Tuesday, 24 September 2013

Mwanamke Mwingereza adaiwa kuongoza shambulio la Westgate



Askari wa Kenya wakiwa wamejipanga kwa ajili ya kuwadhibiti watuhumiwa waliovamia na kuteka watu kwenye Jengo la Westgate Mall mjini Nairobi jana. 
Na  Waandishi Wetu

Posted  Jumanne,Septemba24  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Awali askari wa Kenya walieleza kuwa mwanamke aliyevalia hijab ndiye aliyeongoza kati ya watu 10-15 wenye silaha kuvamia jengo hilo.


Nairobi/Dar es Salaam. Mwanamke mmoja raia wa Uingereza ametajwa na gazeti moja la nchi yake kuwa ndiye aliyeongoza shambulizi la kigaidi lililofanywa katika eneo la maduka la Westgate jijini Nairobi, Jumamosi iliyopita.
Gazeti la Daily Mail la Uingereza lilikariri vyanzo vyake ndani ya duru za usalama za Kenya ambavyo vilieleza kuwa magaidi hao wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa Kundi la kigaidi la Al-Shabaab la Somalia waliongozwa na mwanamke anayeitwa Samantha Lewthwaite maarufu kwa jina la White Widow (Mjane Mweupe).
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku amesema wanaamini kuwa magaidi waliovamia jengo hilo la Westgate wote ni wanaume.
Ole Lenku alisema baadhi ya watekaji hao walivalia nguo za kike ili kuwachanganya watu na kwamba tayari wawili kati yao wameshauawa na vikosi vya usalama.
Wakati Ole Lenku akisema hayo, Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi alisema kuwa wanajua magaidi hao wanatoka wapi lakini hakutaka kueleza zaidi.
Lewthwaite anayeaminika kuwa na umri wa miaka 29, alifiwa na mumewe, Jermaine Lindsay baada ya kulipua bomu la kujitoa muhanga Julai 7, 2005 jijini London, Uingereza.
Kundi la Al-Shabaab ambalo limekiri kuhusika na shambulizi hilo, kupitia mtando wa Twitter lilitoa taarifa jana likimsifia Lewthwaite, ambaye siku hizi anatumia jina la Sherafiyah.
“Sherafiyah Lewthwaite a.k.a Samantha ni mwanamke shujaa na tunajivunia kuwa naye. Askari wetu wa Mujahideen wamejitolea kufa katika operesheni hii.”
Milio ya silaha nzito na mabomu ilisikika kwenye eneo hilo la Westgate wakati wa mapambano kati ya polisi na magaidi hao.
Awali askari wa Kenya walieleza kuwa mwanamke aliyevalia hijab ndiye aliyeongoza kati ya watu 10-15 wenye silaha kuvamia jengo hilo.
Maofisa wa usalama wa Kenya ambao hawakupenda kutajwa majina walikaririwa wakisema kuwa watu wengi waliokuwa wameshikiliwa na magaidi hao walikuwa wameachiliwa na bado jitihada zilikuwa zinafanyika kuwaokoa mateka waliobakia.
Kwa mujibu wa Daily Mail, mbali ya Lewthwaite, raia wengine wa Uingereza wanaohusishwa na tukio hilo ni Liban Adam (23) na Ahmed Nasir Shirdoon (24), ambao pia wametajwa kwenye taarifa ya Al-Shabaab.

Kundi hilo limesema kuwa limefanya shambulizi hilo kwa nia ya kuishinikiza Serikali ya Kenya kuondoa vikosi vyake ndani ya Somalia.
Lewthwaite ni nani?
Lewthwaite, ambaye alikulia katika eneo la Buckinghamshire ni binti wa mwanajeshi wa zamani wa Uingereza.
Katika kipindi cha utoto wake Lewthwaite alipendelea zaidi kusomea muziki wa disco.
Anatokea katika familia ya Kikristo na aliamua kuingia kwenye Uislamu kabla ya kuolewa na Lindsay.
Mwanamke huyo anadaiwa kuwa amekuwa akiendesha mafunzo ya kigaidi kwa wanawake akiwa Somalia na Kundi la Al-Shabaab.
Lewthwaite alifahamiana na marehemu mumewe Jermaine Lindsay kupitia intaneti.
Wakati Lindsay alipohusishwa na shambulizi la kigaidi mwaka 2005 jijini London, Lewthwaite alimshutumu mumewe kwa kitendo kile.

SOURCE: MWANANCHI