Posted Jumapili,Septemba8 2013 saa 11:4 AM
Kwa ufupi
Ilipofika siku ya ufunguzi wa michezo hiyo, jiji
lote la Christchurch lilizizima kwa hoihoi na shangwe. Niliwasili kwenye
Uwanja wa QE11 Park mapema asubuhi kiasi cha saa tatu hivi, ili
kujihakikishia nafasi nzuri ya kuweza kunasa vyema matukio muhimu ya
sherehe hizo.
Tido Mhando amefanya kazi ya utangazaji wa redio
kwa miaka mingi kwa hiyo, kwenye simulizi zake hizi za kila Jumapili,
anahadithia baadhi tu ya yale mengi na makubwa aliyokutana nayo wakati
wa enzi zake hizo. Jumapili iliyopita, Tido alielezea alivyowasili
Christchurch, New Zealand, kwenye michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola
ya 1974, sanduku lake likiwa limepotelea njiani. SASA ENDELEA…
Tuliwasili Christchurch Alhamisi, usiku tarehe 22
Januari, 1974 siku mbili tu kabla ya kuanza rasmi kwa michezo ya Nchi za
Jumuiya ya Madola. Na kwa kweli tulilikuta Jiji la Christchurch likiwa
tayari kabisa kupokea ugeni mkubwa wa wanamichezo na viongozi wao
wasiopungua 1,700 hivi.
Jiji lote lilikuwa limepambika kwa picha kubwa za
wanamichezo pamoja na mabango yenye maneno ya kuwakaribisha. Kuanzia
uwanja wa ndege, tuliweza kuona bashasha hizi wazi wazi nasi
zikatuongezea hamasa ya kutaka kushindana.
Tuliwajibika kwanza kupitia kwenye “kijiji cha
wanamichezo” ili kuwateremsha wale wetu wa Tanzania kabla ya sisi
waandishi wa habari kupelekwa katika hoteli tuliyokuwa tumepangiwa
kuishi kipindi chote cha michezo.
Tuliwasili kwenye kijiji hicho ambacho hasa
kilikuwa ni mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Canterbury hapo
Christchurch ambako tulikuta kukiwa na ulinzi mkali. Karibu kila sehemu
ilikuwa imezingirwa na wanajeshi. Tulielezwa kuwa hii ilikuwa ni mara ya
kwanza kwa michezo kama hiyo kuwa na ulinzi mkali kiasi hicho.
Hali hii ilitokana na kwamba michezo hiyo ya 1974
ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuwa na mkusanyiko mkubwa sana wa wanamichezo
wa kutoka sehemu mbalimbali za dunia tangu kumalizika kwa Michezo ya
Olimpiki ya 1972 kule Munich, Ujerumani.
Kwenye michezo hiyo ya Munich, wanamichezo 11 wa
Israel waliuawa baada ya kutekwa nyara na kikundi cha Wapelestina
kilichofahamika kwa jina la “The Black September”. Wateka nyara wanane
nao baadaye waliuawa na Makomando wa Kijerumani kwenye uwanja wa ndege
wa mji huo wakati walipokuwa tayari kutoroka.
Kutokana na tukio hilo, michezo ya Christchurch
ikawekewa ulinzi mkali kiasi hicho, ulinzi ambao umeendelea kutekelezwa
hadi leo hii kwenye michezo mbalimbali ya kimataifa.
Wanamichezo wetu hata hivyo walipokewa kwa
uchangamfu mkubwa na kuonyeshwa sehemu zao za malazi. Kwa hakika
ukarabati wa hali ya juu ulikuwa umefanyika kwenye mabweni hayo ili
kuwawezesha wachezaji wote kuishi hapo kwa raha mustarehe.
Baadaye, na sisi tulipelekwa hadi kwenye hoteli
yetu tuliyopangiwa. Ilikuwa ni “motel” ndogo tu lakini nzuri na nadhifu
iliyokuwa jijini, siyo mbali sana na mahali ambapo nilipangiwa kutuma
matangazo yangu ya kila siku ya michezo hii na pia hapakuwa mbali na
uwanja mkuu wa michezo hiyo wa QE11 Park.
Nilivutiwa sana na uzuri wa chumba nilichokuwa
nimepangiwa. Lakini ni lazima nikiri ya kwamba kilichonivutia zaidi ni
kuwepo kwa televisheni kwenye chumba kile. Hii ilikuwa ni mara yangu ya
kwanza kuona TV na mara ya kwanza kupata nafasi ya kuitumia!
