
Kwa ufupi
Ni ule wa kupandisha tozo za magari iliyopandishwa na nchi hiyo kwa madai ya kufanya ulinganifu.
Dar es Salaam/Dodoma. Wakati ushuru wa magari 
makubwa ukiwa umeshushwa kwa wiki moja, Serikali ya Rwanda imejitetea 
ikisema haijafanya hujuma yoyote dhidi ya Tanzania, bali imepandisha 
tozo hiyo ili kuifanya ilingane na ile inayolipwa Tanzania.
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake jana, 
Balozi wa Rwanda nchini, Ben Rugangazi alisema kuongezwa kwa ushuru huo 
wa forodha kisichukuliwe kama jaribio la kutaka kuvuruga uhusiano kati 
ya nchi hizi mbili.
Balozi Rugangazi alisema Rwanda imeamua kupandisha
 kiwango chake kutoka Dola za Marekani 152 (Sh240,000) kuwa Dola 500 
(Sh790,000) ambazo pia hutozwa na Serikali ya Tanzania kwa muda mrefu.
“Kumekuwa na majadiliano ya muda mrefu ili kuleta 
ulinganifu wa ushuru wa forodha kwani kwa muda mrefu wafanyabiashara 
Rwanda wamekuwa wakilalamika kutokana na kushindwa kushindana vizuri 
kwenye soko la biashara kutokana na tofauti kubwa ya ushuru wa forodha.
“Hili suala tulishawahi kuliwasilisha katika 
Jumuiya ya Afrika Mashariki tukawaomba wasaidie kurekebisha kasoro hiyo,
 lakini hawakufanya hivyo. Sasa tumeamua kuchukua hatua hii ili kwenda 
sambamba na wenzetu Tanzania.
“Pande zote Tanzania na Rwanda zilikubaliana kuwa 
ushuru mpya ungeanza kutumika Septemba mwaka huu na ndivyo ilivyokuwa,” 
alisema Balozi Rugangazi.
Siku saba
Kutokana na msongamano wa malori kwenye mpaka wa nchi hizo mbili, Serikali ya Rwanda imeshusha ushuru kwa wiki moja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma 
jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema ushuru 
unaotumika ni ule wa zamani badala ya mpya.
Tizeba alisema alishauriana na Waziri wa 
Miundombinu wa Rwanda, Profesa Silas Rwakabamba na kukubaliana ushuru wa
 zamani utumike wakati Serikali hizo zikiendelea na mashauriano. Alisema
 Mawaziri wa Fedha wa Tanzania na Rwanda walitazamiwa kukutana ili 
kuzungumzia suala hilo.
Dk Tizeba alisema juzi wafanyabiashara wa Tanzania
 walipata usumbufu mkubwa baada ya kulazimika kulipa Dola 500 kuingiza 
mizigo yao Rwanda badala ya Dola 152.
Hata hivyo, alikanusha madai kuwa Rwanda imepandisha ada hizo kutokana na mgogoro wa kisiasa baina ya nchi hizo.
Hali mbaya Rusumo
Hatua hiyo inatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika 
mpaka wa nchi hizo huko Rusumo kutokana na kuwapo kwa msururu mkubwa wa 
magari ambao unaelezwa kuwa hadi jana ulikuwa umefikia kilometa 20.
Akizungumza kwa simu kutoka Rusumo, Ngara jana, 
Ofisa Mfawidhi wa kituo cha Uhamiaji mpakani hapo, Mahirande Samuel 
alisema hali hiyo inatokana na madereva wengi kutokuwa na taarifa ya 
ongezeko hilo.
“Hali ni mbaya, kwa sasa foleni ya magari imefika 
hadi Benaco ambako ni umbali wa kilometa 20… Unajua hawa madereva 
hawakuwa na taarifa na wengi walikuwa wakitoa ushuru wa zamani, pengine 
wameamua kusubiri mabosi wao wawaongezee fedha,” alisema Samuel.
Haiondoki Bandari ya Dar lakini...
Kuhusu utumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam balozi
 huyo alisema Serikali yake haina mpango wa kuikacha bandari hiyo, 
lakini akasisitiza: “Sisi tunaangalia fursa za kiuchumi, tutapenda 
kutumia bandari yenye ufanisi na ambayo haina usumbufu kwetu. 
Tutaendelea kutumia bandari zote hii ya Dar es Salaam na ile ya Mombasa 
lakini tungependelea zaidi kuona tunatumia ile yenye ufanisi zaidi.”
source: Mwananchi
source: Mwananchi