Monday, 9 September 2013

Usichokijua kuhusu Askofu Moses Kulola


Cancel

Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na vitukuu 16. Alifungua makanisa zaidi ya 4,600 ya EAGT ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Zambia, Malawi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC). Lakini ana nyumba moja tu aliyojengewa na waumini.


Posted Jumatatu,Septemba9 2013 saa 11:10 AM
Kwa ufupi
Kwa mujibu wa Askofu wa EAGT Sengerema, Joshua Wawa, Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na vitukuu 16.
 
Ni vigumu kuzungumzia historia ya vuguvugu la uanzishaji makanisa nchini, pasipo kumtaja Askofu Moses Kulola.
Askofu Kulola anajulikana na wengi kama mtu aliye na nia ya dhati kutangaza neno la Mungu, kutokana na kile kinachoonekana wazi kwamba hakujilimbikizia mali kama ambavyo tunaona baadhi ya watumishi wa Mungu siku hizi wanavyomiliki majumba, benki na hata magari ya milioni ya shilingi.
Hali halisi
Kwa namna inavyoonekana nchini, ni kama kuna kundi kubwa la watumishi wanaohubiri kwa lengo la kushibisha matumbo yao zaidi; Hawana mpango thabiti wa kusaidia yatima wala maskini, badala yake waumini ndio wanaonyonywa kwa kutoa zaka na sadaka ambazo baadhi yake hata matumizi yake yamekuwa yakizua maswali
Utumishi wa Mungu na mali
“Hakuna shaka kwamba kama kila nyumba ya ibada Tanzania ingekuwa na mpango thabiti wa kusaidia watu maskini, yatima na watu wengine wenye hali ngumu, hali ya maisha ingekuwa nzuri zaidi kwa wengi. Lakini wapi, baadhi ya watumishi wako ‘bize’ kujaza matumbo, wanaendesha magari ya kifahari yenye thamani ya mamilioni ya shilingi badala ya kutumia fedha hizo kutangaza neno la Mungu au kusaidia wasiojiweza,” anasema Charles Mtanga, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam.
Mtanga anawashauri viongozi wa nyumba za ibada kuwa na mkakati wa kusaidia yatima na watu wengine wasio na uwezo, huku wakiendelea kutangaza neno la Mungu, ili wote waweze kuufurahia ulimwengu.
Utanuzi wa huduma
Kwa mujibu wa Askofu wa EAGT Sengerema, Joshua Wawa, Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na vitukuu 16.
Katika uhai wake, Askofu Kulola alifungua makanisa 4,600 ya EAGT ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Zambia, Malawi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) na ameacha wosia kwamba makanisa yafunguliwe kadiri inavyowezekana.
Hata hivyo, licha ya kuwa na wingi wote huo wa makanisa, Askofu Kulola anamiliki nyumba moja iliyoko mkoani Mwanza aliyojengewa na waumini.
Askofu Moses Kulola

