Kwa ufupi
Baada ya Ndugai kutangaza matokeo hayo na
kutaka shughuli za Bunge ziendelee, Mbowe aliposimama na kusema ana hoja
Naibu Spika alimwamuru akae chini.
Dodoma. Jana, Bingwa wa Dunia
wa uzani wa kati (super middle), unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi
Duniani (WBF), Francis Cheka alitembelea Bunge baada ya kutwaa taji hilo
karibuni na jana hiyohiyo, Bunge hilo lilishuhudia ngumi kavukavu
katika vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukumbi
wake.
Katika masumbwi hayo yasiyo rasmi, Mbunge wa Mbeya
Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anadaiwa kumpiga kichwa Askari
wa Bunge na kumchania sare na kung’oa kipaza sauti.
Mbilinyi jana alisema alikuwa anatafutwa na polisi
huku akisema hilo limemshangaza akidai kwamba yeye ndiye
aliyeshambuliwa na askari huyo.
Vurugu hizo zilitokea baada ya Naibu Spika, Job
Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe.
Katika vurugu hizo Mbilinyi alibebwa juujuu na polisi hadi nje ya ukumbi huku akiwa hana viatu.
Pamoja na tafrani hiyo, Ndugai alisema wakati
akihitimisha kikao cha Bunge kipindi cha asubuhi kuwa amewasamehe
wabunge wote waliohusika na kosa hilo la utovu wa nidhamu na kuwaruhusu
kurejea kipindi cha jioni kuendelea na Muswada wa Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Hata hivyo, wabunge wote CUF, NCCR-Mageuzi na
Chadema ambao baada ya tukio hilo walitoka nje ya ukumbi, hawakurejea na
baadaye walitoa msimamo wa pamoja wakisema hawatashiriki katika mjadala
huo.
Msimamo huo ulitolewa na Mbowe ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chadema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na
Mbunge wa CUF, Habib Mnyaa.
Mbowe alisema wameamua kususia majadiliano hayo kuonyesha msimamo wao wa kupinga kupitisha mambo yasiyo na masilahi kwa nchi.
“Hatuko tayari kushiriki katika uchakachuaji wa
Katiba... Matumizi ya nguvu ya polisi kamwe hayatatupatia Katiba nzuri,”
alisema. Alisema kambi rasmi ya upinzani inalaani vikali kitendo cha
Ndugai kuruhusu Bunge kunajisiwa kwa kuruhusu polisi kuingia ndani
kinyume na kanuni.
Mnyaa alisema kitendo cha wadau wa Zanzibar
kutoshirikishwa katika kutoa maoni yao katika muswada huo wa marekebisho
ni dharau kubwa.
Mbatia alisema Tanzania haiwezi kuingia Uchaguzi
Mkuu wa 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa kwa sababu tayari kuna mgongano
wa kikatiba kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu
Lissu alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi kutoa ushahidi kama Rais aliteua wajumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kulingana na mapendekezo ya taasisi zao.
Kuanza kwa tafrani
Sakata hilo lilianza saa 6:45 mchana muda mfupi
baada ya kukamilika kwa kura kuamua kama Bunge liahirishwe au la
kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Hamisi Seif
(CUF). Waliotaka liahirishwe walipata kura 59 na waliokataa 159.
Baada ya Ndugai kutangaza matokeo hayo na kutaka
shughuli za Bunge ziendelee, Mbowe aliposimama na kusema ana hoja Naibu
Spika alimwamuru akae chini.
Baada ya Mbowe kusisitiza ana hoja na kumwomba
Spika amsikilize ndipo Ndugai alipomwamuru atoke nje na alipokaidi
alisema:” Naomba askari wote waliopo katika mazingira haya (ya Bunge)
waingie ndani ya ukumbi wa Bunge”.
Baada ya kitambo kifupi, Mbowe akiwa bado amesimama alitoa maagizo atolewe nje: “Kiongozi wa upinzani atolewe nje.”
Polisi waliingia ndani ya Ukumbi wa Bunge lakini
Wabunge wa Kambi ya Upinzani kwa umoja wao, walimzinga Mbowe asifikiwe
na askari hao.
Baada ya kuona polisi wanaelekea kushindwa, Ndugai
alitoa maagizo mengine: “Askari hamjaletwa humu ndani kufanya
majadiliano mnatakiwa kuhakikisha kiongozi wa upinzani anatolewa nje”.
Alisema yeye ndiye anayeendesha kikao hicho hivyo lazima Mbowe atolewe nje.
Hapo ndipo wabunge hao wa upinzani walipoanza
kuimba: “Hatutaki kuburuzwa hatutaki kuburuzwa… hatutaki kuonewa,” huku
wakiendelea kumzinga Mbowe.
“Askari wote mliopo humu ndani naomba mnisikilize… Sasa naagiza kwa mara ya mwisho... nasema kiongozi wa upinzani atolewe nje.”
Ngumi zarushwa
Baada ya kauli hiyo ya Ndugai, ndipo polisi walipotumia nguvu
hasa kwa Mbilinyi na Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), Silvester
Kasulumbai.
Katika patashika hiyo, inadaiwa kwamba Mbunge wa
Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alipigwa ngumi ambayo
ilimfanya apepesuke hadi sakafuni.
Kilichomponza Mbilinyi ni hatua yake ya kusogelea Siwa. Polisi waliokuwa karibu, walimbeba juujuu hadi nje ya ukumbi.