Nadhani wenyeji wetu walihakikisha ya kwamba kwenye vyumba vyetu
hivi zipo hizi televisheni kwa kuwa kwa mara ya kwanza michezo hii
ilikuwa ikirusha matangazo ya televisheni ya rangi. Kutokana na
mazingira hayo, muda wote mwingine ambapo nilikuwa sipo kiwanjani,
nilikaa chumbani kuangalia televisheni. Wengine wangesema nilikuwa
naondoa ushamba.
Mapema siku ya pili yake, tulirejea tena kule
kwenye Kijiji cha Wanamichezo ili kushiriki katika sherehe ya
kuwakaribisha rasmi wanamichezo wa Tanzania kijijini hapo na ndipo
bendera ya Tanzania nayo ikapandishwa na kuwa miongoni mwa bendera za
nchi 38 zilizoshiriki kwenye michezo hiyo. Usiku huo nilikuwa
nimepangiwa kutuma ripoti yangu ya kwanza ya kutoka New Zealand.
Nikafurahi sana.
Kwa jumla wakati wote huu wa kipindi hiki cha
michezo, ilikuwa ni mimi peke yangu kutoka kwenye orodha ya Watanzania
waliokuwepo huko ambaye alikuwa na fursa ya kuongea na watu wa nyumbani
kila siku, maana siku hizo hali ya mawasiliano ilikuwa bado ni ngumu.
Kwa hiyo, kila siku jioni, saa mbili hivi nilikuwa
studioni nikipeperusha habari za yale yaliyotokea kwenye viwanja
mbalimbali vya michezo siku hiyo. Kabla ya hapo nilikuwa naunganishwa
kwa satalaiti na mafundi mitambo waliokuwa pale “control room” RTD. Na
hapo ndipo nilipokuwa nikipata michapo ya nyumbani.
Kulingana na tofauti ya saa tisa iliyokuwepo baina
ya Christchurch na Tanzania, taarifa zangu hizo zilikuwa zikisikika
moja kwa moja mnamo saa tano mchana huku nyumbani. Na nilikuwa naambiwa
na wale marafiki zangu mafundi mitambo akina Ali Said Tunku, John
Ndumbalo, Noel Namalowe na wengineo, kwamba watu walikuwa wanavutiwa
sana na kufuatilia matangazo hayo kwa umakini mkubwa.
Ilipofika siku ya ufunguzi wa michezo hiyo, jiji
lote la Christchurch lilizizima kwa hoihoi na shangwe. Niliwasili kwenye
Uwanja wa QE11 Park mapema asubuhi kiasi cha saa tatu hivi, ili
kujihakikishia nafasi nzuri ya kuweza kunasa vyema matukio muhimu ya
sherehe hizo.
Ilipofika saa sita, tayari uwanja huo ulikuwa
umefurika kupindukia. Mgeni rasmi kwenye ufunguzi huo alikuwa ni mume wa
Malkia Elizabeth wa Uingereza, Prince Phillip, huku wanafunzi wa shule
za msingi zaidi ya 2,500 wakishiriki kwenye tamasha la kuvutia, kukiwepo
pia na ngoma ya Wamaori, ambao ndio wenyeji asilia wa kisiwa hicho cha
New Zealand.
Kilele cha sherehe hizi kilikuwa gwaride maridadi
la wanamichezo wenyewe, zaidi ya 1250, wakiwa wamevalia mavazi rasmi,
wengi wao wakivaa mavazi yao ya taifa. Wasichana wa timu yetu ya
Tanzania walikuwa wamevaa mavazi marefu ya vitenge na wavulana wakiwa
wamevaa suti za rangi ya kijivu za mtindo wa Mao. Ilipendeza sana. Usiku
ule nikarusha kwa mbwembwe kubwa taarifa ya ufunguzi huo.
Wanamichezo wetu walianza mara moja kuonekana
kwenye viwanja mbalimbali vya michezo. Kulikuwepo na michezo 10
iliyokuwa ikishindaniwa kwenye kinyang’anyiro hicho na wachezaji wa
Tanzania walikuwa wakishiriki kwenye michezo minne: riadha, ngumi,
baiskeli na mpira wa vinyoya (badminton).
Hata hivyo, mambo hayakuwa yanakwenda vizuri hadi
siku ya tatu ya michezo hiyo wakati Tanzania ilipojinyakulia medali yake
ya kwanza wakati Clever Kamanya aliposhika nafasi ya tatu kwenye mbio
za mita 400 riadha ambazo zilitawaliwa na wanamichezo wa kutoka Afrika
ya Mashariki pekee.
