Monday, 9 September 2013

Wahamiaji walioolewa ruksa kuishi na wenza’



Rais Jakaya Kikwete
Na Phinias Bashaya, Mwananchi

Posted Jumatatu,Septemba9 2013 saa 9:38 AM
Kwa ufupi
Operesheni hiyo inafanyika kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete kutokana na kukithiri kwa uhalifu katika maeneo hayo.
Bukoba. Serikali imesema wahamiaji haramu walioolewa na Watanzania wanaruhusiwa kubaki nchini, hawalazimiki kuvunja ndoa zao ingawa wanatakiwa kupata kibali maalumu kutoka Idara ya Uhamiaji.
Akizungumza mjini hapa jana, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, alisema wahamiaji haramu walioolewa wanatakiwa kwenda Idara ya Uhamiaji kupata hati hizo.
“Hatupendi kuachanisha familia zilizoishi kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo, wanatakiwa kwenda uhamiaji kuhalalishwa na baadaye ikigundulika hana tatizo anaweza kupewa uraia,” alisema Kanali Massawe.
Pia, alisema kwa mujibu wa sheria, mhusika atapewa kibali alichokiita ‘Independence Pass’ kitakachomwezesha kuendelea kuishi nchini na kwamba, kinyume chake itakuwa ni kuvunja haki za binadamu.
Hata hivyo, Massawe alibainisha kuwa lazima zoezi la kuondoa wahamiaji haramu lifanyike, kwani walioondoka kwa hiari ni 11,601 na waliokadiriwa kuondoka ni kati ya 52,000 na 53,000, hivyo idadi kubwa bado wanaishi nchini.
Akizungumzia zoezi la kurudisha wahamiaji haramu lililoanza rasmi Septemba 6, mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma, Mkuu Msaidizi wa Operesheni hiyo, Simon Sirro, alisema tayari wamewakamata 1,851.
Pia, Sirro alisema ng’ombe 1,765, sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na bunduki saba vimekamatwa na kwamba, wahamiaji wanaokamatwa wanarudishwa kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia haki za binadamu.

source: Mwananchi