Monday, 16 September 2013

Taifa la vyama vingi, katiba ya chama kimoja


 Posted  Jumapili,Septemba15  2013  saa 12:46 PM
Kwa ufupi
  • Haya, baada ya kufanya mazoezi kidogo kwa kutwanga mtoto hadi mama watoto alitahayari niliamua kusoma barua nyingine.


Kama kawaida yake, Bunge letu tukutu limeleta muvi tamu sana. Tena wameongeza utamu kwa kuleta muvi za vitendo badala ya manenomaneno tu. Kwa kweli watu wengi siku hizi hatukosi vipindi vya Mjengo kwa kuogopa kukosa uhondo. Nani anasikiliza maneno yao? Raha vitendo bwana.
Ndiyo maana nilipata barua nyingi wiki hii.
Makengeza ng’wanamasumbwi
Hujambo bwana? Umefanya mazoezi leo?
Usicheke. Hata wazee msibaki nyuma. Mimi nashangilia lakini sishangai kwamba hatimaye tunacheka na Cheka, tumepata bondia aliyeshinda taji la kimataifa maana kwa masumbwi sisi hatujambo. Tena napendekeza tuanzishe mitalaa rasmi kwenye shule zetu. Hebu fikiria:
• Kwa masumbwi nyumbani hatujambo. Watu wanatwangana kila siku. Mara mume kwa mke, mara wazazi kwa watoto, mara nyumba kubwa kwa nyumba ndogo. Inavyoonekana wengi bila kutwanga, wanaona wana kasoro. Kwa nini wasifundishwe kupigana kisayansi?
• Sheria ya viboko shuleni imefunikwa kabisa na walimu viboko ambao licha ya kutofuata sheria kuhusu nani anaruhusiwa kupiga viboko, kwa wakati gani na idadi gani, wanaona njia bora ni makonde na ngumi.
• Hali yetu ya daladala inaeleweka. Bila ngumi ngumu wanafunzi wengi wataingiaje kwenye daladala huku sisi wazee tunaangalia tu. Na wakichelewa nyumbani sisi wazee tunafanya mazoezi ya ngumi kwao eti wamekuwa wahuni siku hizi.
• Bila kusahau wanaopenda kufanya mazoezi ya masumbwi kwa wezi wadogo kwa sababu wamekakamaa zaidi na kuacha wezi wakubwa eti ni laini mno hawawezi kupigwa, waabudiwe tu.
Na sasa nifurahi sana kwamba hata waheshimiwa wetu wa sponji wameachana na ulainilaini wao na kuamua kuonyesha mfano bora kwamba bila kupigana hakuna maisha. Ila tu, nawalaumu wale wote ambao walipenda kujificha nyuma ya vyombo vingine vipige kwa niaba yao badala ya kuingia ulingoni wenyewe. Pigo ni uhai na bila kupiga, miili yetu inadhoofika. Tena nashangaa hawa wengine wanaopenda kupiga nyumbani au shuleni lakini wanalaani wanaotuwakilisha kwa kufanya vilevile tunavyofanya nyumbani kwetu. Nchi ya masumbwi yahitaji mifano bora ili tupevuke katika ngeu.
Kwa hiyo anza mazoezi sasa. Usibaki nyuma!
Haya, baada ya kufanya mazoezi kidogo kwa kutwanga mtoto hadi mama watoto alitahayari niliamua kusoma barua nyingine.


