Monday, 4 November 2013

Kanuni mpya kuwaadhibu wabunge wanaozomea bungeni

4th November 2013
Naibu Spika wa Bunge,Job Ndugai
Hatimaye  utaratibu wa Bunge wa kuwa na kanuni za kuwadhibiti wabunge kimaadili ‘umeiva’, ambao pamoja na mambo mengine, zinazuia mbunge yeyote kufanya fujo au kuzomea akiwa bungeni.

Kadhalika, wabunge hawatotakiwa kujishirikisha na watu au vyombo binafsi kwa ajili ya kujipatia maslahi ya kifedha au mali yoyote yanayoweza kuathiri utendaji wa kazi za Bunge.

Utaratibu huo ambao umewekwa pia na mabunge mengi duniani, yakiwamo ya Jumuiya ya Madola, unalenga kuwawezesha wabunge katika utekelezaji wa majukumu yao ndani na nje ya Bunge ili kutoa mwongozo wa viwango vya maadili unaopaswa kufuatwa.

Vilevile, kujenga imani kwa wananchi na matumaini katika uadilifu ili kuimarisha misingi ya utawala bora.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusu taarifa za kuwapo kwa kanuni hizo, alisema suala hilo ni mchakato unaoendeshwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Hata hivyo, alisema licha ya kuitwa na kamati hiyo na kuelezwa kuhusu suala hilo, hadi sasa bado hawajawapelekea yaliyopendekezwa na kamati kuwamo kwenye kanuni hizo.

“Kwa hiyo, ni mapema kusema lolote kuhusiana na hilo,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka bungeni, kilieleza kuwa dhana kuu ya uandaaji wa kanuni hizo kwa wabunge, ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa shughuli zote za Bunge unatekelezwa kwa kufuata misingi ya uwazi, demokrasia na utawala bora.

“Kutokana na mahitaji ya kuwa na Maadili ya Viongozi, Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2003 ulipitisha azimio juu ya uandaaji wa kanuni za maadili. Nchi yetu imeridhia,” kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, chanzo hicho kimeeleza kuwa kanuni hizo hazitajihusisha na maisha ya mbunge au familia yake au pale mbunge anapotoa maoni yake ya kisiasa kwa kuzingatia kuwa yeye ni mwanachama wa chama cha siasa.

Pia hazitawahusu wabunge, ambao ni mawaziri wanapotekeleza majukumu yao.

Katika kanuni hizo, mbunge yeyote katika kutekeleza majukumu yake atakuwa na wajibu wa kuzingatia maadili mbalimbali, ikiwamo uadilifu.

Pia atatakiwa kuepuka mgongano wa maslahi, kuepuka vitendo vya rushwa, kutokuwa na ubinafsi na kutopokea au kutoa zawadi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Vilevile, atatakiwa kuweka wazi umiliki wa hisa, kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na wabunge wenzake pamoja na madaraka aliyonayo, kujenga mahusiano mazuri kati yake na watu wengine na kujiepusha na tabia za udhalilishaji wa jinsia.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, katika kanuni hizo pia mbunge anapaswa kutangaza maslahi yake binafsi yanayohusiana na nafasi yake kama mbunge na hapaswi kujiingiza katika migogoro inayohusiana na maslahi yake binafsi na ile ya umma.

Pia kilibainisha kuwa kanuni hizo zinamzuia mbunge kutoa au kupokea rushwa kwa namna yoyote ile kwa madhumuni ya kupitisha muswada wa sheria, hoja au jambo lingine lolote litakalowasilishwa au litakalokusudiwa kuwasilishwa bungeni au kwenye kamati za Bunge kwa kutumia ushawishi wake kama mbunge.

Aidha, chanzo hicho kilieleza kuwa katika kanuni hizo, mbunge pia hatatakiwa kufanya vurugu kwa kuzomea au vinginevyo zinazoweza kusababisha shughuli za Bunge kusitishwa.

Pia itakuwa marufuku kwa mbunge kuwa na nyaraka za siri zinazohusu utendaji wa serikali bila kibali cha mamlaka zinazohusika na kutunza siri hizo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mbunge hatatumia taarifa zozote atakazozipata kwa wadhifa wake wakati akitekeleza shughuli za Bunge au kamati ya Bunge kwa ajili ya kujinufaisha au kujipatia umaarufu au fedha.
 
CHANZO: NIPASHE