Wakati akitolewa nje ya ukumbi, alijaribu kujizuia kwa kushika kipaza sauti kinachotumiwa na upande wa upinzani hadi kikang’oka.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Mozza Abeid,
alivuliwa hijabu katika vurumai hizo wakati polisi walipokuwa wakitumia
nguvu ili kumfikia Mbowe.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mbowe
aliamua kutoka nje huku akisindikizwa na polisi pamoja na wabunge wa
vyama hivyo na alipofika nje ya ukumbi alipokewa na polisi wa kawaida
waliomweka chini ya ulinzi kabla ya kumwachia baada ya ombi la Mbunge wa
Rombo (Chadema), Joseph Selasini.
Kutokana na hali ya mambo kuwa tete, askari wa
Bunge waliwaondoa wageni waliokuwa wamekaa katika kumbi za wageni
wakiwamo wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari huku baadhi ya
wabunge wa CCM waliokuwa na simu za kisasa za mkononi na kompyuta
mpakato (Ipad) wakichukua picha za tukio zima.
Inadaiwa kwamba baada ya kutoka nje ya ukumbi,
Mbilinyi alimtwanga ngumi mmoja wa askari waliomtoa kwa nguvu kabla ya
kuamuliwa na wabunge na polisi.
Wakati wote huo, wafanyakazi wa Bunge na wageni
walionekana wakiwa wamejikusanya katika makundi wakitafakari na
kushangaa yaliyokuwa yakitokea.
Balaa lilivyoanza
Akitumia Kanuni ya 69(1), Mbunge wa Mkoani (CUF),
Ali Hamisi Seif, alitaka kuahirishwa kwa mjadala wa Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 kutokana na
ukweli kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala ya Bunge ilipaswa
kukusanya maoni ya wadau mbalimbali nchini ikiwamo upande wa Zanzibar
jambo ambalo halikufanyika wakati wa maandalizi ya muswada huo.
“Ilipaswa sheria hii inapotaka kufanyiwa marekebisho iende tena
kulekule Zanzibar lakini jambo la kusikitisha kamati inayohusika na
masuala ya Katiba haikwenda. Mimi ni mjumbe wa kamati na tuliitwa Dar
lakini ratiba waliyotupa haikuonyesha kama tungekwenda Zanzibar,”
alisema. Mkosamali naye aliomba mwongozo kwa Spika, akisema kwa
kuzingatia matakwa ya kiapo cha Spika au Naibu alipaswa kuendesha Bunge
kwa haki bila upendeleo.
“Kanuni inasema Spika ama Naibu Spika ama
Mwenyekiti ataendesha shughuli za Bunge kwa haki, uadilifu, bila chuki
wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na Katiba ya nchi,” alisema na
kuongeza: “Kwa kuwa sisi tumekuweka hapo ili uendeshe Bunge kwa
uadilifu, usiburuzwe na chama chako na uzingatie miongozo yote kwa
wakati. Kwa nini usitumie mamlaka yako kuondoa muswada huu”?
Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenister Mhagama aliomba
mwongozo kwamba kwa kuwa bado kuna malalamiko basi waipe Serikali
nafasi ya kuthibitisha kwamba majadiliano ya kamati yalikamilika.
Lissu katika kuomba mwongozo wake, alisema
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala, Pindi Chana
alilidanganya Bunge alipowasilisha maoni ya kamati kwamba wadau wa
muswada huo walishirikishwa jambo ambalo alisema si kweli.
Lissu alisema hakuna Mzanzibari aliyefika mbele ya kamati hiyo kutoa maoni kuhusu muswada wowote.
Hata hivyo, Chana alijibu akisema wadau wa
Zanzibar walitoa maoni yao na kukabidhi nyaraka mbalimbali kwa Spika
kuthibitisha kauli yake hiyo. Alivitaja vyama vya Jahazi Asilia na ADC
kuwa vilihojiwa.
Kwa upande wake, Lukuvi alimshambulia Lissu kwa
kauli yake ya juzi kwamba uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ulikuwa na walakini. “Lissu
alisema jana (juzi) kwamba wapo wadau ambao walisema ijapokuwa
waliandikiwa barua ya kuwasilisha majina matatu kila moja ili Rais ateue
mmoja lakini hakuna mjumbe aliyeteuliwa”.
Alitaja majina ya walioteuliwa kuwa ni Maria
Kashonda (Tec), Jesca Mkuchu (CCT), Humphrey Polepole (Civil Society) na
Profesa Palamagamba Kabudi (Kundi la Wasomi).
Lukuvi aliwataja wengine waliopendekezwa na
taasisi zao na Rais kuwateua kuwa ni Mwamtumu Malale (Bakwata) na Dk
Sengondo Mvungi (NCCR) na Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema
alisema katika mchakato wa muswada huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ) iliwasilisha maoni yake mbele ya kamati.
Alisema Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi
Seif Ali Iddi aliwasilisha kwa kamati mapendekezo ya SMZ, Mei mwaka huu
na mapendekezo hayo ikiwamo uteuzi wa wajumbe 166 yalizingatiwa.
Waacha muswada, wapiga vijembe
Baada ya kurejea katika kikao cha Bunge cha jioni
jana, wabunge wa CCM waliopewa fursa ya kuchangia mjadala wa muswada huo
walitumia muda mwingi kuwajadili wabunge wa kambi ya upinzani.
source: Mwananchi
source: Mwananchi