Na James Magai
Posted Jumanne,Septemba17 2013 saa 19:57 PM
Posted Jumanne,Septemba17 2013 saa 19:57 PM
Kwa ufupi
Wakili wa utetezi, Evod Mmanda alisema haikuwa
sahihi kwa upande wa mashtaka kuwasilisha taarifa hiyo mahakamani hata
kabla ya uamuzi wa Mahakama.
Dar es Salaam. Kesi ya dawa za kulevya
inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina
la Mama Leila au Naima Mohammed Nyakiniwa na wenzake wanane, imeendelea
kugubikwa na utata wa kisheria na kuzua mvutano uliosababisha iahirishwe
kwa mara nyingine ili kusubiri uamuzi wa Mahakama.
Jana, Mahakama Kuu ilitengua hoja iliyozua mvutano
mkubwa juzi kwa kuruhusu upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya
kuongeza shahidi muhimu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Eva
Mamuya jambo lililopingwa na upande wa utetezi.
Mbali ya Mama Leila, washtakiwa wengine katika
kesi hiyo ni Anthony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote
Wakenya). Wengine ni Watanzania watano, Sarah Munuo, Almas Said, Yahya
Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Juma Mzome na John William.
Wakati upande wa utetezi ukipinga uamuzi huo wa
jana, upande wa mashtaka ulitoa hoja nyingine ya kuongeza shahidi wa
pili, ASP Neema na kuibua mvutano mkali wa kisheria uliomlazimu Jaji
Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi hiyo, kuiahirisha hadi Ijumaa wiki
hii atakapotoa uamuzi kama upande wa mashtaka ulikuwa sahihi au la
kuwasilisha notisi hiyo mahakamani kabla ya uamuzi wa jana.
Mvutano wa kisheria
Ubishi ulianza mapema mahakamani wakati Jaji
Mwakipesile alipokuwa akijiandaa kusoma uamuzi wake juu ya maombi ya
upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi.
Wakili wa utetezi, Yassin Member alisimama na
kumwomba jaji kutokusoma uamuzi wake kwani tayari walikuwa na notisi ya
upande wa mashtaka ya kuongeza ushahidi wakati ni kinyume cha sheria.
Member alilalamika kuwa upande wa mashtaka uliomba
kuongeza shahidi mmoja lakini notisi ilionyesha walikuwa wanataka
kuongeza mashahidi wawili.
“Mheshimiwa tunaomba usisome kwani tunashangaa
tayari tumepewa notisi ya upande wa mashtaka wakati ukiwa bado hata
hujatoa uamuzi wa maombi yao ya kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi.
Kibaya zaidi wanataka kuongeza mashahidi wawili na siyo mmoja,” alisema
Member.
Jaji Mwakipesile alijibu kwa kutaka upande wa
utetezi kuipa nafasi mahakama kutoa uamuzi wake wa maombi ya upande wa
mashtaka yaliyosababisha kesi hiyo kuahirishwa juzi.
“Ipe nafasi Mahakama kutoa uamuzi wake wa ombi la
upande wa mashtaka la kuahirisha kesi ili waweze ku-file notice
(kuwasilisha taarifa) ya additional witness (shahidi wa nyongeza), jambo
ambalo ninyi mlipinga,’’ alisema Jaji Mwakipesile na kisha kutoa uamuzi
wake na kukubali upande wa mashtaka kuongeza shahidi.
Uamuzi huo ulisababisha mvutano mkali mawakili wa
utetezi wakisema haikuwa sahihi kwa upande wa mashtaka kuongeza
mashahidi wakati ulishindwa kwenye Mahakama za chini wakati wa
usikilizwaji wa mwanzo.
Wakili wa utetezi, Evod Mmanda alisema haikuwa sahihi kwa upande
wa mashtaka kuwasilisha taarifa hiyo mahakamani hata kabla ya uamuzi wa
Mahakama.
“Mheshimiwa Jaji, Prosecution (upande wa mashtaka)
waliomba jana ahirisho ili waweze ku- file (kuwasilisha) hicho
walichokiomba (taarifa ya kumwongeza shahidi), ruhusa umeitoa leo kwenye
uamuzi wako, hivyo walitakiwa wa-file notice yao hiyo baada ya uamuzi
wako (wa leo),” alisema na kuongeza:
“Hivyo hakuna notisi halali hapa mahakamani.
