Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 21:40 PM
Kwa ufupi
Matukio yaliyotokea Bungeni mjini Dodoma siku
mbili mfululizo sio tu yanatishia kutopatikana mwarobaini wa tofauti
zilizopo katika kambi hizo za kiitikadi, bali pia upatikanaji wa Katiba
Mpya na katika wakati uliopangwa.
Vurugu zilizotokea Bungeni juzi na jana wakati
wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba
wa mwaka 2013 zimeacha mashaka kama kweli nchi yetu itaweza kupata
Katiba Mpya ya kutupeleka kule tunakotaka kwenda. Vurugu hizo ni
mwendelezo wa hali ya kutovumiliana miongoni mwa wabunge kutokana na
kuweka mbele itikadi na misimamo ya vyama vya siasa badala ya
kutanguliza masilahi ya taifa.
Tunadiriki kusema kwamba kama hautatokea muujiza
katika muda mfupi ujao, hapa tulipofika ndio utakuwa mwisho wa maono na
ndoto za Watanzania za kupata Katiba Mpya waliokuwa wakiitafuta kwa muda
mrefu sasa.
Moja ya matatizo yanayochochea hali ya
kutosikilizana wakati wa mijadala ya muswada huo ndani ya Bunge ni kila
kambi kutaka kupata kila kitu, hivyo kushindwa kukubali ukweli kwamba
katika hali ya mapatano kama hayo ya mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya
kuna kupata hili na kukosa lile.
Matukio yaliyotokea Bungeni mjini Dodoma siku
mbili mfululizo sio tu yanatishia kutopatikana mwarobaini wa tofauti
zilizopo katika kambi hizo za kiitikadi, bali pia upatikanaji wa Katiba
Mpya na katika wakati uliopangwa.
Wabunge kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na
CUF walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge jana na juzi wakitaka muswada huo
uondolewe Bungeni kwa madai kwamba Wazanzibari hawakupewa fursa stahiki
kuutolea maoni. Upande wa Serikali na chama tawala ulishikilia msimamo
kwamba muswada huo hautaondolewa Bungeni kwa sababu wadau wote
walishirikishwa ipasavyo.
Wakati huohuo, mbunge wa kambi ya upinzani alisoma
vifungu vya muswada huo ambavyo alidai vilichomekwa na Serikali
kinyemela na kwamba havikuwa katika muswada waliopelekewa wabunge.
Kila kambi iliituhumu nyingine kwa kukwamisha
mjadala wa muswada huo ili Katiba Mpya isipatikane. Mtafaruku zaidi
ulitokea jana wakati Naibu Spika, Job Ndugai alipomwamuru Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutoka nje ya Ukumbi wa
Bunge kwa kukaidi maagizo yake ya kukaa chini. Ghasia kubwa zilizuka
kabla ya kiongozi huyo kutolewa nje, huku akifuatana na wabunge wengi wa
upinzani.
Kama ilivyokuwa juzi, wabunge wa CCM jana pia
waliendelea na mjadala wa muswada huo mara baada ya wabunge wa upinzani
kutoka nje.
Hata hivyo, badala ya kujadili muswada huo,
wabunge wengi wa CCM walijielekeza katika kuwapiga vijembe wabunge wa
upinzani waliotoka nje, hivyo kusababisha hali inayoweza kuongeza
msuguano na kuweka mazingira ya kutowawezesha wabunge kuwa kitu kimoja
katika kujadili muswada huo kwa kina na umakini kwa lengo la kupata
msimamo wa pamoja.
Sisi tunadhani zinahitajika nguvu za ziada
kulirudisha Bunge ndani ya mstari kama tunataka kupata muswada
utakaokubalika.Kuna msemo usemao wengi wape, lakini wachache nao
wasikilizwe. Maana ya msemo huo ni kwamba sio lazima walio wengi wakati
wote kuwa na maoni sahihi, bali pia kuna wakati walio wachache nao huwa
na maoni sahihi.
Kwa mfano, ukweli wa usemi huo tuliushuhudia
wakati Tume ya Nyalali kuhusu kuwapo au kutokuwapo vyama vingi ilipotoa
ripoti kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania waliotoa maoni yao
walitaka utawala wa chama kimoja. Pamoja na hali hiyo, Tume hiyo
ilipendekeza uwapo wa vyama vingi na hatimaye ikawa hivyo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi