Monday 16 September 2013

Lowassa: Machifu wana nafasi ya kuimarisha maadili

15th September 2013
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema machifu, watemi na wakuu wengine wa kimila wana nafasi kubwa katika kuzuia mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.
Akizungumza mjini Tabora jana wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 124 ya shujaa wa Unyanyembe, Chifu Isike Mwana Kiyungi, Lowassa alisema wakuu hao wa kimila wakitumika wanaweza kusaidia masuala mbalimbali katika jamii.


"Hawa machifu wanaweza kabisa kusaidia tatizo hili, mimi kule kwetu Monduli ni Laigwanan mkuu...kuna wakati hali ya maambukizi ya Ukimwi yalikuwa makubwa sana kwa wamasai, sasa nikawaita malaigwanan wenzangu nikawaomba waondoe baadhi ya mila zinazochangia hali ile, tukakubaliana na kupita kijiji kwa kijiji kuelezea, na kweli ikaleta mafanikio makubwa sana maambukizi yale yakapungua," alisema Lowassa.
Alipongeza hatua iliyofikiwa ya kuenzi kumbukumbu hiyo na kusema kizazi cha sasa kina kila sababu ya kuiga mfano wa Chifu Isike wa kutetea utu wake.
"Chifu Isike alisimama imara kutetea utu wake dhidi ya wakoloni, alionesha ushupavu, sasa kizazi hiki ni lazima kiige mfano huu wa kutetea utu wa Mtanzania dhidi ya wadhalilishaji," alisema Lowassa.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji cha Itetemia ambako ndiko iliko Ikulu ya chifu huyo wa Unyanyembe, aliyepigana dhidi ya majeshi ya Mjerumani Von Prince (Mwana sakaraga) kuanzia mwaka 1889 hadi 1893.
Lowassa aliwataka wakazi wa Tabora kuwekeza mji wao kitalii kutokana na historia kubwa ya mkoa huo.
"Tabora ina historia kubwa sana katika uhuru wa nchi yetu, viongozi wengi nikiwemo mimi tumesoma hapa, neno ikulu asili yake ni hapa tulipo, ikulu ya chifu Isike, chama changu wakati huo TANU kina historia na mjini huu, sasa hivi vitu ni utalii tosha, kwa hivyo naunga sana mkono hatua ya kujenga mnara wa kumbukumbu ya chifu Isike, muitangaze ili kupata watalii wa nje na ndani," alisema.
Mapema Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alitawazwa kuwa Chifu wa Nyanyembe na kuteuliwa kuwa mlezi wa watemi wote wa Unyanyembe. Aliweka jike la msingi la ujenzi wa mnara wa kumbukumbu ya shujaa huyo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na machifu na watemi kutoka makabila mbalimbali, pamoja na watu wengine mashuhuri katika kabila la kinyamwezi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI