Posted Jumapili,Septemba22 2013 saa 13:16 PM
Kwa ufupi
Tido Mhando amefanya kazi ya utangazaji kwa
zaidi ya miaka 40. N i kipindi kilichomwezesha kufanya na kuona mengi
kwenye kazi yake hiyo. Kwa hiyo, katika makala zake hizi za kila wiki,
anadokeza tu baadhi ya mambo hayo. Sasa endelea…
Niliamka asubuhi ya Jumapili, Februari 3 mwaka
ule wa 1974 nimechokachoka. Nilikuwa na ile aina ya uchovu ambayo kule
kwetu Bonde tunaiita “mavune”, unaosababishwa na shughuli kubwa. Naam,
nilikuwa na shughuli kubwa usiku uliotangulia, au niseme siku yote ya
jana yake, ambayo ilikuwa ya heka heka nyingi.
Jumamosi ile ndiyo siku ambayo sisi tuliokuwepo
kule Christchurch, New Zealand, tulimshuhudia Mtanzania Filbert Bayi
akiweka rekodi mpya ya dunia kwenye mbio za mita 1,500, tukashangilia
kupindukia.
Halafu ikawa ndiyo siku yangu ya mwisho ya kutuma
ripoti za michezo ile ya Nchi za Jumuiya ya Madola. Nikawa nimeamua
kuchapa kazi ya nguvu ya kweli kweli, maana nilikuwa nautua mzigo.
Hatimaye, usiku kukafanyika tafrija ya kuagana
ambayo ilikuwa ya kukata na shoka. Waliokula wakala, waliokunywa
wakanywa na wapenzi wa muziki na wao wakaselebuka kefu yao; ili mradi
ilikuwa usiku wa kujimwaga. Usiku wa furaha.
Ndiyo maana siku hiyo ya pili ikawa ya mavune.
Pamoja na hali hiyo, nilikuwa na mambo kadhaa muhimu ya kukamilisha
kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani keshoye.
Kwanza nilikuwa niende kwenye ofisi za Shirika la
Ndege la Qantas kuulizia sanduku langu ambalo nilikuwa sijalipata hadi
wakati huo, sanduku ambalo lilipotea njiani wakati nikija.
Hawa jamaa waliniambia nisiwe na shaka hata
kidogo, lingepatikana tu kabla hata ya siku za michezo kumalizika.
Lakini sasa kukiwa kumesalia saa chache tu nisanzue, hali bado ilikuwa
ya utata mtupu.
Tayari walikuwa wamenipatia fedha ya kuridhisha,
ili niweze kujinunulia mahitaji muhimu na hasa mavazi, na hii
ilinisaidia sana. Nilijinua mavazi, si ya kunipamba tu vyema wakati wote
wa michezo, lakini pia nikihakikisha ni nguo za uhakika ambazo
zingenifanya nilibabaishe jiji nirejeapo Dar.
Kwa kuwa hii pia ilikuwa siku ya Jumapili, siku ya
mapumziko, nilitaka nifike ofisi za Qantas mapema, maana sikuwa hata na
uhakika kama ningekuta mtu yeyote wa kunisaidia. Nilikuwa na wasiwasi,
maana kama nisingefanikiwa kupata msaada unaofaa siku hiyo, basi kila
kitu kingesambaratika.
Niliondoka hotelini kwangu mapema asubuhi ile na
kwenda kwenye ofisi za Qantas. Nilikuwa nimepewa maelekezo ya jinsi ya
kuzipata na hivyo nikawasili hapo kwa rahisi.
Nilifurahi sana kukuta ofisi zikiwa wazi na kwa
hakika, nilipokewa vizuri sana, hasa baada ya wenyeji wangu kutambua ya
kwamba nilikuwa natoka Tanzania. Walikuwa bado na shauku ya kujua zaidi
juu ya ushindi wa Filbert Bayi.
Kwa muda walijisahau kuhusu kile nilochokifuata
mapema asubuhi ile, badala yake wakawa wanajadili tu kuhusu pata-shika
hasa baina ya mwanaraidha wao John Walker na Filbert Bayi.
Hapana shaka gumzo kuhusu mchuano ule ndilo lililokuwa
likitawala mazungumzo mengi nchini mle, hasa kwa kuwa magazeti yote ya
Jumapili hiyo yalikuwa vilevile yametawaliwa na stori hiyo, ikiwa ni
pamoja na picha kadhaa za kusisimua.
Hatimaye walirejea kwenye shughuli za kazi,
wakaniuliza shida yangu. Niliwafahamisha kwa kifupi tu, na palepale
wakaelewa shida yangu, kisha wakanifahamisha ni nini cha kufanya.
