Na Mwinyi Sadallah
Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 20:13 PM
Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 20:13 PM
Kwa ufupi
Kamishna wa Chuo cha Mafunzo (Magereza)
Zanzibar, Khalifa Hassan alisema wamelazimika kuomba mwongozo kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) ambaye kwa niaba ya Serikali ndiye
aliyemfungulia mashtaka.
Zanzibar. Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya ya
Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumuki), Sheikh Azzan Khalid Hamadan,
amebainika kuwa figo zake zina vijiwe na matibabu yake hayawezekani
kufanyika Zanzibar, imefahamika.
Sheikh Azzan na wenzake tisa walifunguliwa
mashtaka Oktoba mwaka jana, wakituhumiwa kufanya uharibifu wa mali na
kusababisha hasara ya Sh500 milioni.
Pia wanatuhumiwa kuhatarisha usalama wa taifa
kinyume na kifungu cha 3(4) sura ya 47 ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya
mwaka 2002.
Akizungumza na Mwananchi jana, daktari mmoja
bingwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, alisema mawe yaliomo katika figo
za Sheikh Azzan yamekuwa yakimsababishia maumivu na hakuna njia ya
kuokoa maisha yake zaidi ya kusafirishwa nje ya nchi.
Hata hivyo daktari huyo hakutaka jina lake
litajwe. Alisema vifaa kwa ajili ya tiba ya Sheikh huyo havipatikani
Zanzibar wala Tanzania Bara na kwamba ni vya kisasa.
Kwa mujibu wa daktari huyo, tiba yake hufanyika
kwa mgonjwa kuwekewa kifaa maalumu mgongoni kinachopitisha mawimbi
yanayosaga mawe kwenye figo yaani Extracorporeal shock wave Lithrotripsy
(ESWL).
Alisema baada ya mawe hayo kusagwa kwa kutumia
mawimbi, chembechembe za vijiwe huhamia katika kibofu na baadaye kutoka
kupitia njia ya mkojo.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Omar Abdallah
Ali, alithibitisha mgonjwa kukabiliwa na matatizo ya figo na kwamba
daktari anayemtibu atalazimika kuwasilisha ripoti yake kwa bodi.
Kamishna wa Chuo cha Mafunzo (Magereza) Zanzibar,
Khalifa Hassan alisema wamelazimika kuomba mwongozo kwa Mkurugenzi wa
Mashtaka Zanzibar (DPP) ambaye kwa niaba ya Serikali ndiye
aliyemfungulia mashtaka.
“Hatutaki kufanya mambo kinyume na utaratibu,
kinachotakiwa ni kupata mwongozo kwanza ili kusitokee utata...taarifa ya
Jamhuri ambayo ndiyo iliyomshtaki,” alisema.
“Kesi kama hii ni ya kwanza kutokea huku mahabusu
wakiwa chini ya dhamana yetu, tumelazimika kuomba mwongozo kwa DPP kujua
kama anaweza kutibiwa nje au la,” alisema Kamishna huyo.
Hata hivyo, DPP Ibrahim Mzee Ibrahim mara kadhaa
alipopigiwa simu yake ilikuwa ikiita bila majibu hata baada ya kutumiwa
ujumbe wa maneno, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Kwa muda mrefu tangu kukamatwa kama kiongozi huyo wa kikundi cha Uamsho, afya ya yake imekuwa ikizorota siku hata siku kutokana na kukabiliwa na matatizo hiyo ambayo sasa inaelezwa anatakiwa kusafirishwa nje kwa matibabu.
source: Mwananchi
Kwa muda mrefu tangu kukamatwa kama kiongozi huyo wa kikundi cha Uamsho, afya ya yake imekuwa ikizorota siku hata siku kutokana na kukabiliwa na matatizo hiyo ambayo sasa inaelezwa anatakiwa kusafirishwa nje kwa matibabu.
source: Mwananchi