasiliana nawe na kuanza kuomba kutumiwa fedha, huenda ni tapeli.
  4. Dalili za kutambua utapeli ni pamoja na mtu kuomba umtumie majina yako rasmi, anwani, tarehe ya kuzaliwa, namba za simu, maelezo ya akaunti za benki na hata password za email au benki.
  5. Unapotumiwa kiambatanisho kwenye email au chat session, usiwe mwepesi kukifungua kwani hata firewall na anti-virus zinaweza zisiwe na mbinu ya kung'amua ikiwa kuna virusi vimefungashwa kwenye kiambatanisho hicho ambacho ukikifungua utakuwa umefungulia njia virusi kuiba taarifa zako binafsi kama vile kunakili kila unapo-type password ya kufungua tovuti ya benki ama tovuti zenye taarifa zako za siri. Kwa bahati mbaya sana, utapeli huu pia umeziingilia simu za kisasa (smart phones) na virusi hutumwa kwa njia ya iyo hiyo ama kupitia apps au kwa kupokea link ya website na kuifungua bila kujua unatembelea tovuti ya virusi.