Na Lauden Mwambona, Mwananchi
Posted Jumapili,Septemba8 2013 saa 1:2 AM
Posted Jumapili,Septemba8 2013 saa 1:2 AM
Kwa ufupi
Mbeya. Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha)
mkoani Mbeya, limelaani tukio la vurugu lilitokea katika Ukumbi wa Bunge
mjini Dodoma, ambapo askari wa Bunge walimburuta na kumjeruhi Mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu wakati wakimtoa
nje ya ukumbi huo.
Mwenyekiti wa Bavicha mkoani humo, Joseph
Kasambala alisema tukio hilo limewashtua wapigakura wa mbunge huyo,
wanachama wa Chadema na wananchi wa mkoa huo kwa jumla.
Kasambala alidai kuwa chanzo cha vurugu hizo ni
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kutotaka kumpa nafasi Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alipoomba mwongozo ili
azungumze aliyokuwa nayo.
“Bavicha inalaani tukio zima, lakini pia inamtaka
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aache tabia yake ya kulivuruga Bunge
kwa kutozingatia kanuni za uendeshaji wa shughuli za Bunge,’’alisema.
Wakati huohuo, wakazi jijini humo, juzi
walionekana wakiwa katika vikundi wakijadili tukio hilo lililotokea
bungeni huku wengine wakisema limeidhalilisha nchi.
Mmoja wa walioshiriki katika mijadala hiyo eneo la
Mwanjelwa,Damasi Mwalyego wa Kabwe alisema kuwa tukio hilo ni la kwanza
katika historia ya Tanzania.
Alhamisi iliyopita, vurugu kubwa zilitokea bungeni
baada ya Naibu Spika wa Bunge, kuwaamuru askari wote waliokuwa bungeni
kumtoa nje Mbowe alipokataa kutekeleza amri ya naibu spika huyo.
Askari waliingia na walipotaka kumtoa, wabunge wa
upinzani waliamua kuwazuia jambo ambalo lilisababisha vurugu na
kusababisha Sugu kubebwa msobemsobe.
source: Mwananchi
source: Mwananchi