Kwa ufupi
Ni kamati ya maridhiano ya kina Hassan Nassor Moyo, Mansour na Ismail Jussa.Wataka iwe na sarafu yake, mambo ya nje na uhamiaji, isajili vyama vyake vya siasa 
Zanzibar.  Kamati ya Maridhiano
 imetoa maoni yake ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania kwa kutaka Zanzibar ijitegemee karibu kwa kila kitu.
Maeneo inayotaka yaondolewe kwenye Muungano ni 
uraia na uhamiaji, sarafu na Benki Kuu, mambo ya nje na usajili wa vyama
 vya siasa.
Kamati hiyo inayounga mkono muundo wa muungano wa 
Serikali tatu inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo, 
iliwasilisha mapendekezo hayo juzi katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya
 Katiba na kusema kuwa maoni hayo ndiyo mawazo ya Wazanzibari wengi.
Mapendekezo hayo yalisomwa na Mwakilishi wa Mji 
Mkongwe ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Ismail Jussa katika 
Kongamano la Katiba lililoandaliwa na kamati hiyo.
Msimamo wa kamati hiyo unaelezwa kuwa chanzo cha 
mmoja wa wajumbe wake, Mansour Yussuf Himid kuvuliwa uanachama wa CCM, 
Agosti 26 mwaka huu.
Akisoma mapendekezo hayo, Jussa alisema kwa kuwa 
Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar uliziunganisha nchi 
zilizokuwa huru, unatakiwa kuitwa Muungano wa Jamhuri za Tanzania, 
kusisitiza kuwa rasimu hiyo inatakiwa kueleza wazi kwamba nchi nyingine 
zinaweza kuingia kwenye muungano huo.
Alisema kamati hiyo imependekeza kuwa mambo ya nje
 yasiwe suala la muungano na badala yake nchi washirika zisimamie 
zenyewe eneo hilo.
Alisema kwa kuwa muungano umetokana na nchi mbili 
 zilizokubali kuungana na kuunda shirikisho,  msingi wa uraia wa 
shirikisho utokane na msingi wa mtu kuwa raia wa nchi mshirika na si 
kinyume chake.
“Kila nchi mshirika (Zanzibar na Tanganyika), 
ibakie na uraia wake na mtu kuwa na uraia wa nchi mshirika ndiko kumpe 
uhalali wa kuwa raia wa shirikisho,” alisema.
 Pia kamati imependekeza Rais wa muungano ambaye 
atakuwa na madaraka ya juu katika shirikisho lote kwa mambo yote ya 
Muungano, hivyo nchi washirika zinapaswa kuwa na haki sawa katika kutoa 
watu wa kushikilia Baraza la Mawaziri la Muungano, Bunge na Mahakama.
Alisema rasimu inatakiwa itamke wazi kwamba urais 
wa Muungano utashikwa kwa zamu na kwa kupokezana baina ya nchi washirika
 yaani Tanganyika na Zanzibar na kwamba Rais atangazwe mshindi baada ya 
kupata kura zaidi ya asilimia 50 kutoka Tanganyika na Zanzibar.
Alisema badala ya kuendeleza mfumo uliopo sasa wa 
Makamu wa Rais kupatikana kutokana na mgombea mwenza, marais wa nchi 
washirika (Zanzibar na Tanganyika) moja kwa moja wawe makamu wa kwanza  
na makamu wa pili wa Rais wa Muungano.
  
Mambo ya kuondolewa
Alisema uchumi si suala la Muungano hata katika 
Katiba ya sasa na kwamba nyenzo za kuendeshea na kusimamia uchumi wa 
nchi kwa maana ya sera za fedha na uchumi zimeendelea kudhibitiwa 
kupitia Serikali ya Muungano. 
“Vyombo vikuu vinavyosimamia sera hizo ambavyo ni 
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara 
ya Fedha ya Serikali ya Muungano vimekuwa vikifanya uamuzi na 
kuyatekeleza bila ya kuzingatia kuwa Zanzibar inategemea uchumi wa 
utoaji huduma na haiwezi kuwa sawa na uchumi wa Tanganyika ambao 
unategemea rasilimali,” alisema.
Akizungumzia usajili wa vyama vya siasa alisema 
Rasimu ya Katiba haipaswi kujumuisha suala la vyama vya siasa katika 
mambo ya Muungano na kwamba Zanzibar na Tanganyika zinatakiwa 
kuandikisha vyama vyake vya siasa.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