Mwishiwa Makengeza,
Najua wewe huna busara nyingi ndiyo maana umeshindwa kuponyesha makengeza yako miaka yote hii lakini kwa kuwa nimekata tamaa na wakalia sponji na kuwaona wenye hasara badala ya busara, nimeamua angalau nichokoze nyinyi wenye upungufu kibao labda mtanionyesha njia. Iwapo wenye macho mazuri wanatuongoza hadi shimoni, si bora kuwafuata wenye makengeza.
Tuchukue mfano wa katiba. Kwanza sikubaliani kabisa na watu ambao wanasema kwamba katiba inatakiwa kuwa ya wananchi, si kitu cha wanasiasa. Maisha ni siasa, uamuzi wa kuwa na vyama vingi au chama kimoja ni siasa, kuweka haki za binadamu ndani ya katiba ni siasa, kuamua kutoa kipaumbele kwa hiki au kile ni siasa. Na kama kila kitu ni siasa na wananchi wote hawana msimamo mmoja hiki au kile, ni dhahiri kwamba wamba ngoma watawamba kweli. Shida yangu ni wawambe tu siyo kuwanga.
Ndiyo. Mabosi watakuwa na msimamo mmoja na wafanyakazi wao? Mkulima anayetaka kuuza mazao ili apate kupeleka mtoto wake shuleni atakuwa na msimama mmoja na mfanyakazi anayetaka kununua chakula kwa bei nafuu ili alishe watoto wake? Vijana watakuwa na msimamo mmoja na wazee? Wabinafsi na walafi wanaotaka kuneemeka juu na noma za watu wengine watakubaliana kweli na wanaotaka maendeleo ya wote? Thubutu! Ndiyo maana katiba ni mawasiliano, ni kuvutana na kuelekezana na kushawishiana hadi kufikia mwafaka ambao unazingatia maslahi ya watu wote si wa kundi moja tu.
Na katika hayo inabidi kuwa wataalamu wa hesabu pia. Hebu fikiria kuna uamuzi ngapi unayohitaji hesabu. Tunataka kuhesabu tuwe na nchi ngapi, serikali ngapi, marais wangapi, waheshimiwa wa sponji wangapi, walaji wa jasho letu wangapi, haki ngapi katika zile zinazotambulika kimataifa, wateule wa mtu mmoja wangapi, hesabu kali kwelikweli. Na bila kusahau wangapi wa kutuamulia tuwe na katiba ya aina gani.
Lakini si hivyo tu. Ndani ya hisabati kuna hesabu za uwiano pia. Haitoshi kujumlisha tu, ni lazima kutafuta uwiano unaokubalika. Pia hesabu za kanuni ambazo nazo zinaendana na uwiano moja kwa moja.
Ndipo hapo napata wasiwasi kama kweli waheshimiwa wetu wa sponji wamesoma hesabu kweli. Sikatai kwamba hawakubaliani kwenye kujumlisha maana wengine wanajumlisha kikompyuta na wengine wanatumia hesabu za mwaka uleee. Lakini wenye uwiano na kanuni nashangaa. Ni kama hawajawahi kusikia hesabu zingine kabisa. Wote wanadai kwamba wanataka katiba ambayo inaleta mwafaka na maelewano, na wote wanapaswa kujua kwamba mwafaka na maelewano hutokana na uwiano na kanuni. Kwa mfano iwapo a = 8 na b = 3, huwezi kuandika kwamba a = b. Unaweza kuwalazimisha watu waimbe a = b lakini iwapo, kwa mfano, unajaribu kujenga kitu, au kufanya biashara kwa hii a = b, matokeo yake ni janga moja kwa moja.
Ndiyo maana nakimbilia kwako Makengeza, wewe na wenzio ambao hamtaki kulazimishwa a = b. Utajengaje mwafaka wakati robo tatu wako kwenye kundi moja na wanajaribu kulazimisha asilimia tisini wawe wa kundi moja hilohilo. Kwanza hawajui hesabu, na pili, katika kulazimisha uwiano na kanuni, hawalitakii mema taifa letu hata kidogo. Na tatu, wanaonyesha kiburi kile cha dhambi ya asili, eti wao wanajua kila kitu, uamuzi wao wote ni sahihi, matakwa na mawazo ya makundi mengine yote ni batili. Hawawezi hata kutambua kwamba ili kujenga mwafaka wapaswa kufikiria mawazo ya watu wengine. Na mwisho wameonyesha dhahiri kwamba wanajali maslahi yao tu ndiyo maana hesabu za uwiano na kanuni wamezipiga marufuku katika mitaala ya hisabati kwa sababu inaleta mawazo mabaya kwenye fikra za watu.
Kweli huwezi kuwa na nchi ya makundi mengi na katiba ya kundi moja au nchi ya vyama vingi lakini katiba ya chama kimoja au nchi ya madhehebu mengi lakini katiba ya dhehebu moja. Bora watangaze kabisa kwamba hawajui kuhesabu zaidi ya moja. Nchi moja, chama kimoja, amri moja, mteule mmoja, mwenye uamuzi moja na kadhalika. Lakini wasitudanganye kwamba wanapenda hesabu kubwakubwa na hesabu za kisasa huku hawajui kabisa.
Mwalimu wa Hisabati
Uzuri wa walimu wa hisabati ni kwamba ni watu wa mantiki pia. Ndiyo maana huyu mwalimu amechambua kimantiki. Lakini ubaya wa walimu wa hisabati na hata sisi wengine wengi ni kwamba tunaamini watu wote wanafuata mantiki.
Hasa katika kutafuta katiba yenye tiba bila kutibua Hivyo wanangoja mantiki itawale huku maslahi na mihemko imeshafukuza mantiki zamani au kuifungia jela.

 Lakini tusiposimama na kutetea mantiki, kila kikundi kisipokuwa tayari kuvuta kwake pia hati tunavutana kwa uwiano, ngoma itapasuka nakuambia.

SOURCE: MWANANCHI