“Yoooh! Unapenda niseme?” hicho ndicho kilikuwa ‘kibwagizo’ cha Askofu Moses Kulola wakati wa uhai wake hasa alipokuwa akihubiri mikutano ya injili.
Askofu Kulola alifariki Agosti, 29 mwaka huu katika Hospitali ya AMI (African Medical Investments) iliyopo Slipway jijini Dar es Salaam.
Mikakati mingine
Askofu huyo mkuu wa EAGT, ameelezewa kuwa amewahi kwenda Ikulu mara kadhaa kuombea nchi kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete alishuhudia hayo wakati wa maziko yake yaliyofanyika Bugando, jijini Mwanza kwamba kwa namna inavyoonekana Askofu Kulola alikuwa ana maanisha kuifanya kazi ya Mungu.
Kufungwa na kunusurika kuuawa
Askofu Kulola amewahi kufungwa gerezani kwa ajili ya kuhubiri injili, pia amewahi kunusurika kifo katika ajali. Rais Kikwete anamzungumzia kama mchungaji aliyekuwa mkweli na aliyeutumia muda wake kusaidia wote bila kujali imani zao za dini.
Maisha yake
Katika maisha yake, Kulola alisoma Shule ya Msingi ya Ligsha Sukuma, mwaka 1939 baadaye akajiunga na taasisi ya usanifu mwaka 1949. Alibatizwa mwaka 1950 katika Kanisa la AIC Makongoro. Alimwoa Elizabeth.
Mwaka 1959 alianza kufanya kazi serikalini, wakati huo huo akihubiri injili katika miji na vijiji. Utumishi wake serikalini ulifika mwisho mwaka 1962, aliamua kujitolea moja kwa moja katika kazi ya kutangaza neno la Mungu.
Mwaka 1964 alijiunga na chuo cha theolojia na kuhitimu 1966. Aliendelea na masomo ya theolojia ndani na nje ya nchi.
Alihudumu kama mchungaji katika Kanisa la AIC kabla ya kuhamia madhehebu  ya Pentekoste mwaka 1961-1962 na alifanya kazi katika Kanisa la TAG 1966 mpaka 1991 alipoamua kuanzisha Kanisa la Evangelistic Assemblies God (EAGT) baada ya kutokea mgogoro wa kiuongozi.
Kisa cha Askofu Kulola kuanzisha kanisa lake
Katika kitabu cha Historia ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God, mwandishi Dk Jotham Mwakimage anasimulia kiini cha mtafuruku uliolikumba kanisa hilo miaka ya 1980 kiasi cha kusababisha mgawanyiko mkubwa. Anasema kulikuwa na mikutano mikuu ya kanisa hilo kati ya mwaka 1980 na 1982.
“Mkutano mkuu wa mwaka 1980 ulikuwa wa kipekee kwa wale waliohudhuria, kwani ulitawaliwa na ujumbe wa kinabii zaidi, ulifanyika kwenye jengo la udongo lililoko Chuo cha Biblia Dodoma,” kinasema kitabu hicho na kuongeza:
“Kwa mtazamo wangu, mkutano huu haukuonekana kama mkutano wa shughuli za kikanisa, bali kama kusanyiko la uamsho wa kiroho katika kuwatia nguvu wachungaji wa TAG kwa ajili ya huduma za kichungaji.”
Dk Mwakimage anaendelea kusema kuwa kulikuwa pia na mkutano wa aina hiyo pia mwaka 1982. Lengo la mkutano huo uliofanyika pia Dodoma lilikuwa ni kuchagua viongozi wakuu wa kanisa hilo na hapo ndipo kanisa lilipopasuka.
“Sababu ya mgawanyiko ilitokana na ule mtafaruku uliokuwa kati ya wainjilisti wawili mashuhuri waliokuwa na mvuto ambao ni Emmanuel Lazaro aliyekuwa Askofu Mkuu wa TAG na Moses Kulola. Ushawishi wa viongozi hao kiroho ulikuwa mkubwa na uligusa watu wengi,” anasimulia.
Anasema ushawishi huo uliwagusa siyo waumini tu wa kanisa hilo, bali hata wamisionari waliolisaidia kanisa hilo.
“Viongozi hawa hawakukubaliana katika mambo ya msingi na mgongano wao ukawagusa watu wengi na matokeo yake hayakuweza kuepukika.”
“Kabla ya mwaka 1982, sheria ndogo ya uhamisho iliongezwa katika Katiba ya TAG. Katika mwaka huo, uongozi wa TAG chini ya Askofu Lazaro ulitumia mamlaka ya kikatiba kuwahamisha baadhi ya wachungaji muhimu ndani ya mfumo wa huduma ya kanisa hilo,”
“Uhamisho huo haukueleweka vizuri… hasa uhamisho wa Mchungaji Calist Masalu wa Kanisa la Temeke ambalo lilikuwa ndiyo kituo kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli za Moses Kulola.”
“Wachungaji, washirika na hata wamisionari hawakuelewa sababu za kuwahamisha wachungaji hao, hivyo wakatafsiri kwamba kumhamisha Mchungaji Masalu kulilenga kuharibu huduma ya uinjilisti za Kulola. Kwa sababu hiyo Mchungaji Masalu akagoma kuhama, akisubiri uamuzi wa mkutano mkuu”. Dk Mwakimage aliyekuwa mjumbe katika mkutano huo uliotawaliwa na minong’ono ya uhamisho wa wachungaji anasema uchaguzi ulifanyika na Lazaro kuchaguliwa kuwa askofu mkuu na Kulola kuwa msaidizi wake. Hata hivyo mambo yakazuka tena.
“Siku iliyofuata wakati wa kipindi cha shughuli, suala la uhamisho wa Mchungaji Masalu likajitokeza tena na hoja kama sharti la Kulola kuikubali nafasi yake hiyo ikaibuka. Kulola alinukuliwa akisema, “Kama uhamisho wa Mchungaji Calist Masalu kwenda Bugando Mwanza hautatangazwa, kuondolewa au kufutwa, basi siko tayari kupokea wadhifa mlionichagua.”
“Huo ndiyo ulikuwa msimamo wa Kulola,” anasema Dk Mwakimage na kuongeza:
“Baada ya hapo Askofu Mkuu Lazaro akasimama kujibu hoja akimpinga Kulola akisema; “Uhamisho wa Mchungaji Masalu utabakia na kamwe hautafutwa wala kubadilishwa”.
Ni kutokana na kauli hizi mbili zilizosigana ikawa ndiyo sababu ya mgawanyiko kutokea. Mgawanyiko huo kwanza ulizaa chuki na kashfa endelevu kati ya makundi hayo mawili hadi leo. Lakini kwa upande mwingine umeyaimarisha makundi hayo, kwani hadi sasa ni madhehebu yaliyokua.
TAG bado yaidai EAGT
Akizungumzia uhusiano kati ya TAG na EAGT hivi karibuni Askofu Mkuu wa TAG, Dk Barnabas Mtokambali, licha ya kusema kuwa makanisa hayo yana uhusiano mzuri, anaongeza kuwa bado kanisa lake linaidai mali zake EAGT. Anaongeza kuwa mwaka 1991 kabla Askofu Kulola hajasajili kanisa lake, Serikali ilimpa sharti la kurejesha mali za TAG ili apate usajili, ndipo alipoweka ahadi ya kurudisha jambo ambalo hakulifanya hadi anafariki.
EAGT haidaiwi
Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile akisema mgogoro uliopo ni wa kikatiba:
“Hakuna mali yoyote tunayodaiwa na TAG, tatizo letu lilikuwa ni la kikatiba tu,” anasema Mwakipesile. Kanisa la EAGT chini ya Askofu Kulola limeendelea kukua kwa kasi. Tofauti ya uongozi kati ya makanisa hayo mawili ni kwamba, EAGT imekuwa chini ya Askofu Kulola hadi mauti yanamkuta huku TAG ikibadilisha uongozi, kutoka Askofu Lazaro kuja kwa Ranwel Mwenisongole hadi askofu wa sasa Dk Barnabas Mtokambali.
source: Mwananchi