Kwa jumla tayari shida yangu ya kupotea kwa
sanduku ilikuwa imeshapatiwa ufumbuzi. Ilishakubalika kwamba kulikuwepo
na uwezekano mdogo sana wa sanduku hilo kupatikana, kwa hiyo
lilichobakia, kwa kuzingatia sheria za safari za Shirika la Ndege la
Qantas, lilikuwa ni kunilipa fidia ipasavyo.
Kutokana na hali hii, waliniambia kuwa mipango
ilikwisha kukamilishwa kwa mimi kulipwa fidia keshoye nitakapofika
jijini Melbourne, Australia, wakati nikiwa njiani kurejea nyumbani.
Walinieleza kuwa nitakapofika hapo, ambako ndipo
yaliko makao makuu ya shirika hilo la ndege, nitamkuta ofisa wa shirika
hilo atakayekuwa ananisubiri na ambaye atanipeleka kwenye ofisi husika
za malipo. Kwa hiyo niliondoka ofisini hapo nikiwa na matumaini makubwa
ya kupata malipo yangu.
Niliondoka haraka haraka na nikiwa mwenye furaha
tele, nikaamua kukamilisha jukumu langu jingine kubwa ambalo nilikuwa
nimejipangia kulikamilisha kabla ya kuondoka jijini humo.
Kwa kuwa nilikuwa nafahamu kwamba ningefanya
harusi siku chache tu baada ya kurejea nyumbani, nilikuwa
nimejitayarisha kununua pete zote za harusi huko huko New Zealand.
Wazee walikuwa wameniarifu mapema kuwa ilikuwa ni
wajibu wangu kununua pete, hivyo nilikuwa nimejitayarisha kwa hilo,
tatizo likawa kukosa muda wa mapema wa kutimiza jukumu hilo.
Haraka nilisimamisha teksi na kumfahamisha dereva
nilikotaka kwenda. Nilifika mahali ambako kulikuwa na maduka chekwa ya
vito. Nilihangaika kidogo na mara nikafanikiwa kupata duka lililokuwa na
aina ya pete nilizokuwa nikizitafuta.
Nilichagua mbili zilizonipendeza na kuzilipia kama
ilivyotakiwa na wauzaji wakaniambia kwamba, ili kuweka kumbukumbu,
ingefaa kuziandika kwa ndani, tarehe iliyokuwa imepangwa kufanyika
harusi: 24.02.74.
Niliondoka dukani hapo nikiwa nimefarijika kwamba
nilikuwa nimekamilisha jukumu langu jingine muhimu. Ila ghafla
nikakumbuka kwamba nilikuwa nawajibika kujinunulia sanduku jingine la
kusafiria. Nikafanya hivyo haraka haraka na nilihakikisha kuwa na nina
sanduku bora kuliko lile lililopotea.
Nilirejea hotelini kwangu na kujipumzisha kwa
kuangalia televisheni ambayo nilikuwa nimeanza kuizoea na kuikubali kama
chombo kizuri mno kwa kutangazia habari. Nikawa nawaza na kujiuliza ni
lini Tanzania nayo itakuwa na kituo chake cha televisheni.
Jambo la kupendeza zaidi ni kwamba siku nzima ile vipindi pekee
vilivyokuwa vikionyeshwa mara kwa mara vikuwa vinahusu michezo
iliyomalizika, na hasa mbio zile za mita 1,500.
Sijui hata ilikuwakuwaje, lakini nilipitiwa na
usingizi na niliposhtuka kulikuwa kumekaribia saa saba usiku, huku bado
televisheni ikiwa bado inaendelea na matangazo. Niliizima haraka haraka
na kulala vizuri kwa kuwa nilifahamu siku inayofuata ningewajibika
kuamka asubuhi na mapema kwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya safari
kurejea nyumbani.
Ilikuwa ni siku ya Jumatatu; nikaamka mapema
nikitilia maanani kuwa nilibaki na muda mfupi sana wa kuendelea kuwepo
New Zealand na kwamba baada ya muda mfupi tu ningeanza safari ya
kuelekea uwanja wa ndege, tayari kwa kuondoka.
Ilikuwa mnamo saa moja asubuhi tulipofika uwanja
wa ndege uliokuwa umefurika watu, hasa wanamichezo mbalimbali waliokuwa
wanarejea makwao baada ya kukamilisha wajibu wao, nami nikaenda kuungana
na wanariadha wa timu ya Tanzania waliokuwa wamechangamka kweli kweli.
Tulikamilisha haraka taratibu zote za uhamiaji na punde tukawa tayari
kwa safari yetu ndefu ya kurejea nyumbani kupitia Australia.
Nilipokuwa ndani ya ndege, wakati huo inapaa
taratibu, nilichungulia kupitia dirishani na kwa chini, nikauona uwanja
wa QEII Park, mahali ambapo Filbert Bayi wetu aliipatia heshima kubwa
Tanzania. Nikawa nawaza: Sijui tutapokewa vipi wakati tutakapotua jijini
Dar es Salaam!
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI