Monday, 9 September 2013

Maelfu hatarini kukosa mtihani kidato cha nne 2013

Dk Joyce Ndalichako 

Na Fredy Azzah, Mwananchi

Posted  Jumapili,Septemba8  2013  saa 1:0 AM
Kwa ufupi
Tayari Necta imetuma barua kwa watahiniwa hao kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani mwaka huu.


Dar es Salaam. Watahiniwa 3,000 wa kujitegemea wako hatarini kutofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutokuwa na taarifa zao za kulipia karo za mtihani huo pamoja na zile za usajili.
Tayari Necta imetuma barua kwa watahiniwa hao kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani mwaka huu.
Licha ya maelezo hayo ya Necta, taarifa zinaonyesha kuwa watahiniwa hao walishalipa ada za mtihani huo kupitia njia mbalimbali za kielektroniki zilizoainishwa na baraza hilo, ikiwamo benki na kampuni za simu za mkononi.
Watahiniwa walipaswa kulipa Sh35,000 ikiwa ni ada za mtihani huo kupitia wakala mbalimbali walioteuliwa na Necta.
Gazeti hili lilifanikiwa kuona barua ya Necta kwenda kwa mmoja wa wanafunzi waliojisajili kufanya mtihani huo kwa mwaka 2013 ikimweleza kuwa, hataweza tena kufanya mtihani huo kwa kuwa hakulipa karo ya mtihani huo.
Barua hiyo ilieleza kuwa, kumbukumbu za Necta zinaonyesha kuwa wanafunzi hao wamejiandikisha kufanya mtihani, lakini hawajawasilisha fomu za usajili wala kulipa karo za mtihani huo.
“Hivyo kwa barua hii, unafahamishwa kuwa umeondolewa kuwa mtahiniwa mwaka 2013,” ilisema sehemu ya barua hiyo zilizosambazwa kwa watahiniwa hao.
Kutokana na kuwepo hali hiyo, baadhi ya watahiniwa kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameanza kufuatilia Necta kujua hatima yao wakiwa na vielelezo vya malipo yao.
Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alithibitisha kuwa baraza hilo liliandika barua kwenda kwa watahiniwa takriban 3,000 waliokuwa wamejiandikisha kama watahiniwa binafsi na kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani huo kwa mwaka huu.
Alifafanua kuwa, baadhi yao walifika Necta wakiwa na stakabadhi zilizothibitisha kuwa wamelipa karo hiyo na hivyo kurudishwa kwenye kundi la watakaofanya mtihani huo mwaka huu.
“Necta hatupokei fedha moja kwa moja, tuna mawakala, kilichotokea ni kuwa baadhi ya watu walilipa karo za mitihani, lakini kwenye mfumo wetu tulikuwa hatuoni kama walilipa,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo watu wote walioandikiwa hizo barua ni wale ambao kwenye mfumo wetu hawaonekani kama wamelipa, lakini wengi wa hawa walikuja na risiti zikionyesha kuwa walikuwa wamelipa na wakarudishwa kwenye mfumo,” alisema.

Alipoulizwa ni wanafunzi wangapi ambao tayari walikuwa wamelalamika na kurejeshwa kwenye orodha ya watakaofanya mtihani huo mwaka huu, Nchimbi alisema mpaka wiki ijayo watakuwa na idadi ya waliothibitisha kuwa wamelipa fedha hizo.
“Mfumo wetu sisi uko sawa, hauna tatizo lolote. Na siwezi kusema ni wapi tatizo lilitokea, lakini ninachojua ni kuwa suala hilo kwa sasa linashughulikiwa,” alisema.
Alieleza kwamba, wiki ijayo wataweza kujua ni watahiniwa wangapi bado wana matatizo, kwani utaratibu wa kupanga namba za watahiniwa utakuwa umekamilika.
Alisema pia kuwa, idadi hiyo inaweza kuonekana kubwa kutokana na baadhi ya walioomba kurudia mtihani huo kuahirisha kufanya hivyo, baada ya matokeo ya mtihani wa taifa yaliyotangazwa mara ya pili kuwawezesha kuendelea na kidato cha tano ama mfumo mwingine wa elimu ya juu.
Alisema kwamba, kwa wale ambao wamepata barua na walishalipa karo hiyo, wanatakiwa kupeleka stakabadhi zao za malipo hayo Necta ili warudishwe kwenye kundi la watahiniwa watakaofanya mtihani huo mwaka huu.
Kwa mwaka 2012 watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne walikuwa 68,804 ambapo wasichana walikuwa 34,605 sawa na asilimia 50.30, huku wavulana wakiwa 34,199 sawa na asilimia 49.70.
Kati ya watahiniwa hao, waliofanya mtihani walikuwa 61,001 wakiwamo wasichana 30,918 na wavulana 30,083. Watahiniwa 7,803 sawa na asilimia 11.34 hawakufanya mtihani huo.
Hata hivyo, kutokana na matokeo ya mwaka jana kuwa mabaya zaidi yakilinganishwa na yale ya mwaka juzi, ilitarajiwa kuona idadi kubwa zaidi ya watahiniwa wakijiandikisha kufanya mtihani huo mwaka huu kama watahiniwa wa kujitegemea. Jumla ya watahiniwa wote waliosajiliwa kufanya mtihani huo mwaka jana walikuwa ni 480,029, wakiwamo wasichana 217,587 na wavulana 262,442 na waliofanya mtihani huo walikuwa ni 458,139 sawa na asilimia 95.44.
Mfumo wa udahili kwa kutumia mtandao wa kompyuta ulikwaza pia baadhi ya wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali chini ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).
Hivi karibuni Necta ilikumbwa pia na utata katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne yaliyokuwa kwenye mtandao, hali iliyolazimisha Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kulitolea ufafanuzi.
source: Mwananchi