Monday 16 September 2013

Bekele amuonyesha kivumbi Mo Farah

 16 Septemba, 2013 - Saa 04:21 GMT

Mwanariadha wa Ethiopia Kenenisa Bekele alimuonyesha kivumbi bingwa wa olimpiki Mo Farah kwa kumshinda katika mbio za Great North Run.
Fara mwenye umri wa miaka 30 na mkimbiaji wa Uingereza, alijitahidi kusalia mbele ya Bekele katika mita 400 za mwisho lakini akapokonywa ushindi katika msitirati wa mwisho kwa sekunde moja.
Mkimbiaji mwingine wa Ethiopia, Haile Gebrselassie, alimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuanza kuchoka katika maili 13.1 za mwisho.
"Sijafurahia sana leo lakini nilimaliza wa pili kwa mwanariadha shupavu.’’ Alisema Farah baada ya kumaliza kwa muda wa saa moja na dakika kumi.
Farah na Bekele walimaliza kwa mtindo wa aina yake kila mmoja akitaka kumaliza wa kwanza katika mashindano ya kufana na ambayo yalisubiriwa kwa hamu kuu katika mtaa wa Newcastle hadi South Shields.
Mabingwa hao watatu wa mbio, Farah, Bekele na Gebrselassie – wanajivunia ubingwa wa dunia kila mmoja na ubingwa wa olimpiki na walikimbia kwa karibu sana hadi Bekele, aliyekuwa anakimbia nusu Marathon yake ya kwanza , kujitenga nao.
Upande wa wanawake, Mkenya Priscah Jeptoo nusura avunje rekodi ya dunia baada ya kukimbia kwa kasi zaidi katika nusu Marathon ya wanawake.
Priscah mwenye umri wa miaka 29, na mshindi wa mbio za Marathon za London mwaka huu alichelewa tu kwa sekunde 5 kuweza kuvunja rekodi iliyowekwa na mkimbiaji wa Uingereza Paula Radcliffe miaka kumi iliyopita.
Meseret Defar alivunja rekodi ya Ethiopia alipochukua nafasi ya pili ingawa mbele ya Tirunesh Dibaba.

SOURCE: BBC SWAHILI