Mhe.
Waziri Bernard K. Membe (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, akiongea na waandishi wa habari jana mchana katika Ofisi za
Wizara ya Mambo ya Nje. Kulia ni Balozi Vincent Kibwana, Kaimu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Baadhi ya waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Balozi
Celestine Mushy (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa
Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Bw. Elibariki Maleko (kulia),
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo
ya Nje wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Balozi
Dora Msechu (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika
Wizara ya Mambo ya Nje na Bw. Omari Mjenga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje nao wakimsikiliza
Mhe. Waziri Membe.
Mhe. Waziri Membe akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yake na waandishi wa habari alipokutana nao jana Wizarani. (Picha nyingine zote na Tagie Daisy Mwakawago).
Waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe. (picha hii na Reginald Philip).
Na Ally Kondo
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard K. Membe (Mb)
ameuambia Umma wa Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa Serikali ya Tanzania
haijamfukuza mtu yeyote nchini mwenye sifa za ukiimbizi kama
inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Mhe.
Waziri aliyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake
jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 06 Septemba, 2013.
“Serikai
haikumfukuza mkimbizi yeyote isipokuwa iliwafukuza wahamiaji haramu,
Aidha, wahamiaji haramu hao walipewa onyo la kuondoka nchini na wengi
wao wametii kabla ya operesheni maalum ya kuwatia mbaroni haijaanza”
Waziri Membe alisikika akisema.
Kuhusu
hoja kuwa operesheni ya kuwafukuza wahamiaji haramu inawalenga
Wanyarwanda, Waziri Membe alisema kuwa hoja hiyo sio ya kweli. Alisema
kuwa hadi kufikia wakati huu zaidi ya wahamiaji haramu 31,000 wameondoka
nchini. Kati ya hao Warundi ni 21,000, Wanyarwanda ni 6,000 tu na
waliobaki ni kutoka nchi nyingine..
Mhe.
Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa Tanzania imekuwa kimbilio la
wakimbizi kwa muda mrefu na hadi sasa inahifadhi wakimbizi zaidi ya laki
4. Wakati wote wakimbizi wamekuwa wakipewa huduma nzuri na haijawahi
kusikika kuwa Tanzania inalaaniwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa au Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali inawanyanyasa wakimbizi.
Sambamba
na taarifa hiyo, Mhe. Waziri aliwaambia waandishi wa habari kuhusu
mikutano inayofanywa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (Kenya, Uganda na Rwanda) bila kuhusisha nchi nyingine
wanachama wa jumuiya hiyo.
Mhe.
Membe alisema kuwa yeye binafsi hana tatizo na mikutano hiyo endapo tu,
imepata kibali cha Wakuu wa Nchi wa EAC pamoja na kutoa ripoti ya
masuala yanayozungumzwa katika vikao vya jumuiya. “Mimi binafsi sioni
tatizo kwa nchi hizo kukutana endapo zimepewa Baraka na Wakuu wote wa
Nchi wa EAC na ripoti za mikutano yao kuwasilishwa katika vikao rasmi
vya jumuiya” alisema Mhe. Membe.
Aliwatoa
shaka Watanzania kutokuwa na hofu na mikutano hiyo kwa kuwa Tanzania ni
nchi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo hainabudi nchi
nyingine kuitegemea kutokana na rasilimali zilizopo na jiografia yake.
Alihitimisha
mazungumzo yake kwa kusema kuwa anaamini vikao vinavyofanywa,
vinafanywa kwa nia njema pasipo kuwa na dhamira ya kuleta mgawanyiko
ndani ya jumuiya. Na endapo vinafanywa kwa dhamira ya kuleta mgawanyiko
basi muda wa kurekebisha hali hiyo upo.
source: Dewji blog