Tuesday 1 October 2013

Obama afunga serikali Marekani kisa utata wa bajeti

Wapita njia wakikatiza jirani na jengo la Bunge la Marekani jana jioni, wakati wabunge wakiwa katika majadiliano makali ya kutafuta jinsi ya kuidhinisha bajeti ya serikali ya Obama. Mazungumzo yao hayakufanikiwa, hali iliyopelekea baadhi  ya huduma za serikali kusimama leo. PICHA | AFP 
Na Mwandishi Wetu, AFP

Posted  Jumanne,Oktoba1  2013  saa 10:39 AM
Kwa ufupi
Wafanyakazi katika vitengo mbalimbali vya serikali nchini humo waliodamkia maofisini leo alfajiri wamejikuta wakirudishwa majumbani, huku karibu 800,000 kati yao wakiambiwa wachukue likizo bila malipo mpaka muafaka utakapopatikana.
 

Washington. Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 17, utawala wa Rais Barack Obama umeidhinisha baadhi ya shughuli za kiserikali zisimamishwe  kuanzia mapema leo baada ya Bunge la nchi hiyo kuikataa bajeti yake, wakipinga mabadiliko ya kisheria ya sekta ya afya yaliyofanyika hivi karibuni.
Huku matumaini ya suluhisho la mtafaruku huo wa bajeti unaopambanisha wabunge wa chama tawala cha Democrat dhidi ya Republicans yakizidi kufifia, wachumi na wataalamu wa uongozi wameonya kuwa uamuzi wa kusitisha huduma ‘zisizo muhimu’ utaathiri uchumi wa Marekani kwa kiwango kikubwa.
Wafanyakazi katika vitengo mbalimbali vya serikali nchini humo waliodamkia maofisini leo alfajiri wamejikuta wakirudishwa majumbani, huku karibu 800,000 kati yao wakiambiwa wachukue likizo bila malipo mpaka muafaka utakapopatikana.
Wafanyakazi pekee watakaobakizwa ni wale ambao shughuli zao haziwezi simama, kama vile madaktari na manesi, waongoza ndege na wafanyakazi wa shirika la posta la Marekani.
Katika baadhi ya vitengo kama NASA – inayofanya tathmini za usafiri wa kwenda sayari nyingine na anga za mbali – zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi wote wamewekwa benchi katika kipindi hiki cha mtafaruku wa bajeti.
Vilevile huduma za utoaji hati za kusafiri na viza zinatarajiwa kusimama kwa kiwango kikubwa, na wasafiri toka nchi nyingine wanaambiwa watarajie foleni ndefu kidogo katika vituo vya uhamiaji kwa sababu wafanyakazi wengi wa kitengo hicho wamepumzishwa. (AFP)

SOURCE: MWANANCHI