Na Daniel Mjema,Mwananchi
Posted Jumatatu,Septemba9 2013 saa 8:35 AM
Posted Jumatatu,Septemba9 2013 saa 8:35 AM
Kwa ufupi
Mnyika alisema baada ya CCM kuhodhi muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kulifanya Bunge la Katiba liwe
ni hodhi ya chama hicho tawala karata pekee waliyobakiwa nayo ni kura ya
maoni...
Dodoma. Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kimesema kitatumia nguvu ya umma kuikataa Katiba
Mpya endapo CCM na Serikali yake: “vitaendeleza hila na ubabe katika
mchakato unaoendelea.”
Pia chama hicho kikuu cha upinzani nchini,
kimeitaka Serikali kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura kabla ya
upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Mpya huku kikisema kinyume chake
suala hilo litaibua mgogoro mkubwa.
Kauli hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa
chama hicho, John Mnyika katika mahojiano yaliyofanyika Mjini Dodoma
mwishoni mwa wiki.
Mnyika alisema baada ya CCM kuhodhi muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kulifanya Bunge la Katiba liwe
ni hodhi ya chama hicho tawala karata pekee waliyobakiwa nayo ni kura ya
maoni... “Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ndiye
atakayeteua wajumbe 166 kutoka taasisi na makundi na kufanya Bunge zima
la Katiba kuwa na wajumbe zaidi ya 600.”
Alisema kwa sasa, Tanzania Bara hakuna utaratibu wa kikatiba wa namna ya kuendesha kura ya maoni na kuongeza.
“Wenzetu Zanzibar katika Katiba yao wanao mfumo wa
kura ya maoni, sisi haupo ni lazima tutengeneze sheria ya kura ya maoni
ya Katiba Mpya na Sheria ya kura ya maoni ya Muungano,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema Kamati ya Bunge la Katiba, Sheria
na Utawala inapaswa kuanza kukutana kwa dharura kupata maoni ya wadau
kuhusu kura ya maoni na ianze na Zanzibar ambayo haikushirikishwa.
“Kamati ianze sasa, isisubiri Bunge la Oktoba 29
maana kati ya mambo yaliyoifanya Serikali kuondoa muswada wa Sheria ya
Kura ya Maoni ni mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Muungano,”
alisema.
Alisema pia Tanzania inahitaji kuwa na Katiba ya
mpito ambayo itaweka chombo huru kitakachosimamia upigaji wa kura ya
maoni badala ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mbowe alisema Serikali ya CCM inatumia hila na
ubabe kuhakikisha inapatikana Katiba Mpya itakayobeba masilahi ya chama
hicho kwa gharama yoyote.
“Endapo CCM itaendelea na hila zake hizi
niwaambie Chadema tumejipanga… Tutatumia teknolojia ya kisasa kuwafikia
Watanzania hata ikibidi kutumia helikopta nne ili waikatae wakati wa
kupiga kura ya maoni,” alisema Mbowe na kuongeza: “Hila yoyote
itakayotokea kwenye Katiba tutahamasisha Watanzania kuikataa, wasifikiri
wanachokifanya ni salama kwao… Wanageuza mchakato kuwa wa kichama
badala wa wananchi.”
Alisema msimamo wa CCM kukataa mapendekezo ya
muundo wa Serikali tatu si wa wanachama wake wa kawaida, bali matakwa ya
viongozi wake wa juu.
“Tunapozungumzia kumdhibiti Rais, wao (CCM) wanafikiri
tunamzungumzia Rais Kikwete (Jakaya)… Tunataka kudhibiti madaraka ya
Rais yeyote ajaye awe wa Chadema, CCM au NCCR”.
Alisema mapendekezo ya wananchi kuhusu Serikali
tatu yalianzia wakati wa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe mwaka 1984 na
baadaye mwaka 1991 wakati wa Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali.
Alisema pamoja na kutotekelezwa kwa mapendekezo
hayo ya wananchi, bado wabunge wa G55 walianzisha vuguvugu hilo lakini
likazimwa kwa kutumia nguvu kubwa.
“Tume ya Jaji Robert Kisanga nayo ilikuja na
mapendekezo hayohayo na sasa Tume ya Jaji Joseph Warioba na bado CCM
haitaki kuamini ni ya wananchi,” alisema.
Mbowe alisema ndiyo maana Chadema sasa kimeamua
kujitoa mhanga kuwahamasisha hadi wanachama wa CCM kuikataa Katiba Mpya
endapo itapatikana nje ya matakwa ya Watanzania... “ Nia tunayo, sababu
tunayo na uwezo tunao.”
Alisema matumizi ya polisi hayatalipatia taifa
Katiba Mpya na nzuri. “Wajue kuwa wako Watanzania wenye busara kwa
mamilioni walioko nje ya Bunge ambao wana sauti katika Katiba yao na CCM
wasifikiri wao ni alfa na omega (mwanzo na mwisho),” alisema Mbowe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia amesema hata kama Tanzania haitapata Katiba Mpya hadi ifikapo
2015, bado ya sasa haitafaa kutumika.
“Hata kama tutashindwa kupata Katiba Mpya hatuwezi
kwenda kwenye uchaguzi na katiba hii ya sasa kwa sababu katiba mpya ya
Zanzibar imejiingiza katika mgogoro na Katiba ya Muungano,” alisema.
Alisema kama dalili za kutopatikana kwa Katiba
Mpya zimeanza kuonekana, ni vyema ikatumika busara na hekima katika
kuvuka kikwazo hicho na njia pekee ni meza ya mazungumzo.
“Sisi siyo tutakaoifanya Tanzania isitawalike,
bali CCM… Tunafanya haya kwa nia njema kabisa, hatutaki damu ya
Watanzania imwagike kwa jambo linaloepukika,” alisema.
source: Mwananchi
source: Mwananchi