Na Faustine Fabian, Mwananchi
Posted Jumapili,Septemba8 2013 saa 1:1 AM
Posted Jumapili,Septemba8 2013 saa 1:1 AM
Kwa ufupi
Bariadi. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya
Bariadi jana wamewaweka kiti moto Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na
Mkaguzi wa Ndani kwa tuhuma za utendaji mbovu.
Watuhumiwa hao ni Mkurugenzi wa Halmashauri Abdallah Malela na Mkaguzi wa Ndani Jonais Shayo.
Mkurugenzi pia anatuhumiwa kuwa na uhusiano mbaya
na madiwani wenyewe, huku Mkaguzi wa Ndani akilalamikiwa kwa kushindwa
kuwasomea taarifa ya ukaguzi kwa mwaka mzima.
Hali hiyo ilijitokeza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hali ya uendeshwaji wa halmshauri hiyo.
Mkutano huo uliofanyika ndani ya ukumbi wa Bardeco mjini Bariadi, pia ulijadili suala la ukusanyaji mapato.
Kikao hicho kilichodumu kwa muda wa saa sita
kilikuwa chini ya Mkuu wa Mkoa huo Paschal Mabirti. Wengine
waliohudhuria ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Simon Maganga na Mkuu wa
Wilaya hiyo Erasto Sima.
Katika kikao hicho madiwani hao walimlalamikia
Mkurugenzi huyo kwa kuendesha shughuli za halmashauri bila ya
kuwashirikisha na kutofuata utaratibu wa kazi za Serikali.
Madiwani hao walibainisha kuwa tangu kuletwa kwa Mkurugenzi huyo, uhusiano wake na mwenyekiti umekuwa haupo.
Walidai kuwa pia walishangazwa kusikia kuwepo kwa
wakaguzi wa ndani ya halamshauri yao kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa, bila ya wao kupewa taarifa yeyote kuhusiana na ujio wa wakaguzi
hao.
Mbali na hilo madiwani hao walilalamika kwa
kutosomewa taarifa ya Mkaguzi wa Ndani wa halmshauri hiyo kwa mwaka
mzima na kutopewa sababu za msingi za kushindwa kusomewa taarifa hiyo.
Akijibu hoja hizo za madiwani, Mkurugenzi huyo
alikiri kutotoa taarifa kwa Mwenyekiti kuhusu ujio wa wakuguzi hao,
kutokana na kutopata barua kutoka katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa
kuhusu ujio wa wakaguzi hao kwa wakati.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa yeye wakati yupo
ofisini kwake hakuweza kuiona barua hiyo kwa wakati kutokana na kuwepo
kwa barua nyingi ofisini kwake, na kusababisha kutoifikia.
Hata hivyo madiwani hao walionekana kutokubaliana na majibu ya
Mkurugenzi huyo, kwa madai alikuwa akijua ujio wa waguzi hao, na kufanya
maksudi kutotoa taarifa kwa madiwani hao ambao ndiyo wenye mamlaka ya
juu ndani ya halmashauri.
Akitoa uamuzi wa sakata hilo Mkuu wa Mkoa
aliilaumu ofisi ya Katibu Tawala Mkoa kwa kushindwa kupeleka barua hiyo
kwa wakati na kuita kitendo hicho kuwa ni uzembe.
Alisema kama ofisi ya RAS ingepeleka barua hiyo
siku saba kabla mgogoro huo usingekuwepo na aliwaomba madiwani na
watumishi wa halmashauri hiyo kuwa na mawasiliano ya karibu na kuacha
malumbano.
source: Mwananchi
source: Mwananchi