Monday, 4 November 2013

MBUNGE ALIYEOLEWA NA KIJANA MDOGO ADAI KUWA KIJANA NDO ALIMNG'ANG'ANIA


Hatimaye Mbunge Rosweeter Kasikila (60), aliyefunga ndoa na kijana mwenye umri wa miaka 26, amefunguka kwa kusema aliyeng'ang'ania kufunga ndoa hiyo ni kijana mwenyewe licha ya kumtahadharisha tofauti ya umri wao.

Kasikila alitoa kauli hiyo jana, baada ya kutakiwa kujibu shutuma zilizotolewa na mumewe huyo, Michael Christian (26) ya kung'ang’ania vyeti vyake vya elimu kwa lengo la kumtaka arudi nyumbani.


Christian aliyefika katika ofisi za NIPASHE jana alitoa nakala ya barua aliyoituma kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuomba atumie uwezo wake wa kisheria ili mbunge huyo amrudishie vyeti vyake alinavyovishikilia.

Kufuatia maelezo hayo, NIPASHE ilimtafuta Dk. Nchimbi kwa njia ya simu ili athibitishe kupokea nakala ya barua hiyo lakini simu yake ilikuwa imezimwa.

Nakala nyingine za barua hiyo zilitumwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Haki za Binadamu kwa jamii-Madhehebu ya dini nchini, Askofu William Mwamalanga, Mchungaji wa Kanisa la Assembilies of God, Mikocheni B, Mchungaji Getrude Rwakatare na vyombo vya habari.

Akijibu shutuma hizo, mbunge huyo alisema hajawahi kung'ang'ania vyeti vya kijana huyo wala kulazimisha ndoa kama anavyodai Christian.

"Nahisi kuna watu wanamtumia ili wanichafue, siwezi kung'ang'ania vyeti, kwanza vya kazi gani kwangu, ukweli ni kwamba Michael, shida yake anataka nichafuliwe, kwangu aliondoka wakati sipo, sasa hivyo vyeti nimeving'ang'ania saa ngapi," alisema na kuongeza:

"Mwaka jana nikiwa Dodoma nilipata taarifa ameondoka nyumbani, kweli nilivyorudi nilikuta amechukua vitu vyake vyote kasoro tu vile nilivyomnunulia, hivyo vyeti anavyosema nimeving'ang'ania mbona hajawahi kutamka mbele yangu zaidi nimeona kwenye magazeti," alihoji.

Alisema baada ya kufika nyumbani alipata taarifa kuwa, mume wake huyo amepanga chumba na anaishi na mwanamke mwingine (askari) ambaye ni mjamzito.

Alisema utaratibu alioutumia kijana huyo wa kumchafua kwenye magazeti siyo sahihi na kumshauri angeenda mahakamani au kanisani kama aliona haitaki ndoa tena.

Aliongeza kuwa yeye na Christian walifahamiana mwaka 2009 baada ya kufiwa na mume wake aliyemtaja kwa jina moja la Mushi.

"Sikumtongoza kama anavyosema, alikuja katika hospitali ya Bagamoyo akitokea chuo cha Red Cross wakati huo nilikuwa Muuguzi Mkuu, aliponiona alinipenda alianza kunitongoza, nilimkatalia na kumwambia mimi ni mtu mzima sana kwake, " alisema na kuongeza:

"Alikuwa ananitumia email (barua pepe) za kunitaka, nilimwambia umri wangu ni mkubwa, lakini yeye alikuwa ananiambia kwenye vitabu vya dini kuna sehemu gani kumeandikwa umri," alisema.

Alisema alijikuta ametumbukia kwenye penzi la kijana huyo na kuanza mahusiano naye.

"Nina nakala zote za vidhibitisho ambavyo alikuwa akinitumia kunitongoza nimevichapisha kama vielelezo vyangu, tena wakati tumeanza uhusiano Taasisi ya Safina ambayo ilikuwa ikimsaidia katika masomo yake, ilinipigia simu," alisema na kuongeza:

"Safina walitaka kujua kama nina mahusiano na huyu kijana niliwajibu ni kweli, waliniambia kama ndiyo hivyo wanafuta kumsaidia kwa sababu wao huwasaidia wale ambao hawana uwezo, yatima, " alisema.

Alisema wakati taasisi hiyo ikimfuta, ilikuwa imemlipia Christian sehemu ya ada ya masomo aliyokuwa akiyachukua."

"Nililazimika kumlipia ada ya mwaka wa pili na watatu wa masomo yake pamoja na mambo mengine na ilifika kipindi aliniambia anataka kunioa, ndipo tulipofanya mchakato ambapo nilitolewa mahari na ndoa ilifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kutangazwa mara tatu," alisema.

Alisema Christian alifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kutoa mahari ya Sh. 200,000 na baada ya harusi alipelekwa Kondoa kwa ndugu wa kijana huyo.

"Huko tulienda kati ya mwezi Julai au Agosti, mwaka jana, tulifanyiwa sherehe za kimila na ndugu za mume wangu ambao ni baba mdogo, bibi mzaa baba yake na shangazi, pia ndugu zake wa Kimara na Dodoma wananijua, " alisema.

Hata hivyo, mbunge huyo alipoulizwa kama ndoa hiyo ipo sasa hasa kufuatia shutuma hizo, alisema hawezi kujua kwa sababu mume wake aliondoka bila kumuaga na kwa sasa anaishi na mwanamke mwingine toka Novemba mwaka jana.

Alisema wakati wa mahusiano yao wafanyakazi wenzake Christian walikuwa wakimhoji kwa nini ameamua kuwa na mtu mzima kama (mbunge), lakini yeye aliwajibu hakuna umri kwenye biblia.

Alipoulizwa kama ana mpango wa kuchukua hatua dhidi ya kijana huyo, mbunge huyo alisema hana mpango.

Mbunge huyo alijitetea kuwa, hakumlazimisha kufunga ndoa na kwamba wakati kijana huyo akimtongoza, alimweleza kuwa hawezi kuzaa kwa sababu umri wake umeshapita.   
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI