Monday, 9 September 2013

Joe Robinson; Mlemavu wa macho hodari wa kutengeneza bustani


Posted  Jumapili,Septemba8  2013  saa 11:32 AM
Kwa ufupi
“Mwanzoni nilikuwa na wasiwasi kwamba huenda nisiweze kuotesha maua yangu vizuri,lakini watu wamekuwa wakitoka maeneo mbalimbali na kuja kujionea na kufurahia bustani yangu , na hivi karibu nilipata wenza kutoka New Zealand ambao walikuja kwa ajili ya kuona bustani hii”.


Bustani yake hiyo ina dazeni za vikapu vya maua vinavyoning’inia ambavyo vimebeba aina tofauti tofauti za maua mazuri ya kuvutia, jambo ambalo limewafanya hadi majirani zake kuona wivu kwa jinsi mazingira ya nyumba yanavyopendeza na kuvutia.
Licha ya kuwa juhudi za kikongwe huyo zinajidhihirisha waziwazi pale wageni na wenyeji wanapopita eneo hilo na kusifia bustani hiyo nzuri, lakini Joe mwenyewe hana uwezo wa kuona matunda ya jasho lake hilo kwa kuwa ni kipofu.
Joe alipata hitilafu katika macho yake na hivyo kupoteza uwezo wake wa kuona miaka 20 iliyopita, lakini bado vidole vyake viliendelea kupenda kuona na kuhisi hali ya kijani.
Katika eneo analoishi linalofahamika kama Crook katika jimbo la Durham, Joe anaweza kukusanya aina mbalimbali za maua kwa hisia na kugusa tu na kwa jitihada zake hizo ameweza kushida tuzo kadhaa.
Joe ambaye zamani alikuwa akifanya kazi katika kiwanda kilichopo jimboni humo anasema: “Nilipopata hali hii ya upofu, hilo halikunifanya niache kutengeneza na kupenda maua, japokuwa siwezi kukiona kile nikifanyacho, natumia ana hisia kwa kunusa na kugusa maua ninayoyapenda”
“Mwanzoni nilikuwa na wasiwasi kwamba huenda nisiweze kuotesha maua yangu vizuri,lakini watu wamekuwa wakitoka maeneo mbalimbali na kuja kujionea na kufurahia bustani yangu , na hivi karibu nilipata wenza kutoka New Zealand ambao walikuja kwa ajili ya kuona bustani hii”.
“Napenda sana aina zote za maua , japokuwa siwezi kuotesha mauaridi kwa wingi kama ilivyokuwa mwanzo kwa naogopa sana kuchomwa na miiba” anasema na kuongeza.
“Kwa kawaida huwa naanza mwezi wa tatu kwenda wa nne kwa kuanza kuotesha maua kwenye vitalu vidogo, wakati mwingine huwa inakuwa vigumu kuotesha na kisha kuyatoa kwa ajili ya kuyapanda, inahitaji umakini zaidi ili yasije kukatika na kushindwa kustawi kwenye vyungu, wakati mwingine huwa nahisi nikiwa napanda maua yangu watu husimama na kuniangalia sana na kuwasikia wakisifia jinsi bustani yangu ilivyo na mvuto” anasema.
Mkewe Joe, Heather ana mzio kwa maua, hivyo mara nyingi hatoi msaada wowote kwenye bustani, lakini wenza hao wanaye mjukuu Jamie ambaye husaidia kazi ya kuninginiza vikapu vya maua na shuguli za usafi bustanini.
Mstaafu huyo amepata vikombe kdhaa vya ushindi katika maonyesho ya maua yaliyofanyika jimbo analoishi katika miaka ya hivi karibuni, lakini kwa mwaka huu mashindano hayo hayakufanyika kutokana madhara ya msimu wa joto kwa mwaka 2011 na 2012.
Mkewe Heather 68, anasema: “Ninajivunia sana kuwa na mwanamume wa aina hii, akishaamua kufanya chochote bustanini hakataziki, bustani yetu ni nzuri sana na ina maua mengi ya kuvutia”.
“Hii ni pepo halisi ya mchanganyiko wa rangi za maua, wakati mwingine tunashuhudia magari yaskisimamishwa hapo nje huku watu wakishuka kwenye magari yao kuomba japo kuchuma ua bustanini.” Anasema Heather.

Joe anasema mara kwa mara huamka usiku wa mnene na kuangalia maendeleo ya bustani yake, na wakati mwingine hufurahia zaidi anapogusa vile vikapu vya maua vinavyoninginia na kujiridhisha kuwa vipo na vinazidi kumfurahisha.
Licha ya bustani hiyo ya kuvutia ambayo amefanikiwa kuistawisha mbele ya nyumba yake, pia ana miti ya matunda, michikichi na miti mingi ya kudumu muda mrefu ambayo ameiotesha upande wa nyuma ya nyumba yake, lakini anasema amesikitishwa na kitendo cha mkewe Heather baada ya kuukata mti wa tufaa wakati ilikuwa mapema kufanya hivyo.
“Ninaweza kuzungukia bustani yangu na kuangalia maendeleo ya maua yangu mazuri na mara nyingi watu huamini kuwa naona, nimekuwa nikiwasikia wakinong’ona kichinichini kuwa, ‘anaona huyo’” anasema na kuongeza.
“kama ningelikuwa naona mbona ningekuwa nawafukuza na kuwaambia tokeni msiharibu maua yangu, hii ni kwa sababu bustani yangu naijua vizuri sana , nimeiweka kwa aina ambayo binafsi nina uwezo wa kutambua kila mahali na kila ua lilipo.’.
Makala hii imetafsiriwa na Jamila Kilahama kutoka Gazeti la Daily Mail la Uingereza.
source: Mwananchi