Na Waandishi wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Septemba23 2013 saa 8:19 AM
Posted Jumatatu,Septemba23 2013 saa 8:19 AM
Kwa ufupi
Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi
vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa
wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia
kupambana nao.
Bado jengo hilo limezingirwa na wanajeshi, kuhakikisha magaidi hao hawatoki nje kuhatarisha usalama wa wananchi.
Nairobi. Magaidi wanaokadiriwa
kuwa kati ya 10 na 15 wamelitikisa Jiji la Nairobi kwa siku mbili
mfululizo baada ya kuteka jengo kubwa la biashara la Westgate lililopo
Westlands na kuua watu wapatao 69 hadi leo asubuhi.
Magaidi hao walivamia jengo hilo juzi saa tano
asubuhi na hadi jana, jitihada za kuwadhibiti zilikuwa hazijafanikiwa.
Zaidi ya watu 1,000 wameokolewa na wengine zaidi ya 170 wamejeruhiwa.
Tukio hilo limesababisha shughuli mbalimbali
katika Jiji la Nairobi kusimama na hata maduka mengine makubwa ya
Nakumatt kufungwa, hivyo kusababisha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali
kuwa shida kwa wakazi wengi wa Nairobi.
Wakazi wengi wa eneo la Westlands jana walikwama
kufika katika maeneo yao na watu wengi waliokuwa kwenye jengo hilo
waliacha magari yao na kukimbia huku na huko ili kujiokoa huku vyombo
vya usalama vikiwataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo.
Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi
vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa
wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia
kupambana nao.
Risasi zimekuwa zikisikika usiku kucha na watu
zaidi wameendelea kuuawa huku Serikali ikisema mateka wanaodaiwa kuwepo
ndani ya jengo hilo wakiwa chini ya magaidi hao ni 30.
Jengo hilo limezingirwa na vyombo vya usalama vya
ndani na nje ya Kenya vikiongozwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya pamoja
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), David Kimaiyo, ambaye amekuwa akitoa
taarifa mbalimbali za tukio hilo kupitia account yake ya Tweeter ili
kuhakikisha vyombo vya habari na jamii vinajua kinachoendelea.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitoa
taarifa kupitia mitandao yake, huku televisheni zote za Kenya zikirusha
tukio hilo moja kwa moja tangu lilipotokea juzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole
Lenku akizungumza na vyombo vya habari alisema watu 69 waliouawa ni
pamoja na raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali. Hata hivyo, alisema
haijajulikana ni wangapi na wanatoka nchi gani haswa.
Canada imethibitisha kuwa raia wake wawili wameuawa kwenye tuko hilo, pia raia wawili wa Ufaransa nao wameuawa.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na
tukio hilo ambalo ni kubwa kutokea Kenya tangu ubalozi wa Marekani
ulipolipuliwa mwaka 1998 jijini Nairobi.
READ MORE : mwananchi.co,tz
READ MORE : mwananchi.co,tz