Monday, 23 September 2013

Boko Haram wafanya mashambulizi Abuja na Borno

 20 Septemba, 2013 - Saa 14:56 GMT
Vijana wanaotoa ulinzi kwa wenyeji dhidi ya Boko Haram
Vikosi vya usalama nchini Nigeria, visema kuwa vishambuliwa na wapiganaji wa kiisilamu , Boko Haram, mjini Abuja.
Vikosi hivyo vimesema kuwa watu kadhaa walijeruhiwa wakati wapiganaji hao walipowafiatulia risasi maafisa waliokuwa wanatafuta silaha haramu.
Mapigano haya yanakuja siku tatu baada ya shambulio lengine lililofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram katika jimbo la Borno.
Mwandishi wa BBC katika eneo hilo anasema kuwa baadhi ya watu hawajulikani waliko na kuwa huenda zaidi ya watu miamoja waliuawa.
Katika siku tatu zilizopita wafanyikazi katika sekta ya afya wamekuwa wakiondoa miili ya watu waliofariki kwenye malori.
Afisa mmoja alisema kuwa alihesabu mili themanini na saba.
Lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa miili zaidi inaweza kupatikana katika misitu na taarifa nyingine zinasema kuwa wapiganaji hao wanaodaiwa kuwa wa Boko Haram, waliwaua zaidi ya watu mia moja arobaini baada ya kuweka vizuizi vya barabarani na kuvalia magwanda ya jeshi wakijidai kuwa wanjeshi.
Jumanne shambulio karibu na Benisheik ni kati ya mabaya mno tangu hali ya hatari itangazwe Kaskazini Mashariki mwa Nigeria Mei.
Juhudi za kumaliza wapiganaji wa kiislamu zimefanya maeneo ya mijini kuwa salama lakini jeshi haliwezi kusema kuwa limeshinda vita kwani watu wanaoishi mashambani wamo katika hatari ya kushambuliwa.
Kwa sasa ni vigumu kupata habari kwani laini zote za simu zimekatwa katika juhudi za kuwasaidia wanajeshi kufaulu katika mpango wao.
Manusura wa mashambulio hayo yanayodaiwa kufanywa na Boko Haram wanasema kuwa wapiganaji hao walikuwa wamevalia sare za jeshi.
Waliwasili kwa magari , wakaweka vizuizi kati ya Maiduguri na Damaturu na wakaanza kuwaua watu.
Waliojaribu kukimbilia misituni  walifuatwa na kupigwa risasi.

.................................................................................................................................................
Mashambulizi yameongezeka tangu jeshi la Nigeria kuanza vita dhidi ya Boko Haram
Wapiganaji wa Boko Haram wamewaua watu 87 katika shambulio katika Jimbo la Borno nchini Nigeria.
Mashahidi wanasema kuwa wapiganaji hao waliteketeza nyumba kadhaa katika tukio hilo la kutisha mnamo Jumanne usiku.
Shambulio hili limetokea siku chache baada ya makabiliano makali kati ya jeshi na wapiganaji wa Boko Haram
Wanamgambo hao waliokuwa wamevelia magwanda ya jeshi, waliweka vizuizi barabarani nje ya mji wa Benisheik na kuwapiga risasi wale waliokuwa wanajaribu kutoroka.
Kwa mujibu wa taarifa za mashahidi , wapiganaji hao waliteketeza nyumba katika shambulizi hilo la Jumanne.
Kundi la Boko Haram, ambalo linapigania linachosema ni taifa la kiisilamu nchini Nigeria, limekuwa likifanya mashambulizi sawa na haya kuanzia mwaka 2009.
Jeshi linadai kuwa Agosti mwaka huu, kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau na naibu wake Momodu Bama waliuawa , ingawa hakuna taarifa za kujitegemea kuthibitisha hilo.
Mawasiliano katika jimbo la Borno, yamekumbwa na hitilafu, tangu mwezi Mei, wakati hali ya hatari, ilipotangazwa katika jimbo hilo na majimbo mengine mawili.
Lakini mashambulizi yameongezeka sana hivi karibuni tangu jeshi kuanza kukabiliana na kundi hilo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.


SOURCE: BBC SWAHILI