Saturday, 5 October 2013

Waziri ahoji matumizi ya Sh 500mil kujenga soko Korogwe

05: Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Agrey Mwanri akiwaonyesha wananchi ufa za ukuta wa choo wa soko la Makuyuni Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, ambapo zaidi ya Sh500 milioni  zimeshatumika katika ujenzi wa soko hilo na bado halijakamilika na baadhi ya kuta za majengo  ziko hatarini kuanguka. PICHA | SALIM MOHAMMED 
Na Salim Mohammed, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Oktoba4  2013  saa 19:17 PM
Kwa ufupi
- Ujenzi wa soko la Makuyuni ambalo lilianza  mwaka 2008 na kutarajiwa kukamilika 2009, limeshindwa kukabidhiwa kwa halmashauri kwa kile kinachodaiwa kufanyika kwa ubadhirifu wa pesa za Serikali.


Korogwe. Naibu  Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri amemwagiza  Katibu Tawala  pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kuunda timu ya uchunguzi wa  ujenzi wa Soko la Makuyuni  unao daiwa kugharimu zaidi ya Sh500 milioni  huku  ujenzi huo ukishindwa kukamilika.
Ujenzi wa soko la Makuyuni ambalo lilianza  mwaka 2008 na kutarajiwa kukamilika 2009, limeshindwa kukabidhiwa kwa halmashauri kwa kile kinachodaiwa kufanyika kwa ubadhirifu wa pesa za Serikali.
Akizungumza mara baada ya kulikagua soko hilo, Mwanri alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Korogwe, Lucas Mweri kuhakikisha ndani ya siku 30 soko hilo  linafanya kazi ikiwa  ni pamoja na kukamilisha ujenzi wake.
"Ndugu wananchi hapa kuna tatizo na siamini kuwa Sh500 milioni zimeshindwa kujenga kasoko haka na kuomba katibu tawala kuunda timu ya uchunguzi juu ya hili soko ...mimi siamini,” alisema Mwanri.
Mwanri alisema hatokuwa tayari kuona pesa za Serikali na  nguvu za wananchi zikifujwa na wajanja na kusema kuwa mtu yeyote anayefanya ufisadi atachukuliwa hatua na kurejesha pesa alizochukua.
Alisema soko hilo ambalo hata kukamilika kwake ni utata limeanza kukatika kuta zake pamoja na vyoo kubomoka na hivyo kuitaka kamati ya ujenzi kuwaeleza wananchi mamilioni ya pesa zilivyotumika.
Akisoma taarifa ya ujenzi huo, Mhandisi  wa soko hilo, Lucas Mweri, alisema ili kuweza kukamilika kwa ujenzi huo zinahitajika Sh28 milioni zaidi zikiwa ni pamoja na kuweka vizimba vya biashara.
Alisema soko hilo limeshindwa kukamilika baada ya kuishiwa pesa na hivyo kuitaka halmashauri kuidhinisha kiwango hicho ili kuweza kukamilisha ujenzi huo na kuanza wananchi kulitumia.
Alisema soko hilo ambalo litatumika kuuzia stakabadhi ghalani pamoja na wananchi kuuza na kununua bidhaa, litakuwa ni mkombozi  wa wakulima wa mahindi na mbogamboga wakiwamo wa makabichi na nyanya.

SOURCE: MWANACHI