Monday, 9 September 2013

CUF: Ndugai anahujumu

Na Aidan Mhando, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Septemba9  2013  saa 8:53 AM
Kwa ufupi

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema, Cuf inalaani vitendo vya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kudai kuwa inaonyesha wazi CCM wanampango wa kutengeneza katiba ya upande mmoja.

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (Cuf), kimesema kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kuamuru askari wa Bunge wamtoe nje ya ukumbi huo ni kumhujumu Rais Kikwete kwenye azma yake ya kupata Katiba Mpya.
Pia, chama hicho kimesema kinafanya juhudi za kuwasiliana na viongozi wa vyama vingine ili kuweka mkakati wa pamoja wa kukabiliana na hujuma dhidi ya mchakato wa kupata Katiba Mpya na kuimarisha umoja wa kitaifa  kwenye kipindi hiki cha kukabiliana na changamoto za nchi jirani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema, Cuf inalaani vitendo vya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kudai kuwa inaonyesha wazi CCM wanampango wa kutengeneza katiba ya upande mmoja.
“Kwa mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, kwa Tanzania Waziri Mkuu na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ndiyo wanawakilisha pande mbili ndani ya Bunge, hivyo kumnyima Mbowe fursa ya kuzungumza ni unyanyasaji na udhalilishaji na kwamba kitendo hicho hakikubaliki,” alisema.
Profesa Lipumba alisisitiza muswada uliokuwa unajadiliwa  ulikuwa na utata, Serikali imeubadili kwa nguvu na kuondoa maoni muhimu ya wadau.
source: Mwananchi