Notisi halali ni ile watakayoiwasilisha baada ya uamuzi wako. Kwa hiyo
sisi tunasema kuwa hadi sasa hakuna notisi halali ya kuita mashahidi wa
ziada.”
“Kama Mahakama yako itaikubali hii wanayoita
notisi, ingawa sisi tunasema siyo notisi halali, basi tunaomba Mahakama
yako ione kuwa haikutolewa ‘in a reasonable time’ (wakati mwafaka).”
Pia alidai kuwa hata hiyo taarifa inayodaiwa na
upande wa mashtaka kuwasilishwa, walipewa muda mfupi baada ya kuingia
mahakamani na kwamba upande wa mashtaka katika maombi yao juzi walimtaja
shahidi mmoja, Mamuya, lakini taarifa waliyopewa inawataja mashahidi
wawili.
Wakili Mmanda aliiomba Mahakama chini ya Kifungu
cha 289 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), iamue kama
huo ni wakati mwafaka, kwa kuzingatia vigezo vya mazingira na wakati
ambao upande wa mashtaka ulibaini umuhimu wa kuwaongeza mashahidi hao.
“Hawa wanatajwa kuwepo katika mchakato tangu
mwanzo. Mamuya anakiri kupokea kifurishi (bahasha yenye vielelezo) Juni
16, 2011, hadi leo ni miaka miwili na miezi mitatu imepita. Hivyo
walijua uwepo wa Mamuya mapema. Huu si wakati mwafaka,’’ alisema Wakili
Mmanda.
Hata hivyo, alisema hawana maelezo ya maandishi ya
Mamuya wala ya ASP Neema huku akidai kuwa maelezo ya ASP Neema
yanaonyesha kuwa yameandikwa Juni 11, mwaka huu wakati hatua ya maelezo
ya kesi ilishakamilika.
Hoja hizo za Wakili Mmanda ziliungwa mkono na
Wakili mwingine wa utetezi, Jamhuri Johnson ambaye pia alidai hadi
wakati huo alikuwa hajaona taarifa ya upande wa mashtaka kuongeza
mashahidi.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Prosper
Mwangamila alidai kuwa katika kesi zote za jinai si jukumu la upande wa
mashtaka kuwapatia upande wa utetezi nyaraka mbalimbali wanazokusudia
kuzitumia katika kesi, bali Mahakama.
“Notisi wanayoitaja iko mahakamani tangu jana,
hivyo utaratibu uliotumika wao kupata nyaraka nyingine ndiyo unaotumika
kuwapatia notisi hii. Hivyo hoja ya upande wa mashtaka kuchelewa kuwa
‘serve’ (kuwapatia) haina msingi,” alisema Wakili Mwangamila.
Alisema taarifa hiyo iko mahakamani kisheria kwa
mujibu wa Kifungu cha 289 (1) na (2) cha CPA na kuiomba mahakama ione
kuwa imewasilishwa katika muda mwafaka.
Alisema endapo itaona kuwa haikuwasilishwa kwa muda mwafaka,
kinachopaswa kufanyika si kuiondoa, bali kuwapa muda zaidi upande wa
utetezi ili kuipitia.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Mwakipesile aliahirisha kesi hiyo hadi keshokutwa, Ijumaa, atakapotoa uamuzi wake.
Washtakiwa wawavaa waandishi
Washtakiwa wa kesi hiyo jana walizua patashika wakati waandishi wa habari walipokuwa wakipiga picha mahakamani hapo.
Mshtakiwa wa nane katika kesi hiyo, Mzome alianza
kuwa mkali ndani ya Ukumbi wa Mahakama alipotaka kwenda kuwavamia
wapigapicha hao. Washtakiwa wenzake nao walicharuka wakizuia kupigwa
picha jambo lililowalazimu askari wa Magereza kuwadhibiti na kisha
kuwafunga pingu.
Muda mwingi, washtakiwa katika namna ya kukwepa
kupigwa picha walificha nyuso zao kwa vitabu huku wanawake wakijifunika
kwa mitandio.
SOURCE: MWANACHI
SOURCE: MWANACHI