Mshindi wa mbio hizi zilizokuwa na upinzani mkubwa
alikuwa ni Mkenya Charles Asati aliyetimka kwa muda wa sekunde 46.04,
akifuatiwa na Silver Ayoo wa Uganda aliyetumia sekunde 46.06 huku wakati
Kamanya wetu akichukua medali ya shaba kwa kutumia muda wa sekeunde
46.16.
Hii ikawa siku ya hoihoi kubwa kwenye kambi ya
wachezaji wa Tanzania na hata nami nilikwenda huko kushangilia na pia
kufanya mahojiano ya nguvu na wachezaji ikiwa ni pamoja na aliyekuwa
kiongozi wa timu ya wanariadha Elias Sulus.
Baada ya hapo bahati ikiwa siyo ya kwetu, pamoja na juhudi kubwa
waliyofanya wanamichezo wetu wengi waliishia kumaliza kwenye nafasi za
nne hasa wale wa ngumi na pia timu yetu ya riadha ya kupokeza viti mita
400 mara 4.
Lakini yote kwa yote matumaini yetu makubwa
yalikuwa kwenye mchezo wa mwisho kabisa wa michezo hiyo, hapo tarehe 2
Februari, mbio za mita 1500. Mbio ambazo siyo tu zilikuwa zikisubiriwa
kwa hamu kubwa hapo Christchurch, bali duniani kote.
Kwa mara ya kwanza kwa kipindi kirefu kwenye mbio
hizi, walikuwepo wakimbiaji mahiri sana duniani hasa hasa Ben Jipcho wa
Kenya, mwenyeji John Walker na nyota kutoka Tanzania, Filbert Bayi.
Hakika, huu ulikuwa ni mchezo wa fainali.
Usiku kabla ya siku hii, kambi ya Tanzania
ilipigwa na butwaa pale zilipopatikana habari ya kwamba Bayi alikuwa
hajisikii vizuri. Tulijikuta ghafla tukiwa wanyonge na kuanza kuwa na
masikitiko. Niliwafahamisha Watanzania nyumbani kuhusu hali hiyo, lakini
nikawaambia wasikate tamaa, mambo yalikuwa bado!
Siku hiyo ya siku, mnamo saa sita na nusu hivi,
Uwanja wa QE11 Park ukiwa umefurika kupita maelezo, nilijibanza pembeni
mwa sehemu ya kutangazia, huku mwili wote ukinizizima. Sikujua kama
nisimame ama niketi. Watu walikuwa wakipiga mayowe. Na ghafla kwenye
eneo la kukimbilia nikawaona wachezaji wakiingia, mmoja wao alikuwa
Filbert Bayi, akivalia fulana iliyokuwa na michirizi ya bendera ya
Tanzania kifuani.
Wakajipanga wote kwa utaratibu unaotakiwa na
majina yao kuanza kutangazwa, moja baada ya jingine. Uwanja ukalipuka
lilipotajwa jina la Filbert Bayi lakini ukatetemeka zaidi pale
lilipotajwa jina la mtoto wa nyumbani, John Walker. Na mara bunduki
ikapigwa.
Nikamwona ghafla Bayi akifyatuka kama risasi
kutoka kwenye mtutu wa bunduki, huyo peke yake, akiwa mbio mbele kwa
kasi ambazo hazijawahi kuonekana popote. Uwanja ukawa umelipuka kwa
gharika ya mayowe.
Nilishindwa kuvumilia kuangalia mkimbizano ule,
maana mara wenzake nao wakawa kama wamezinduka, John Walker akiwa amevaa
jezi yake nyeusi na Ben Jipcho nyekundu, wakawa wanakimbizana wao kwa
wao huku wakimfukuza Bayi.
Ilikuwa ni kama simba wawili wanaoshindana
kumkamata paa aliyenona wakiwa na uchu wa mwenye kupata apate. Nilijua
nashuhudia tukio la kipekee kabisa kwenye mchezo wa riadha, tukio ambalo
litabakia kuwa kumbukumbu kubwa kwangu, tukio la kihistoria kabisa.
Nikaanza kupata kizunguzungu, moyo ukinienda mbio kuliko kawaida, kichwa
kikaanza kuniuma, huku tumbo nalo likinguruma. Nikaamua kukimbilia
chooni. Hali ilikuwa mbaya.
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO...
source: Mwananchi
source: Mwananchi